Mbunge wa Chalinze mkoani Pwani kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) Ridhiwan Kikwete, amesema siasa ni shule ambayo haina mwisho na ndiyo maana anaendelea kujifunza mengi kutoka kwa wanasiasa wenzake hususani waliomtangulia bila kujali chama.
Kikwete alitoa ujumbe huo jana mara baada ya kukutana na kuteta na aliyekuwa mgombea urais kupitia CHADEMA katika uchaguzi wa mwaka 2015, Edward Lowassa katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam, wakati wa mchezo wa ligi kuu Tanzania Bara kati ya Simba na Yanga.
Kikwete ambaye ni mwanachama na kiongozi ndani ya klabu ya Yanga, alimfuata Lowassa alipokuwa amekaa na kufanya naye mazungumzo ambayo hajayaweka wazi, na kisha kurudi sehemu yake huku akishuhudia timu yake ya Yanga ikilala mabao 2-1.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Kikwete ameandika "Siasa ni shule ambayo haina mwisho. nahisi bado niko shule ya msingi na ninaendelea kujifunza".
Pia mbunge huyo alitumia fursa ya mchezo huo kukutana na mbunge wa Hai ambaye pia ni mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na kuzungumza naye mawili matatu.
Kikwete na Mbowe wote ni wapenzi wa Yanga, kwahiyo bila shaka wote waliondoka uwanjani hapo wakiwa na majonzi ya kipigo kutoka kwa Simba.
Mbali na hao, mechi hiyo pia iliwakutanisha mahasimu wengine katika siasa za Bongo, ambao ni Nape Nnauye na Edward Lowassa waliokuwa wamekaa katika eneo moja, ambapo Nape ndiye aliyekuwa mgeni rasmi katika mchezo huo
No comments:
Post a Comment