Friday, March 31, 2017

HIVI UNAJUA KWAMBA SIMU YAKO INAWEZA KUKUPUNGUZIA UFANISI KAZINI?




Na Jumia Travel Tanzania



Inawezekana wewe ni miongoni wa watu wasioweza kustahimili kukaa mbali na simu hata kwa dakika moja. Ni suala gumu sana kwa wengi wetu kuweza kuitelekeza simu na kufanya shughuli nyingine kama vile tukiwa ofisini. Lakini je ushawahi kujiuliza kuna madhara gani kwa kuiendekeza tabia hiyo?  
Kutokana na kukua kwa teknolojia simu imekuwa ni kifaa muhimu sana kwa maisha ya kila siku ya binadamu kwani kinamfanya kuwa anapatikana kwa urahisi muda wowote. Jumia Travel imeelezea kwa kifupi katika makala haya athari na namna ya kudhbiti matumizi ya simu ukiwa mahala pako pa kazi.

Kwanza kabisa simu hupoteza muda mwingi kama usipopangilia ni wakati gani wa kuwa nayo na wakati gani sio. Suala hili liko wazi kwa sasa hususani uwepo wa programu nyingi zinazozidi kuvumbuliwa kila kukicha kama vile facebook, twitter, whatsapp, linkedin, pinterest, snapchat, nakadhalika. Programu hizi humhitaji mtu kuzitumia muda wote kutokana na ushirikishwaji wa taarifa kutoka marafiki na vyanzo mbalimbali vya habari. Kupotea kwa muda kutakuja kama na wewe utataka kufuatilia kila jambo linaloendelea kwenye mitandao hii.

Usipokuwa muangalifu pia utapoteza umakini kwenye shughuli zako unazozifanya. Hii inaweza kutokea wakati upo katikati ya kazi fulani na ghafla ukapigiwa simu au ukapokea ujumbe au ishara fulani kutoka kwenye programu zilizopo kwenye simu yako. Sio watu wote wanaoweza kujizuia kutojibu simu au jumbe au pengine kupitisha macho kwenye aidha ya programu hizo. Zipo tafiti nyingi tu zinazoelezea ni namna gani umakini hupotea kutokana na ishara zinazotokana na simu.  

Kutomaliza kazi kwa wakati. Hii inaweza kusababishwa na kila mara kutumia muda kutaka kujibu au kujua kila kitu kinachoendelea kwenye simu yako. Kwa mfano, kama umejiunga kwenye makundi kadhaa ya mtandao wa Whatsapp na mlikuwa mnajadili kuhusu tukio la kusisimua linaloendelea kwa wakati huo; sidhani kama utaweza kutotazama simu yako pindi ujumbe ukiingia huku ukiwa katikati ya kazi fulani.  

Sidhani kama watu wengi wameshagundua kwamba hili ni tatizo. Wafanyakazi wengi wanachokifanya ni kujificha tu ili wasionekane na mabosi wao lakini si kujizuia wasitumie kabisa simu zao.
Unawezaje basi kuiepuka hali hii ambayo inawatesa watu wengi? Zifuatazo ni mbinu chache endapo ukizizingatia unaweza kufanikiwa kuwa na udhibiti juu ya simu yako.

Zima sauti ya simu yako. Ni vema ukazima sauti ya simu yako (mute) kama una kazi nyingi na tena zinazohitaji umakini wako wa hali juu. Hii itakusaidia kuwa na utulivu bila ya muingiliano wa
simu, ujumbe mfupi au milio ya sauti za programu zilizomo kwenye simu. Unaweza kufanya kwenye kipindi maalumu ili pia uwe na fursa ya kufanya mawasiliano mengine muhimu na watu wanaokuzunguka.

Weka mbali simu yako. Kama unaona hauwezi kupitisha hata dakika 10 bila ya kuigusa simu yako, inashauriwa pia ukaiweka mbali. Kwa mfano unaweza kuiweka kwenye droo mahali unapokaa au ukampatia mfanyakazi wako akakuhifadhia na kisha kukurudishia pindi utakapomaliza kazi zako. Hii itakufanikishia kumaliza kazi ulizonazo kwa umakini, ufanisi na wakati bila ya bugudha yoyote ile.

Pangilia muda wa kuwa na simu yako. Pia inashauriwa kupangilia muda maalumu wa kuwa na simu yako ili kujua masuala mbalimbali yaliyotokea wakati uko mbali nayo. Kwa mfano, unaweza pengine ukatenga kila baada ya saa moja au mawili ndiyo unashika simu yako au hata wakati wa kupata chakula cha mchana. Kama hauna shughuli yoyote ambayo itahitaji simu yako kuwa mkononi muda wote basi mbinu hii ni bora zaidi. Kwanza itakupatia muda wa kutosha kuweza kuperuzi na kujibu jumbe na taarifa mbalimbali kwa pamoja huku ukiwa huna wasiwasi wa kushikwa na bosi wako.  

Wafahamishe watu unaowasiliana nao mara kwa mara kwamba utakuwa mbali na simu yako. Endapo utakuwa mbali na simu yako au itakuwa katika hali ya kutotoa sauti au ishara yoyote ile basi ni vizuri ukawafahamisha watu unaowasiliana nao mara kwa mara ili wasikutafute. Hii pia inaweza kusaidia hata kupungua kwa kupokea simu na jumbe nyingi wakati wa kazi.

Kila mabadiliko huja na faida na hasara zake hivyo hatuna budi kujifunza kuendana nayo. Mabosi wengi kwa sasa wanawalalamikia wafanyakazi wao kutumia muda mwingi kwenye simu zao, hasa mitandao ya kijamii badala ya kufanya kazi. Kupitia mbinu hizi kadhaa zilizotolewa na Jumia Travel, tunaamini kwamba kuanzia sasa utaanza kudhibiti matumizi ya simu yako ili kulinda kibarua chako kisiote nyasi. 

No comments: