Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Jamal Emil Malinzi ameelezea mikakati mbalimbali ya maendeleo
ya soka nchini akisema hiyo ndiyo sababu ya Kamati ya Utendaji kubuni na kuunda
Mfuko wa Maendeleo ya soka.
Katika Risala yake aliyoitoa jana
mbele ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mheshimiwa Nape Nnauye
katika uzinduzi wa mfuko huo, Rais Malinzi alisema wamefanya hivyo kwa lengo la
kutimiza ndoto za Tanzania kushiriki michuano mbalimbali ya soka.
“Kwa kipindi kirefu Tanzania hatujafanikiwa
kucheza fainali kubwa za mpira Barani Afrika. Mara ya mwisho kupata mafanikio
makubwa kwa Timu ya Taifa (Taifa Stars) ilikuwa ni mwaka 1980 Tanzania
ilipofuzu kucheza fainali za Afrika (AFCON) nchini Nigeria,” amesema Rais
Malinzi na kuongeza:
“Ila kuhakikisha Tanzania inang’ara
tena Kimataifa katika mpira wa miguu Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linania thabiti ya kuhakikisha Tanzania inafuzu kucheza fainali za kombe
la Dunia mwaka 2026 kwa upande wa wanaume (Taifa Stars) na kufuzu kucheza
fainali za Dunia kwa mpira wanawake (Twiga Stars) nchini Ufaransa mwaka 2019.
“Msingi mkubwa wa mafanikio ya Timu za
Taifa duniani kote ni kuwekeza katika mpira wa vijana ili kuhakikisha vijana
wanafundishwa mpira kwa kiwango cha Kimataifa kuanzia wakiwa wadogo. Wakilelewa
pamoja na kufundishwa mpira pamoja ukubwani wanaunda Timu ya Taifa imara yenye
uwezo wa kushindana na timu yoyote duniani. Hakuna njia ya mkato,” alisisitiza
Rais Malinzi ambaye mbali ya Risala hii kupatikana kwenye Mtandao wa TFF wa www.tff.or.tz pia inasomeka
hapa chini neno kwa neno.
Kabla ya kuzindua mfuko huo, Waziri
Nape alisema:
“Kwanza, napenda kuwashukuru wale wote
walioshiriki kuandaa hafla hii na kunialika mimi kuja kuzindua mfuko huu.
“Pili, niwapongeze TFF kwa kubuni
Mfuko huu. Wakati sisi Serikali tunahangaika kuona namna gani tutasaidia,
tayari wenzetu wa TFF umekuja na ubunifu na leo nawazindulia mfuko wenu.
Hongereni sana. Tunawapongeza.
“Kinachohitajika kwa sasa ni kuunga
mkono jitihada hizi za TFF. Ni matumaini yangu kwamba mfuko huu utatimiza
wajibu wenu kwa uaminifu na uadilifu.
“Watu wanaweza kusita kama mtapata
fedha na mkazitumia visivyo. Kama mtapata fedha mkazitumia inavyokusudiwa basi
naamini tutafanikiwa. Na wito wangu kwa viongozi wa mfuko na TFF kuwa wawazi
mna kutoa taarifa kila inapobidi.
“Sisi Serikali, kama wadau wakubwa wa
mpira wa miguu hatutasita kuonyoosha mkono kama mambo yatakuwa hayaendi sawa,
lakini kwa watu walioko kwenye mfuko huu sitatajii kama kunaweza kuibuka
malalamiko yoyote.”
Pamoja na hayo, Waziri Nape alitumia
fursa hiyo kutoa onyo kwa mashabiki wa mpira wa miguu ambao wana lengo la
kufanya fujo kwenye mchezo wa Jumamosi wa Ligi Kuu ya Vodacom utakaozikutanisha
timu za Simba na Yanga kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment