Wednesday, March 29, 2017

Julius Mtatiro: Sophia Simba Anaweza Kumfukuza Kinana?


Na. Mtatiro J

Sofia Simba na wale wenyeviti wa CCM waliofukuzwa na Halmashauri Kuu ya CCM hawawezi kuitisha kikao chochote ndani ya CCM ila wanaweza kuitisha Vyombo vya Habari na kuvieleza kuwa kikao chao kimemfukuza Kinana. Kama ingehusu CCM, tamko hilo moja feki la Sofia Simba na wenzake lingelitosha kuwapa kesi ya jinai hata isiyo na dhamana. 

Lakini kwa CUF jambo hilo hilo linaleta maswali na hofu. Kwa ufupi, Baraza Kuu rasmi la CUF lilichaguliwa na Mkutano Mkuu mwaka 2014 na litakuwa madarakani hadi mwaka 2019 na ndilo lilimfukuza Lipumba uanachama mwezi Septemba mwaka 2016, na Baraza Kuu hilo hilo ndilo limekutana Zanzibar wiki moja iliyopita kwa mahudhurio ya asilimia 81 ya wajumbe wote na likafanya maamuzi mbalimbali ya chama. 

Baadaye Lipumba (aliyekwishafukuzwa uanachama) naye akaita kundi la watu wanaomuunga mkono (wanachama wa kawaida) pamoja na Wajumbe wa Baraza halali wasiozidi watano eti akadai hicho ni kikao cha Baraza Kuu la CUF. Akaenda mbele zaidi akaita vyombo vya habari na kuvisomea taarifa anayoiita ya Baraza Kuu la CUF, na vyombo haraka vikapata habari ya kuandika "SOFIA SIMBA AMFUKUZA KINANA....SOFIA SIMBA AMKALIA KOONI KINANA."

Maajabu ya namna hiyo yanawezekana kwenye vyombo vya habari na kwenye matamanio ya kifikra, katika uhalisia wa ndani ya Uendeshaji wa vyama hilo halipo. Vyama vya siasa vina mamlaka ya ndani ya vyama hivyo. Vikao vyote vya kitaifa vya CUF na mamlaka zake; Kamati ya Utendaji ya Taifa, Bodi ya Wadhamini, Baraza Kuu la Uongozi la Taifa na Mkutano Mkuu wa Taifa - vilishamalizana na Lipumba tangu mwaka jana.

Vituko na matamko ya Lipumba ya sasa yataendelea kwelikweli, lakini hayawezi kubadilisha maamuzi ya vikao vya chama nilivyovitaja hapo juu. CUF imeingizwa kwenye mgogoro mkubwa wa makusudi lakini mifumo yake ya ndani haitatikiswa na Lipumba. Matamko yake hayawezi kubadilisha maamuzi halali ya vikao halali vya chama.

Tofauti ya CUF na CCM ni kuwa, Ofisi ya CCM ingelivamiwa na Sofia Simba na wenzake, Serikali ingelituma askari na silaha za kutosha wakawafurumushe kina Sofia Simba. Ila kwa CUF, serikali kwa saa 24 imempa Lipumba askari wa kutosha wamlinde ili aendelee kutoa matamko ya KIPUUZI kama hili la sasa.

CUF ina Baraza Kuu moja tu na lilipomsimamisha Lipumba na wenzake walikata RUFAA kwenda mkutano mkuu. Kwa hiyo Lipumba hawezi kuanzisha Baraza Kuu lake leo hii na likafanya maamuzi yoyote kuhusu CUF. 

Julius Mtatiro,
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi,
Safarini.
29 Machi 2017.

No comments: