Wednesday, January 25, 2017

Wateja Tigo Pesa kupata 5.82bn/-gawio la 11 la faida la robo mwaka

Mkuu wa Kitengo cha fedha cha Fedha TigoPesa Christopher Kimaro (kushoto) akiongea na waandishi wa habari(hawapo picha) wakati wa kutangaza gawio kwa wateja wa Tigo Pesa jijini Dar Es Salaam jana. Kulia ni Mkuu wa Huduma za Fedha kwa Simu, Ruan Swanepoel .

Mkuu wa Huduma za Fedha kwa Simu, Ruan Swanepoel akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari katika mkutano wa waandishi wa habari 

Dar es Salaam, Januari 23, 2017 - Kampuni inayoongoza kwa maisha ya kidijitali Tigo Tanzania imetangaza gawio jingine la malipo ya faida ya robo mwaka la shilingi bilioni 5.82 ambalo kampuni inagawa  kwa wateja  wote wanaotumia huduma ya pesa kwa kupitia simu. Gawio hilo ni kipindi cha robo ya nne ya mwaka  uliyoishia Desemba 31 2016.
 
Akizungumza katika mkutano wa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, Mkuu wa Huduma za Fedha kwa Simu, Ruan Swanepoel alisema  kampuni hiyo kwa ujumla  imeshawalipa wateja wake wanaotumia huduma za fedha kwa njia ya simu  jumla ya shilingi bilioni 58.10 sawa na dola za Marekani milioni 26.3 kama malipo ya robo mwaka tangu kuanzishwa malipo hayo ya riba na Tigo Julai 2014.
 
Swanepoel alisema kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka riba iliyotolewa kama gawio ilipanda  hadi asilimia 11 ikiwa ni matokeo mazuri ya viwango vilivyopokelewa katika mfuko wa fedha  uliowekwa katika benki mbalimbali za biashara nchini Tanzania.
 
“Riba hii ni malipo kwa wateja binafsi, mawakala wa reja reja, mawakala wakubwa na wabia wengine wa kibiashara wa Tigo ambao kila mmoja anapokea malipo kulingana na thamani ya fedha zilizohofadhiwa katika pochi ya kielektroniki ya Tigo Pesa,” Swanepoel alifafanua.
 
Swanepoel aliongeza, “Tunayo furaha sana kuwatangazia  ongezeko hili la gawio la riba kwa mara ya 11 mfululizo,  hali inayoleta nafuu kwa mamilioni ya watumiaji wa Tigo Pesa kwa kuwasaidia kukabiliana na majukumu mbalimbali ya kifedha. Hii inaonesha jinsi tulivyojikita katika  kutoa huduma ya fedha inayowafikia wateja wetu na nchi kwa ujumla  kupitia huduma yetu ya Tigo Pesa.”
  
Alibainisha kuongezeka kwa faida kuwa ni kutokana na kuboreshwa kwa mazingira ya soko na kasi ya kuongezeka kwa idadi ya watumiaji wa Tigo Pesa kama kichocheo kikubwa katika ongezeko kubwa la gawio la riba hususani kwa upande wa wafanya biashara. Tigo Pesa hivi sasa ina mtandao mkubwa wa wafanya biashara zaidi ya 55,000 wanaowezesha malipo ya miamala  nchini kote.
 
Kama ilivyokuwa awali kwa mujibu wa Swanepoel malipo kwa wateja  yanakokotolewa kwa kuzingatia wastani wa salio la kila siku  linalokuwa katika pochi ya kielektroniki ya simu na kwamba mgawanyo wa gawio hili la faida  ni kulingana na waraka wa Benki Kuu uliotolewa Februari 2014.

Tigo Pesa inakuwa ni huduma ya kwanza ya fedha kwa njia ya simu  duniani  ambayo mwaka 2014 iligawa gawio la hisa  lililozalishwa  kutoka katika akaunti ya dhamana ya pesa katika simu  katika mfumo wa gawio wa robo mwaka kwa wateja wake.

No comments: