Wednesday, February 1, 2017

FAIDA ZA KUWAHI KAZINI MAPEMA


Na Jumia Travel Tanzania

Kuamka asubuhi ni mtihani mgumu ambao umewashinda watu wengi, si wafanyakazi, wanafunzi, wafanyabiashara au watu wa kawaida. Watu wengi hulazimika kuamka asubuhi kwa sababu inawalazimu kufanya hivyo vinginevyo wasingefanya hivyo.

Wataalamu mbalimbali wa afya, watu mashuhuri na waliofanikiwa katika shughuli zao, wametoa ushuhuda kuwa ukitaka kufanikiwa ni lazima ujijengee mazoea ya kuamka asubuhi na mapema. Jumia Travel inapenda kukushirikisha faida zifuatazo za kuwahi mapema kuelekea kwenye shughuli zako.

Inakuwezesha kuwahi usafiri
Hakuna asiyefahamu kwamba usafiri ni changamoto kubwa katika maeneo mengi duniani, sio barani Afrika peke yake. Iwe unatumia usafiri binafsi au wa umma, lazima utakumbana na aidha foleni au upatikanaji wa haraka wa usafiri. Jambo zuri ni kuwa wataalamu na washauri mbalimbali walikwishaliona hilo mapema na kupendekeza namna ya kulikabili. Ukiwahi asubuhi utajiepusha na foleni na kupata usafiri wa uhakika utakaokufikisha ofisini mapema tofauti na ukichelewa ambapo kila mtu amekwishaamka. 

Ni vizuri kwa kuanza siku
Kuwahi kazini mapema ni jambo ambalo linaleta amani kubwa sana moyoni kwa sababu unakuwa huna hofu ya jambo lolote. Ukiwahi itakuwezesha kujiandaa mapema tofauti na ukichelewa ambapo utakuwa unawaza mambo mengi kama vile, kazi ambazo hukuzimaliza jana au kumkuta bosi wako akiwa ameshafika tayari.

Kujibu barua pepe na simu zilizoingia wakati wewe haupo
Ulimwengu wa biashara hauna mipaka ya kwamba simu au barua pepe ziingie muda gani. Hivyo unaweza kujikuta unazipokea wakati muda wa kazi umekwisha na ukahitajika kuzijibu. Muda pekee wa kufanya hivyo ni pale unapowahi ofisini mapema, kwa kufanya hivyo utajikuta pindi muda wa kawaida wa kuanza kazi unawadia, wewe umekwishazijibu na kuanza upya na makujukumu yaliyoko mbele yako. 

Kuwavutia wakuu wako wa kazi
Wakati mwingine huna budi kuwaonyesha wakuu wako wa kazi kwamba unafaa na unastahili kwa majukumu uliyopewa. Kuchelewa kunaweza kutafsiriwa kwamba hauwezi kumudu majukumu mengi kama ukipewa ikiwa suala la kuwahi tu linakushinda. Hivyo kama ulianza tabia ya kuwahi basi endelea kufanya hivyo kwani jitihada zako zinaonekana kwa wakuu wako wa kazi.

Kujitengenezea mazingira mazuri ya utulivu
Asilimia kubwa ya ofisi nyingi huwa hazina utulivu pindi muda wa kazi unapofika kutokana na kuwa na wafanyakazi wengi huku kila mtu akiwa na majukumu yake ya kuyatimiza. Lakini kama ukiwahi asubuhi na mapema utaikuta ofisi katika hali ya utulivu kwa sababu wafanyakazi wengi wanakuwa hawajafika. Hii itakupa fursa ya kufanya kazi zako zile zinazohitajika kwa umakini wa hali ya juu na ustadi zaidi.

Unapata muda wa kupata kifungua kinywa na kufanya mazoezi
Sio ofisi zote mabosi ni waelewa ambao watakuwa wanakuruhusu kupata kifungua kinywa muda wa kazi. Katika ulimwengu huu wa biashara wafanyakazi wengi hulipwa kulingana na muda wanaoutumia ofisini. Kwa hiyo, kula wakati muda wa kazi umekwishafika ni upotezaji wa muda na huweza kutafsiriwa kwamba hauzingatii taaluma yako. Lakini ukiwahi kuamka mapema, unaweza kupata muda mfupi wa kupata kifungua kinywa na kufanya mazoezi na kuuweka mwili wako thabiti kwani sio wote wanaopata muda baada ya kutoka kazini.

Inakupa fursa ya kupangilia siku yako
Unapowahi ofisini asubuhi na mapema unapata muda wa kutosha wa kutafakari na kupangilia majukumu yanayokukabili siku uliyonayo. Mfanyakazi makini ni lazima azingatie muda wa kila kazi anayopewa kwani mwisho wa siku unalipwa mshahara kutokana na majukumu uliyoyatekeleza na sio kuhudhuria kazini.

Zipo faida nyingi ambazo zimekuwa zikishirikishwa na watu mbalimbali lakini hazitokwisha kama tukiamua kuzielezea zote hapa.  Wapo wanaodai pia kuwahi mapema husaidia kujenga hali ya kufanikiwa pamoja kuwa na utayari wa majukumu yako. Kwa faida hizo chache Jumia Travel inaamini kama ulikuwa umeshaanza kujenga mazoea ya kufanya hivyo utaendelea na kama hujaanza basi huu ndio muda muafaka ikiwa ndio mwaka bado mchanga.

No comments: