Mara baada ya wiki iliyopita Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF) kuipongeza timu ya Lipuli ya Iringa, leo Jumanne Februari 21,
mwaka huu kwa mara nyingine, Rais wa TFF Jamal Malinzi amezipongeza kwa mpigo,
timu za Singida United ya Singida na Njombe Mji ya Njombe kwa kupanda daraja.
Juma lililopita, Rais Malinzi aliuandikia barua uongozi wa
Lipuli ya Iringa kwa mafanikio ya kupanda daraja msimu huu kutoka Ligi Daraja
la Kwanza hadi Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) msimu wa 2017/18 kama
alivyofanya sasa kwa Singida United ya Singida na Njombe Mji ya Njombe.
Katika salamu hizo kwa Lipuli ambayo imepanda daraja baada ya
kusota miaka 17 iliposhuka daraja, Rais Malinzi alimwandikia barua Katibu Mkuu
wa timu hiyo akisema: “Nitumie fursa hii kukupongeza wewe, uongozi wa klabu
yako, benchi la ufundi na wadau wote wa timu ya Lipuli kufuatia kupanda daraja
kwenda Ligi Kuu.
Kama ilivyotokea kwa Lipuli, Rais Malinzi pia kwa moyo mkunjufu
amewaandikia barua, viongozi wa Singida United ya Singida na Njombe Mji ya
Njombe, akisema: “Pia nanyi nawapongeza kwa kupanda daraja. Bila shaka ni kazi
kubwa imefanyika ikihusisha kujitolea kwa ari na mali kuhakikisha mnafika hapa
mlipo.”
Pamoja na salamu hizo za kuwapongeza, Rais Malinzi hakuacha
kuziusia timu hizo akisema: “Rai yangu kwenu ni kuongeza juhudi na kuendesha
klabu kwa weledi mkubwa zaidi ili muweze kuwa washindani wa kweli katika ligi
(Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara).”
No comments:
Post a Comment