Tuesday, March 21, 2017

NYUKI WAUA MPISHI WA MAKAMU WA RAIS DODOMA

MPISHI wa Makamu wa Rais, Frank Limo, amefariki dunia baada ya kung’atwa na nyuki.

Limo aling’atwa na nyuki juzi akiwa Mtaa wa Makole, mkoani Dodoma.

Akithibitisha kutokea kwa kifo hicho, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk. Caroline Damian, alisema Limo alifikishwa hospitalini hapo juzi saa 9.15 mchana akiwa ameshafariki.

“Tulimpokea lakini tayari alikuwa ameshafariki kutokana na sumu ya nyuki kuingia kwa wingi katika mwili wake,” alisema Dk. Damian.

Akilizungumzia tukio hilo, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Dodoma, Emmanuel Ochieng, alisema walipigiwa simu na wasamaria wema kuwa katika eneo la Makole, kuna mtu ameng’atwa na nyuki na hajitambui.

“Tulifika eneo la tukio tukiwa na gari pamoja na dawa kwa ajili ya kumwokoa Limo, lakini ilishindikana kwa sababu inaonekana alikuwa na sumu nyingi mwilini.

“Marehemu ni mpishi wa Makamu wa Rais, kwa hiyo baada ya kumwona tulimchukua na kumpakiza katika gari letu na kumpeleka katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma akiwa tayari ameshafariki,” alisema.

Kwa upande wa majirani wa eneo hilo, walisema nyuki hao walimng’ata Limo baada ya kupita eneo hilo kwa miguu.

Akizungumzia tukio hilo, Gloria Kambwembwe, alisema nyuki hao wamekuwa katika mti ulio katika mtaa huo kwa zaidi ya miaka 10 na kwamba wameshapeleka taarifa katika vyombo vinavyohusika, lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa.

“Katika huu mti, hawa nyuki wapo zaidi ya miaka 10, lakini hakuna hatua zilizochukuliwa licha ya kupeleka taarifa katika mamlaka zinazohusika.

Naye Judith Herman, alikilalamikia Kikosi cha Zimamoto kwa kuchelewa eneo la tukio kwa kuwa walipigiwa simu tangu saa nne asubuhi na wao wakafika saa nane mchana. Kibaya zaidi, walipofika walikuwa hawana hata dawa ya kuulia hao wadudu, sasa tunajiuliza hivi kweli wako ‘serious’?


Chanzo-Mtanzania

No comments: