Katibu wa itikadi, mawasiliano na uenezi bw. Ado Shaibu akiongea na waandishi wa habari mapema leo jijini Dar es salaam na kushoto ni Seif Hamad msaidizi katibu na uenezi zanzibar. |
Kuzaliwa Upya kwa Uzalendo wa Rasilimali: Kuiweka Ripoti ya Mruma Kwenye Muktadha
Ndugu Watanzania
Tarehe 24 Mei 2017, kamati iliyoundwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuchunguza suala la usafirishaji wa mchanga wa dhahabu (Makinikia) nje ya nchi iliwasilisha ripoti yake kwa Rais.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Kamati hiyo iliyoongozwa na Profesa Mruma, masuala makubwa matatu yaligunduliwa:
- Kwamba kiwango cha dhahabu kilichoripotiwa kuwemo kwenye kila kontena ni tofauti na kiwango halisi cha dhahabu kilichomo.
- Kwamba mbali na dhahabu, kwenye makenikia kuna aina nyingine ya madini kama vile Chuma, Rhodium, Sulphur n.k ambayo hayaripotiwi na Wakala wa Ukaguzi wa Madini TMAA.
- Kwamba kutokana na sababu ya kwanza na ya pili, Tanzania imekuwa ikipoteza matrilioni ya shilingi katika mapato yake tangu utaratibu wa kusafirisha nje makenikia uanze miaka 17 iliyopita.
Kutokana na unyeti wa suala la upotevu wa mapato kwenye sekta ya madini na maliasili nyinginezo, Chama chetu cha ACT Wazalendo kimeandaa mjadala wa kitaifa kujadili juu ya 'Kuzaliwa Upya kwa Uzalendo wa Rasilimali', kwa kuchambua Ripoti ya Tume ya Prof. Mruma na kutoa mwongozo wa Kisera juu ya usimamizi wa rasilimali madini kwa ujumla wake nchini.
Kwa vile hili ni jukwaa la kitaifa, wataalamu na wanaharakati mbalimbali wamealikwa kutoa mada. Miongoni mwao ni wafuatao:
- Dr. Rugemeleza Nshala - Mkurugenzi Mtendani, Timu ya Wanasheria Watetezi wa Mazingira kwa Vitendo (LEAT).
- Ndugu Nicodemus Kajungu - Katibu Mkuu, Chama cha Wafanyakazi Migodini (NUMET).
- Ndugu Amani Mhinda - Mtendaji Mkuu kutoka Asasi inayosimamia haki za Wachimbaji wadogo pamoja na jamii zinazoishi katika maeneo yenye rasilimali madini ya HAKIMADINI.
- Ndugu Kabwe Z. Ruyagwa Zitto ambaye ni Kiongozi wa Chama chetu cha ACT Wazalendo.
ACT Wazalendo tunaamini kwa dhati kuwa suala la usimamizi wa rasilimali madini, ili liwe na tija, linahitaji mjadala huru na mpana wa kitaifa ili kuliweka suala zima katika uhalisia wake kwa maslahi ya nchi.
Tunachukua fursa hii kuwakaribisha wananchi kushiriki kwenye kongamano letu litalofanyika jumamosi ijayo, tarehe 3 Juni 2017. Taarifa zaidi itatolewa baadae kuhusu Ukumbi wa mada za mjadala.
Ado Shaibu,
Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi,
ACT Wazalendo
Mei 28, 2017
Dar es salaam
No comments:
Post a Comment