Saturday, May 20, 2017

NI KARATA MUHIMU KWA SERENGETI BOYS

Serengeti Boys - Timu ya Taifa ya vijana wa Tanzania wenye umri wa chini ya miaka 17, kesho Jumapili Mei 21, mwaka 2017 inarusha karata muhimu katika mchezo hitajika dhidi ya Niger kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika - AFCON u-17.
Serengeti Boys itaingia Uwanja wa Port Gentil hapa mjini Port Gentil huku mkononi ikiwa na pointi 4 ilizovuna katika michezo yake miwili ya awali kwani ilianza kupata sare tasa dhidi ya Mali Mei 15, mwaka huu kabla ya kuifunga Angola Mabao 2-1 katika mechi zilizofanyika Uwanja wa l’Amitee jijini Libreville.
Vijana wa Serengeti Boys ambao wamefikia Hoteli ya Strange Complex, wana ari ya ushindi dhidi ya vijana wenzao wa Niger ambao wana alama moja waliyoipata kwenye sare ya mabao 2-2 dhidi ya Angola walipocheza mwanzoni mwa wiki hii. Niger walipoteza mchezo wa pili dhidi ya Mali. Walifungwa mabao 2-1.
Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Nyundo Shime amesema: “Huu ni mchezo muhimu wa kupata matokeo muhimu kwa vijana wetu. Tumejiandaa vema kuwania nafasi ya angalau kuingia nusu fainali.”
Shime ambaye wakati wote amekuwa akishukuru uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), kwa namna unavyojitoa kuiandaa timu hiyo kwa kuipa kambi tulivu nchi mbalimbali, amesema: “Hili ni deni.”
Akifafanua zaidi, Shime ambaye anafahamika zaidi kwa jina la Mchawi Mweusi, anasema: “…Nina deni. Nadaiwa na uongozi wa TFF chini ya Jemedari Jamal Malinzi, pia nina deni kwa Watanzania ambao wamekuwa wakihaha kutuombea dua na kuichangia timu hii. 
“Nawashukuru sana kwa namna wanavyojitolea kwetu, na ndio maana nasema hili ni deni na niwaahidi tu kwamba nitaendelea kulilipa kesho kwa matokeo mzuri. Katika kila mchezo huwa na mipango yangu na mpango wa kesho ni ushindi tu. Tutacheza soka la kushambulia.”
Shime ambaye alisema kwamba ataingia kwa mfumo mwingine kesho, hatarajii kikosi chake kikawa na mabadiliko makubwa labda mpaka atakapoangalia mazoezi yatakayofanyika jioni ya leo kwenye Uwanja Sogara.
Nahodha wa timu hiyo, Dickson Job aliwatoa shaka Watanzania akisema vijana wote wako vema kwa ajili ya mchezo huo kwani mpira wa miguu kwao ni ajira kwa manufaa ya yao binafsi, familia kadhalika taifa ambalo limewatua Gabon kutafuta Kombe la Mataifa ya Afrika.

“Kuna watu wanadhani tunapochukuliwa na watu wa doping ni kama tunatumia dawa, hapana. ni utaratibu wa mechi za kimataifa kwamba mara baada ya mchezo wowote wa kimataifa, kanuni zinaruhusu madaktari kuchukua wachezaji kadhaa na kuwapima ili kuandika ripoti ya kila mchezo.

“Mchezo wa kwanza dhidi ya Mali nilichukuliwa mimi na Israel Patrick Mwenda na wachezaji wa Mali wawili. Mchezo wa pili alichukuliwa Abdul Suleiman na Kelvin Naftal na wenzetu wa Angola wawili. Ni jambo la kawaida ni ni utaratibu kwa kitengo cha Doping,” alifafanua Job.

Serengeti Boys inahitaji sare ya aina yoyote ili iwezi kuvuka ilihali Niger ambayo ina alama moja na ikishika mkini, imejiwekea matumaini ya kusonga mbele ikitamba kwmaba itafunga Tanzania.

Hakuna shaka kuwa dua za Watanzania zitakuwa pamoja na timu nzima ya Serengeti Boys ambayo kwa sasa imekuwa ikichungwa na timu pinzani katika kuwania nafasi hii muhimu ya ujio mpya wa mpira wa miguu wa Tanzania.

Mungu Ibariki Serengeti Boys.
Mungu Ibariki Tanzania.
Mungu Barki viongozi wote wa Tanzania.
Mungu Bariki michuano ya CAF.

…………………………………..………………………………………………………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA

No comments: