TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI KUHUSU UFAFANUZI WA AJALI ALIYOPATA JANA MSTAHIKI MEYA WA JIJI LA DAR ES SALAAM ISAYA MWITA.
Ndugu wanahabari na wananchi wote wa jiji la Dar es Salaam, jana Mstahiki Meya wa Jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita alipata ajali ya gari maeneo ya manzese Tiptop walipokuwa wakitoka Dodoma kwenye kikao. Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 11:30 jioni.
Katika msafara huo, kabla ya kufika jijini Dar es Salaam, wakitokea Dodoma, walipofika Dumila Mkoani Morogoro walikuta ajali mbaya ya gari ambapo ndani ya gari hiyo iliyopata ajali alikuwepo mchezaji wa simba Jonas Mkude ambaye alikuwa ameumia.
Kutokana na uzito wa jambo hilo, Mstahiki Meya Mwita aliamua kumchukua mchezaji huyo kwa ajili ya kumpeleka Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu. Baada ya kufika eneo la Ubungo Kibo, walikutana na foleni na hivyo kuamua kupita barabara ya mwendokasi ili kumuwahisha majeruhi huyo ambaye alikuwa akilalamika kuwa anamaumivu makali.
Hata hivyo gari ilipofika eneo la Manzese Tiptop alitokea Dereva wa bodaboda ambaye alikuwa akikatiza kwenye barabara , Dereva aliyekuwa akimuendesha Mstahiki Meya Mwita akiwa anaendesha gari alimgonga mwendesha bodaboda huyo na kusababisha gari kuyumba na baada ya mwendo wa hatua chache ilisimama. Katika ajali hiyo hakuna mtu aliyeumia. Wote waliokuwa kwenye gari hiyo akiwepo Mstahiki Meya wa jiji Mwita hawakupata majeraha yoyote.
Imetolewa leo Mei 29 na
Christina Mwagala, Ofisa habari Ofisi ya Meya wa Jiji.
No comments:
Post a Comment