Thursday, July 6, 2017

HAKIMU PATRICIA KISINDA AJITOA KUSIKILIZA KESI YA GODBLESS LEMA

Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Arusha, Patricia Kisinda aliyekuwa anasikiliza kesi ya uchochezi inayomkabili Mbunge wa Jimbo la Arusha mjini, Godbless Lema dhidi ya Rais John Magufuli amejitoa baada ya kuwekewa pingamizi kuwa ana urafiki na mke wa Lema (Neema Lema).

Hakimu huyo ni wa pili kujitoa katika kesi hiyo, kwani Mei 29, Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Arusha, Desderi Kamugisha pia alijitoa kwa maelezo kuwa hawezi kusikiliza kesi zote nne zinazomkabili Lema hivyo kuwaeleza mahakimu wengine watapangiwa kesi hiyo.
Alhamisi hii wakati kesi ikipangwa kusomewa maelezo ya awali, Wakili wa Jamhuri katika kesi namba 441, Sabina Silayo aliwasilisha hoja katika mahakama hiyo kuwa Hakimu Kisinda ana urafiki na Neema.
Sabina alieleza mahakama kuwa ana ushahidi kuwa hakimu Kisinda ana urafiki wa karibu na mke wa Lema.
“Ombi la Jamhuri ni kuwa hatuna imani na wewe kuendelea na shauri hili na tunaomba ujiondoe kwa vile mke wa mshtakiwa ni rafiki wako wa karibu sana na ushahidi huo tunao na haina pingamizi,” amesema Sabina.
Amesema Hakimu huyo kuendelea kusikiliza kesi hiyo kutaondoa imani kwa upande wa Jamhuri kwani huenda haki isitendeke na hivyo aliiomba mahakama ipange kesi hiyo kwa hakimu mwingine.
Baada ya hoja hiyo kuwasilishwa mbele ya wakili wa utetezi wa Lema, Sheck Mfinanga aliomba mahakama kutupa hoja hiyo kwani haina uzito kwa kuwa Watanzania wote ni ndugu na ni marafiki.
Wakili Mfinanga amesema kesi hiyo haina urafiki hivyo kama mahakama iko kwa ajili ya kusimamaia sheria na haki iache hakimu huyo aendelee na kesi hiyo.
Hata hivyo, Wakili wa Serikali Sabina alijibu hoja hiyo kwa kuonyesha mashauri mbalimbali ambayo yalionyesha kuwa kuna kanuni na sheria za mahakama kuwa endapo itabainika kuwa Jaji au Hakimu ana uhusiano wowote na mshtakiwa au mshtaka atatakiwa ajiondoe kusikiliza kesi hiyo.
Hata hivyo, kutokana na hoja hizo za pande mbili, Hakimu Patricia ametumia dakika 20 kufanya uamuzi mdogo juu ya hoja ya upande wa Jamhuri na amekubaliana ana hoja hiyo ya kujiondoa.
Hakimu Patricia amesema ameamua kujitoa ili kupisha haki itendeke lakini yeye si rafiki na mke wa Mbunge bali anamfahamu tu.
Hata hivyo, amesema rufaa juu ya uamuzi huo iko wazi na kwamba Agosti 2 mwaka huu kesi hiyo itafikishwa mahakamani tena kwa ajili ya kupangiwa hakimu mwingine kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali.

No comments: