Friday, January 13, 2017

Zitto Kabwe:Rais Magufuli awe makini na wasaidizi wake

Jana na juzi  magazeti ya Mwananchi na The Citizen yameandika kuhusu kuhusika kikamilifu kwa Waziri wa Nishati na Madini kwenye mchakato mzima wa kupandisha bei ya umeme nchini. Magazeti hayo yalitoa ushahidi wa maandishi kwamba Waziri wa Nishati na Madini alimwandikia Waziri wa Fedha kuhusu mpango wa kupandisha bei ya umeme nchini.

Jana Wizara ya Nishati na Madini imetoa Taarifa kwa vyombo vya habari kukanusha habari za magazeti hayo. Vile vile Waziri amesambaza SMS kukanusha kushiriki kwake. Katika SMS yake hiyo Waziri amefikia hatua ya kutoa SIRI za Baraza la Mawaziri jambo ambalo ni kinyume cha kiapo chake na kinyume cha sheria.

SMS hiyo inasema " HAIWEZEKANI MUHONGO AKUBALI BEI KUPANDA (1) Mwaka 2012, 2014 na kwenye vikao vya World Bank na AfDB Muhongo aliwakatalia suala la bei Kupandishwa hadi Mramba akamshitaki kwenye Baraza la Mawaziri (2) Muhongo ndiye alishawishi TANESCO iondoe Malipo ya Maombi ya umeme na Service Charge. (3) EWURA na waliotumbuliwa TANESCO na Wizarani wamenunua wasemaje na magazeti ya Kenya. Wapo wasiopenda zoezi la kufuta rushwa na wizi ndani ya TANESCO." Kwamba Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO alimshtaki Waziri wake kwenye Baraza la Mawaziri ni jambo jipya na dhahiri kwamba katika kujitetea Waziri ametoa SIRI za Baraza la Mawaziri. Adhabu ya kosa hili ni kufukuzwa Uwaziri.

Maelezo ya Wizara kuhusu bei ya Umeme yanaonyesha kuwa ni uwongo kwa lengo la kujitetea kwa Rais. Leo nilikuwa ninasoma Taarifa ya IMF ya tarehe 12 January 2017. Taarifa hii ( http://www.imf.org/external/pubs/ft/scr/2017/cr1713.pdf ) inaonyesha kuwa Serikali na IMF wamekubaliana kupandisha bei ya umeme ili kuliokoa Shirika la TANESCO. Wizara ya Fedha kamwe haiwezi kukubaliana na IMF bila Taarifa kutoka Wizara ya kisekta.

Rais John Pombe Magufuli awe makini Sana na Wasaidizi wake. Wanamdanganya wanapoona wamekosea ili kusukumia lawama wengine. Kwenye hili la bei ya umeme ushahidi ulio mbele yetu unaonyesha kuwa Wizara ya Nishati na Madini ilihusika moja kwa moja kupandisha bei ya umeme. 

Rais anapaswa kuchukua hatua kali dhidi ya wasaidizi wanaopiga majungu wenzao ili iwe fundisho kwa wengine. Tunajua na kuunga mkono nia njema ya Rais kutaka wanyonge kuwa na umeme nafuu. Pia tunajua Rais ni msema kweli na haonei mtu. Kwenye hili la TANESCO ameonea mtu kwa kumwadhibu kwa makosa ya watu wengine wenye mamlaka zaidi yake.

No comments: