Thursday, March 2, 2017

MALAWI YAISHAURI GIHON TANZANIA KUFUATA SHERIA

 Mkurugenzi Mtendaji wa Gihon Ministry,  Rebecca Stanford (kushoto), akiwa na  Mwanasheria wa Gihon, Monica Mhoja wakati walipokwenda ofisi ya Balozi wa Malawi nchini.
 Mwakilishi wa Balozi wa Malawi nchini, Micharl Gama (kulia), akiwa na viongozi wa Huduma ya Kiroho ya Gihon ofisi ya ubalozi huo hapa nchini. Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Gihon Ministry,  Rebecca Stanford, Mwanasheria wa Gihon, Monica Mhoja, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano  Gihon, Leonce Zimbandu na Ofisa Habari, Michael Malanyingi.
 Mwakilishi wa Balozi wa Malawi nchini, Micharl Gama (kulia), akiwa na viongozi wa Huduma ya Kiroho ya Gihon ofisi ya ubalozi huo hapa nchini. Kutoka kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Gihon Ministry,  Rebecca Stanford, Mwanasheria wa Gihon, Monica Mhoja, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano  Gihon, Leonce Zimbandu


Na Mwandishi,  Wetu

OFISI ya Ubalozi wa Malawi nchini imeushauri Uongozi wa huduma ya Gihon kuwasiliana na Bodi ya usajili ya Malawi kabla ya kujaza fomu ya maombi ya usajili wa huduma hiyo.

Lengo ni kuutaka uongozi huo kufahamu sheria za usajili za nchini Malawi ili kuepuka usumbufu ambao unaweza kujitokeza iwapo fomu zitajazwa bila kuzingatia sheria na taratibu za nchi husika.

Katibu wa Balozi  wa Malawi nchini, Micharl Gama aliyasema hayo alipokuwa akizungumza na Uongozi wa Gihon jana  katika ofisi ya ubalozi huo ili kupata ufafanuzi wa namna ya kufungua huduma hiyo nchini Malawi.

Alisema ubalozi utahakikisha mawasiliano yanapatikana ili mwanasheria kutoka bodi ya usajili ya Malawi kutoa maelekezo yanayotakiwa kufuatwa kabla ya kufanya usajili wa taasisi (NGO).

“Unajua  mimi siyo mtaalamu wa masuala ya sheria, hivyo mawasiliano nitakayowapatia yatafafanua vizuri kifungu cha sheria  namba 5.05 cha Malawi,” alisema.

Alisema wajibu wa ofisi hiyo ya ubalozi ni kuwaunganisha na wenye mamlaka ili waweze kutekeleza wajibu wao wa kisheria, hivyo  hana uwezo wa tafsiri sharia ya usajili wa NGO.

Mwanasheria wa  Huduma ya Gihon, Monica Mhoja alisema kuwa huduma hiyo imeona kabla ya kujaza fomu za usajili wa huduma  hiyo ya kiroho nchini Malawi, waliamua  kuomba ushauri kutoka katika ofisi za ubalozi huo.

Alisema taratibu zipo tofauti kati ya nchi moja na nyingine, hivyo itakuwa busara kufahamu sheria za usajili kutoka nchini Malawi ili kuepuka uvunjaji wa taratibu za kisheria.

“Tunaomba kufahamu taratibu za usajili wa NGO zilizopo nchini Malawi, kwani tunahitaji kufungua huduma ili kufahamu mgawanyo wa madaraka ulivyo kabla ya huduma kuanza kisheria,” alisema.

Mkurugenzi Mtendaji wa huduma ya Gihon nchini, Rebecca Stanford alisema wamefikia uamuzi wa kushughulikia usajili nchini Malawi baada  ya watu hao kubarikiwa  huduma hiyo kiroho na kimwili.

“Tayari tumefungua tawi la huduma ya Gihon nchini  Malawi  kwa muda wa miaka miwili, hivyo kutokana na uhitaji uliopo tumeona tuisajili huduma hiyo ili itambulike rasmi,” alisema.


No comments: