Na Zitto Zubeir Kabwe.
Naipongeza Serikali kwa Kuchukua Hatua Juu ya Sakata la Escrow
Kwa dhati kabisa naomba nichukue nafasi hii kwa niaba ya Chama changu kuipongeza Serikali kwa hatua hii ya kuwafikisha Mahakamani Watuhumiwa wa Sakata la Escrow kama ilivyoazimiwa na Bunge Septemba, 2014. Hii ni hatua muhimu sana katika mapambano dhidi ya Ufisadi nchini.
Nasikitika ndugu yangu Deo Fulikunjombe hayuko hapa kushughudia matokeo haya ya kazi kubwa aliyoifanya kwaajili ya Taifa.
Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama - ACT Wazalendo
Mikumi- Morogoro
Juni 19, 2017
TUJIKUMBUSHE
Uamuzi wa ICSID kuhusu IPTL mshindi Ni Tanzania
Septemba 12, 2016 Mahakama ya Usuluhishi wa migogoro ya uwekezaji iliwasilisha rasmi maamuzi yake Kwa pande zilizokuwa kwenye mgogoro kuhusu mradi wa kufua umeme Nchini, IPTL. Mahakama hiyo iliamuru kwamba Benki ya Standard Chartered ya Hongo Kong ( SCB-HK ) ilipwe dola za Kimarekani 148 milioni sawa na Fedha za Kitanzania shilingi 320 bilioni. Mahakama hiyo Pia imeamuru kuwa kuchotwa Kwa Fedha kutoka akaunti maalumu ya TEGETA Escrow hakukuondoa Haki ya ya Benki ya SCB-HK kwenye kampuni ya IPTL na hivyo kisheria kwamba Benki hiyo Kwa sasa ndio mwenye uhalali wa shughuli zote za IPTL.
Ilinichukua Siku takribani 2 kusoma na kusoma tena tuzo hii (Award ) ili kuweza kuielewa haswa maana yake Kwa Nchi yetu. Ikumbukwe kwamba niliongoza Kamati ya Bunge iliyoagiza uchunguzi wa sakata la TEGETA Escrow Account na kuandaa Taarifa Maalumu ya Kamati ya PAC iliyosomwa na kukubaliwa rasmi na Bunge na kupitisha maazimio 8 yaliyopaswa kutekelezwa na Serikali. Baada ya kuisoma Kwa kina Tuzo hiyo ya ICSID nilichoona Ni kwamba masuala Yale Yale ambayo PAC iliyafafanua Bungeni Mwezi Novemba mwaka 2014 ndio hayo hayo yaliyopelekea tuzo hiyo. Kwa maana hiyo Ni kwamba iwapo Serikali ingetekeleza Maazimio ya Bunge yote Leo hii tungekuwa kwenye nafasi nzuri sana ya kulimaliza suala Hilo kabisa na kuachana kabisa na mgogoro huu ambao unanyonya Fedha za Watanzania.
Kuna masuala makuu 2 ambayo yakieleweka suala la kashfa ya IPTL litakuwa limeeleweka na maamuzi yanaweza kufanyika kumalizana nalo.
1. baada ya mbia ya kampuni ya Mechmar kufilisika nchini Malaysia, Ni Nani mwenye Haki na Mali za IPTL?
2. Tozo ya malipo ya umeme uliozalishwa na IPTL ilizidishwa?
Kwenye Taarifa ya Kamati ya PAC tulionyesha Kwa vielelezo na ushahidi kwamba kampuni ya PAP haikuwa ina umiliki wa kihalali wa asilimia 70 ya Hisa za IPTL. Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali alionyesha dhahiri kuwa vyeti vya Hisa ( shares certificates ) za kampuni ya Mechmar kwenye IPTL walikuwa nazo Benki ya SCB-HK Kama dhamana ya mkopo waliowapa IPTL. CAG aliziona hati hizo Kwa macho yake kwenye uchunguzi wake ambao ndio uliotumika na PAC kufikia maazimio 8 ya Bunge.
Vile vile Kamati ya PAC ilionyesha Kwa ushahidi kuwa PAP hawakufuata sheria za Tanzania katika kumiliki IPTL ikiwemo kwamba walikwepa kodi kupitia kampuni iliyoitwa PiperLink ya British Virgin Island. TRA walikiri mbele ya Kamati kuwa wakati Mahakama Kuu inatamka kuwa PAP wapewe ' masuala ( affairs ) ya IPTL ) hawakuwa na uhalali wa kufanya Biashara Tanzania kwani hawakuwa wamepewa kibali na Kamishna Mkuu wa Kodi cha kuthibitisha utwaaji wao wa kampuni ya IPTL. Hivyo Kamati ililiambia Bunge kuwa PAP ni matapeli wa Kimataifa waliopiga ganzi Mfumo wa Serikali ya Tanzania Kwa kutumia rushwa na hivyo kuhalalishiwa umiliki wa IPTL ili kuchota Fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya TEGETA Escrow Benki Kuu ya Tanzania.
Hata Gavana wa Benki Kuu alipowaomba PAP uhalali wa wao kumiliki IPTL walichotoa ni kitu kinachoitwa Deed of Assignment badala ya shares certificates. Watanzania watakumbuka kuwa Deed of Assignments ndizo zilizotumika kuiba Benki Kuu kwenye wizi wa EPA mwaka 2004-2005. Jambo la kushangaza Ni kwamba karatasi hiyo ya kugushi ilikubaliwa na hivyo Bwana Harbinder Singh Seth wa PAP akaruhusiwa kuchota mabilioni ya Fedha kutoka Benki Kuu ya Tanzania. Kwa mujibu wa Mwanasheria wa TANESCO Bwana Richard Rweyongeza TANESCO waliilipa PAP $245m Sawa na shilingi 530 bilioni. Itakumbukwa kuwa wakati PAC inasoma Taarifa yake Fedha hizo zilikuwa tshs 306 bilioni tu.
Katika tuzo yake ICSID imethibitisha kuwa PAP hakuwa mmiliki wa IPTL na hivyo alilipwa Fedha za TEGETA Escrow kimakosa. Hoja hii imethibitisha Hoja ya PAC na Bunge la Tanzania ambayo ilipingwa vikali na Serikali ya wakati huo ambayo iligeuka mtetezi wa PAP. Uamuzi wa ICSID kwamba TANESCO wailipe SCB-HK unathibitisha kuwa PAP alipewa Fedha za TEGETA escrow kitapeli.
Baada ya kumaliza hoja hiyo twende Hoja ya pili; je Hata Kama PAP wangekuwa Ni Wamiliki halali wa IPTL walilipwa ziada?
Itakumbukwa kwamba PAC ililiambia Bunge kuwa mgawo wa Fedha ulipaswa kusubiri kukokotoa kanuni za mgawo ambazo ziliamriwa na Mahakama hiyo ya ICSID. Hoja kubwa ya PAC ilikuwa ' Ni Kwanini tulifanya haraka kutoa Fedha kabla ya Uamuzi wa kiwango gani kilipwe? '. Hoja hii ndio iliyochagiza kuwa mule ndani ya TEGETA escrow kulikuwa na Fedha za umma. Uamuzi wa kukokotoa ukatolewa Mwezi Februari mwaka 2014 lakini katika mjadala mzima wa sakata la TEGETA escrow Serikali ilikataa kata kata kutekeleza Uamuzi huu. Hata kwenye Hoja za TANESCO mahakamani huko hawakuwa kabisa na Hoja kulinda Uamuzi ule. Hata hivyo ICSID imeamua kuwa tulikuwa tunaliwa Kwa kulipa tozo kubwa zaidi ya kiwango tulichopaswa kulipwa. Hii maana yake Ni kwamba Hata kwenye hizo za wizi tuliilipa PAP zaidi ya tulichopaswa kuwalipa.
Katika magazeti ya Leo wakili aliyeiwakilisha TANESCO anasema " tulibishania Hoja ya kulipa Kwa viwango vya zamani ikaamuriwa hesabu zifanyike upya Mahakama iliamuru hesabu zifanyike upya Kwa kutumia mkopo wa wana Hisa ". Hii ndio Hoja ambayo PAC iliijenga Kwa muda mrefu na kubezwa na Serikali ndani ya Bunge Kwa mbwembwe zote. Wakili wa TANESCO anaendelea " kutokana na hesabu hizo gharama ilikuwa chini. IPTL ililipwa zaidi hivyo inatakiwa kurejesha Dola za Marekani zaidi ya milioni 100 Kwa TANESCO ".
Hii ndio ilikuwa Hoja ya PAC ambayo ilitokana na maagizo ya CAG kwamba TANESCO wakae chini na SCB-HK kupiga hesabu upya. Hoja hii ilikataliwa na Serikali na TANESCO wenyewe ilipotolewa na PAC lakini Leo mwanasheria wa TANESCO aliyeiwakilisha TANESCO katika Mahakama ya Usuluhishi ya ICSID anakiri tuliwalipa zaidi IPTL.
Jambo la kushangaza Ni kwamba, licha ya ushindi huu mkubwa Kwa Tanzania na TANESCO wanasheria wanataka tukate rufaa. Magazeti ya Serikali ya Dailynews na habari leo ndio yameongoza na habari hiyo. Ikumbukwe kuwa magazeti hayo ndio Siku zote yamekuwa yakiitetea pap na Bwana Seth. Ni dhahiri kuwa ama wanasheria wanataka waendelee kulipwa Fedha kwenye kesi au kuna shinikizo kubwa kutoka Kwa wanaofadika na mchezo huu wa kutapeli ili waendelee kufisadi Nchi. Uamuzi huu wa ICSID unatuweka kwenye nafasi nzuri sana ya kulimaliza kabisa suala la IPTL kwani umetuonyesha kuwa;
1)Kwa miaka yote ya uwepo wa IPTL tumekuwa tunapigwa Kwa kulipa capacity charges Mara mbili ya kiwango tulichopaswa kulipa
2)Tulitapeliwa na Bwana Seth kupitia kampuni ya PAP ambayo Wamiliki wake wengine 50% mpaka sasa hawajulikani Ni kina Nani licha ya kuwajua Kwa jina la Simba Trusts ya Australia.
Wakati wanasheria na baadhi ya maofisa wa Serikali waliofadika na mgawo wa TEGETA escrow wanataka kukata rufaa wanajua kuwa maamuzi ya ICSID hayana rufaa Kwa mujibu wa Ibara ya 53 ya mkataba wa ICSID ( no appeal except those provided for in the ICSID Convention ). Hadhi yake Ni Sawa na maamuzi ya Mahakama ya juu kabisa ya Tanzania Kwa mujibu wa Ibara ya 54 ya mkataba wa ICSID ( convention ). Hata hivyo maamuzi hayo yanaweza kuombewa kufutwa Kwa kutumia Ibara ya 52(2) Kwa sababu maalumu ambazo Ni
a). Baraza la Usuluhishi halikuundwa kisheria ( properly constituted ). Ijulikane kuwa Baraza hili huteuliwa na washiriki wa kesi. SCB-HK waliteua msuluhishi wao, TANESCO waliteua wao na Kwa pamoja wakateua Rais wa Baraza. Hivyo TANESCO hawana Hoja maana Hata msuluhishi waliteua wao kakubaliana na maamuzi haya ya tuzo hii.
b). Kwamba Baraza lilienda nje ya mamlaka yake. TANESCO walishiriki mwanzo mwisho na hawakuwa na malalamiko kuhusu Hilo wanawezaje kuwa na malalamiko sasa. Hata msuluhishi wao kakubali maamuzi haya.
c). Kwamba kulikuwa na rushwa kwenye kufikia maamuzi haya. TANESCO wanaweza kutoa ushahidi Kama Hata msuluhishi waliyemteua wao alihongwa!
d) kwamba tuzo haina sababu za kufikia maamuzi haya. Kwa walioisoma tuzo hii wanajua kuwa sababu zipo kinagaubaga kabisa.
Kwa maoni yangu kutaka kesi iendelee Ni kutaka kulinda maslahi ya wanaofadika na suala zima la IPTL. Suala hili sasa liishe. Nchi imeshaliwa sana. Itoshe.
Ushauri wangu Kwa Serikali Ni Kama ifuatavyo
1. Kutekeleza tuzo hii ya ICSID bila kusita
2. Kuiamrisha kampuni ya PAP kurejesha Fedha zote za ziada ilizolipwa kutoka akaunti ya TEGETA escrow. Kwa mujibu wa tuzo hii Ni jumla ya tshs 202 bilioni
3. Kuitaka kampuni ya PAP kuilipa Benki ya SCB-HK kutokana na hati iliyowasilisha Benki Kuu kwamba madai yeyote yakitokea katika IPTL PAP ndio watalipa ( indemnity ).
4. Kuchunguza na kuishtaki PAP na Bwana Harbinder Singh Seth Kwa utapeli na utakatishaji wa Fedha Kwa mujibu wa sheria za Tanzania
5. Kuchunguza na kuwashitaki maofisa wote wa Serikali walioshirikiana na Seth kuchota Fedha Benki Kuu
6. Kuilipisha faini Benki ya StanBic Tanzania Kwa kushiriki kwenye vitendo vya kutakatisha Fedha kufuatia miamala ya TEGETA escrow
7. Kufunga kabisa suala la IPTL Kwa kuvunja mkataba na kuitwaa mitambo Kwa mujibu wa sheria za Tanzania
Natumai kuwa watu wenye nafasi za Uongozi wa umma ambao maamuzi Yao yamefikisha Nchi hapa watachutama na kuondoka katika Uongozi wa umma. Tumefikishwa hapa na wizi na tamaa za watu madalali wa matapeli. Ninaamini kuwa Rais John Pombe Magufuli hatakubali Nchi hii kuendelea kupigwa na matapeli.
Zitto Kabwe, Mb
Kigoma Mjini
23 Septemba 2016
KUTOKA KWA YERIKO NYERERE---
Nipo kitandani siku 5 nauguza maleria ya Sentero shimoni.....
Dakika cheche zilizopita ndio nimeanza kupata ufahamu na kumwambia bibiyenu anisogezee simu niingie dunia,
Laa haulaa nakutana na picha za Singasinga na Lugemalila wakiwa mahakamani...
Pamoja na tofauti zangu zoooooote na serikali hii, katika hili nampongeza rais Magufuli, uthubutu wa kumfikisha Singasinga mbele ya sheria ni hatua kubwa sana dhidi ya mapambano ya rushwa...
Kwa wasiomjua Singasinga ni mtu wa aina gani Muulizeni Kamanda David Kafulila ambaye leo naamini amefurahi sana,
Ukimgusa singasinga umegusa nchi nyingi kama 20 hivi zikiwemo za Yemen, Ufaransa, Pakstan, USA nk...
Yani yeye ndie kiunganishi (super brocker) wa nchi hizo, mfano ukihitaji msaada wa miradi ya maji toka nchi za Arabuni basi utalazimika kupita kwa Singasinga...
Sisi wapinzani tulipaza sauti sana juu ya mgogoro wa IPTL na ule wa ESCROW lakini kinyume chake wapambanaji kama David Kafulila waliishia mahakamani..
Nitakupinga kwa mengine lakini kwa hili nakuunga mkono mh Rais...
KUTOKA KWA MALISA J
Hili la Escrow wanaohitaji credit ni wafuatao (nimepanga kulingana na unuhimu wao ktk vita hii):
3. Marehemu Deo Filikunjombe
4. Tundu Antipas Lissu
5. Wabunge wote wa upinzani
6. Baraza la vijana la Chadema
7. Vyombo vya habari (vya binafsi)
8. Mitandao ya kijamii
9. Asasi za kiraia
10. Rais John Pombe Magufuli
Wanaohitaji kulaaniwa/kulaumiwa vikali kwa kutetea wizi huu na kusema si pesa za umma:
1._______________ (Mtajaza wenyewe maana tumeambiwa tumuache apumzike),
2. Wabunge wa CCM bunge lililopita (but namuondoa Dr.Kigwangala na wengine wachache),
3. Vyombo vyote vya habari vya umma (TBC 1, TBC Radio, Daily News, Habari Leo, etc),
4. Vyombo vyote vya habari vya CCM (Uhuru radio, Uhuru gazeti),
5. Fredrick Werema (aliyekua Mwanasheria mkuu),
6. Waziri Muhongo,
7. Waziri Ngeleja etc,
8. Waliokua viongozi waandamizi serikalini (RCs, DCs, Mawaziri, etc),
9. Umoja wa vijana wa CCM (Hapa namuondoa Magoiga SN, angalau yeye alionesha ujasiri wa kupingana na chama chake hadharani kwa kukataa kutetea wezi),
10. Chama cha Mapinduzi (CCM).!
KUTOKA KWA DAVID KAFULILA
KAFULILA:LEO NI SIKU MUHIMU KWANGU NA VITA DHIDI YA UFISADI!
Hatimaye imekuwa! Vinara katika ufisadi wa IPTL/ESCROW Singasinga Sethi na Rugemalila watiwa nguvuni. Huu ni uamuzi mkubwa uliosubiriwa sana. Na siku zote sikujua kwanini Mhe Rais alikuwa anahofu kuagiza hatua hii.
Sikujua kwanini kwasababu wakati wa mnyukano wa hoja hii, Mhe Rais alikuwa bungeni na alikuwa sehemu ya maazimio ya Bunge kutaka mitambo ya IPTL itaifishwe na wahusika watiwe nguvuni..
Nakumbuka nikiwa kwenye kipindi kigumu hata kutishwa kuondolewa kichwa na kuitwa majina ya wanyama, yeye alikuwa miongoni mwa mawaziri 5, walionidokeza kwamba ESCROW ni dili.nikomae tu mpaka kieleweke!
Nampongeza Mhe Rais kwa uamuzi huu muhimu uliosubiriwa siku nyingi kuamua hatma ya ufisadi huu uliomshinda vibaya mtangulizi wake.
Singasinga huyu alinifungulia kesi kunidai Sh300bn Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka 2014, Agust2015 nikamshinda lakini akamua kunifungulia upya Mahakama ya Kisutu akidai Sh100m, zote akidai nimsafishe kuwa yeye na wenzake hawakuchota zaidi ya 300bn kifisadi.
Kifupi naomba PCCB na DPP wasituangushe watanzania. Nilipata kuwaza kumwomba Mwanasheria Mkuu wa Serikali anipe kibali niendeshe kesi na hawa majabali wa escrow kwani nina ushahidi wakutosha,Sasa nina furaha kwamba PCCB wameamua kuwaburuza.
Nashauri mambo machache;
1.Mall zote za wahusika hawa ziwekwe chini ya ulinzi kabla hawajahamisha umiliki kwani nimuhimu zikakamatwa kusubiri hukumu ya kesi hii ya Tanzania lakini pia kesi iliyopo Mahakama ya kimataifa ya International Centre For Settlement of Investment Disputes (ICSID).Ambako Sept2016, iliamuliwa tulipe Bank ya SCB-HK kiasi zaidi ya 400bn kwakua ndio wamiliki halali wa IPTL na wenye share certificate za IPTL..
Mwaka huu TANESCO imekata rufaa.Najua TANESCO hawajakata rufaa kushinda kesi bali kuomba wapunguziwe hukumu ifanane na uamuzi wa ICSID wa Feb2014.
Lakini kwakuwa Singasinga Sethi alisaini hati na Bank Kuu ya Tanzania, kwamba deni lolote lotakalotokana na migogoro ya IPTL atawajibika yeye na wenzake wanaomiliki kampuni PAP, ndio maana nasisitiza Mali za watu hawa zishikiliwe.
2.Mtambo wa IPTL uwekwe chini ya TANESCO kama ilivoazimiwa na Bunge Nov2014, tuachane kabisa na kulipa matapeli 7bn kila mwezi ambazo ni malipo ya capacity charges walizokuwa wanalipwa na serikali hii bila kujali IPTL imezalisha au haijazalisha umeme.
3.Mwisho watanzania watambue kwamba huyu Singasinga anaetambulishwa kama mmiliki wa PAP iliyopora 300bn za escrow kama mmiliki mpya wa IPTL,mpaka pesa hizo zinaporwa alikuwa anamiliki asilimia50% tu yakampuni.lakini asilimia 50% zilikuwa zikimilikiwa na kampuni ijulikanayo kama SIMBA TRUST, inayomilikiwa na watu wasiojulikana. Hawajawahi kutajwa popote kwenye report zote.
Nilijaribu kutaka majina yao kwenye Kamati ya Viwanda wakati tukiwahoji BRELA na hata baadae bungeni Serikali iliendelea kusisitiza kuwa majina hayo ni SIRI.Hawa ni wahusika muhimu sana wajulikane kwani inawezekana ndio msingi wa serikali ya awamu ya nne kuibeba IPTL kama mtoto!
Naam, Hongera Mhe Rais kwa hatua hii, nazidi kuomba Mungu kesi hizi zifike mwisho kwani kwangu leo ni siku muhimu katika kumbukumbu zangu kuliko Aprili28,2015, siku niliyopewa tuzo kwa mapambano dhidi ya Ufisadi kwa rejea ya sakata la ESCROW. Kwani tuzo haina maana kama vita haifiki mwisho!
Mwisho nishauli asiwepo yeyote wakulindwa kwa Kinga yoyote kwani Katiba na Sheria vipo kwajili ya watanzania na sio watanzania kwajili ya Katiba na Sheria. Tusipofika huko vita ya UFISADI mkubwa itakuwa ngumu sana kufika mwisho!
David KAFULILA
JUNE19,2017
No comments:
Post a Comment