Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Harrison Mwakyembe, ameliagiza Jeshi la Polisi kumuachia huru Msanii Ney wa Mitego aliyekuwa akishikiliwa na Jeshi hilo.
Waziri Mwakyembe ameishauri pia BASATA kuondoa zuio lake dhidi ya wimbo huo, na badala yake uendelee kupigwa tu kama nyimbo nyingine.
Akiongea na wandishi wa Habari leo mjini Dodoma, Dk. Mwakyembe amesema hata Rais Magufuli amefurahishwa na wimbo huo wa WAPO, na kumshauri Msanii huyo kama inawezekana aendelee kutaja watu wengine kama vile wakwepa kodi, wauza unga, wabwia unga, wezi pamoja na watu wengine wasio na maadili mema katika jamii.
Katibu Mkuu wa Basata, Godfrey Mngereza alieleza kuwa Baraza liliusikiliza wimbo huo na kubaini kuwa ni wimbo usiofaa kwa jamii na zaidi unachochea vurugu.
“Ule wimbo tumeusikiliza, kama Baraza tunasema ule wimbo hauna maadili, ni wimbo ambao una matusi, ni wimbo ambao unachochea vurugu, ni wimbo ambao haufai kwa jamii,” alisema.
Aliongeza kuwa vyombo vyote vya habari ambavyo vitaucheza wimbo huo vitakumbwa na mkono wa sheria kutoka kwa vyombo husika.
Nay wa Mitego alikamatwa na Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro majira ya saa nane usiku, na alifikishwa Dar es Salaam kwa mahojiano na Jeshi la Polisi.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro, Kamanda Ulrich Matei alithibitisha kukamatwa kwa msanii huyo usiku wa kuamkia jana.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, wakili Peter Kibatala alisema kuwa atasimamia kesi dhidi ya msanii huyo na kwamba tayari ameshamjulia hali katika kituo cha kati jijini Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment