Sunday, July 30, 2017

TAARIFA JUU YA HALI YA UPATIKANAJI, USAMBAZAJI NA UGAWAJI WA PEMBEJEO KWA WAKULIMA WA KOROSHO NCHINI TAREHE




HALI YA KILIMO NCHINI
Serikali yeyote makini lazima ihangaike na masuala yanayowahusu wananchi wake walio wengi, na hapa Tanzania watu hao (walio wengi) ni Wakulima. Hivyo basi, kipimo kikuu cha kuondoa umasikini wa Watanzania ni kuondoa umasikini wa wakulima.
Tanzania imeendelea kutegemea Sekta ya Kilimo katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wananchi wake kwa kuwa inatoa ajira kwa asilimia 65.5 ya Watanzania na inachangia zaidi ya asilimia 100 ya chakula kinachopatikana nchini kwenye miaka yenye mvua za kutosha. Katika mwaka 2016 Sekta ya Kilimo ilichangia asilimia 29.1 ya Pato la Taifa ikilinganishwa na asilimia 29.0 mwaka 2015. Mchango mkubwa katika Pato la Taifa ulitokana na Sekta ya Kilimo, ikifuatiwa na Sekta nyingine za kiuchumi.
Kwa kuwa asilimia kubwa ya Watanzania wanashiriki katika shughuli za kilimo, hivyo kilimo kinachangia kwa kiasi kikubwa kuongeza kipato na kupunguza umaskini. Hivyo basi, unapowekeza kwenye sekta ya kilimo unawekeza kwa theluthi mbili ya watanzania. Unapokuza kilimo unakuza uchumi wa theluthi mbili ya watanzania, na unapoacha kilimo kishuke maana yake umewafukarisha theluthi mbili ya Watanzania. 
Kwa mujibu wa wataalamu wa Uchumi, ili kupunguza umasikini Tanzania kwa kiwango kikubwa, sekta ya kilimo inapaswa kukua kwa asilimia zaidi ya 8% angalau kwa miaka mitatu mfululizo, na ukuaji huo uendelee kukua kwa wastani wa 6% kwa muda miaka kumi mfululizo.
Hali ikoje nchini? Kwa mujibu wa hotuba ya Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya bajeti ya wizara yake kwa mwaka wa fedha wa 2017/18, kwa miaka hii mitatu mfululizo ukuaji wa Kilimo umekuwa ukishuka nchini (Na hivyo ukuaji zaidi wa umasikini). Mwaka 2014 sekta ya Kilimo ilikua kwa 3.4%, Mwaka 2015 Kwa 2.3% na Mwaka 2016 Kwa 2.1%.
Taarifa ya ya robo mwaka ya Benki Kuu nchini (BOT quarterly economic bulletin) inayoishia Disemba 2016 inaonyesha tofauti na anachosema Waziri katika hotuba yake hiyo ya bajeti. Kwa mujibu wa tarifa ya BOT ni kuwa sekta ya Kilimo ilikua kwa kasi ya 0.6% tu kutoka ukuaji wa 2.3%. 65.5% ya Watanzania wote wamejiajiri katika sekta ya Kilimo, hivyo mdororo huu ya sekta ya Kilimo kutoka ukuaji wa 2.5% mpaka ukuaji wa 0.6% ni ishara mbaya mno kwa ustawi wa zaidi ya robo tatu ya Watanzania.
Kwa Vijijini 78% ya Watanzania wanajihusisha na Kilimo. Hii maana yake ni kwamba wananchi wengi vijijini hawafanyi uzalishaji, jambo hili ni hatari sana, ni dalili kuwa ufukara wa watu wetu unazidi. Ni kwa sababu hii, pamoja na uchumi wetu kukua kitakwimu, 7% kwa mwaka kama tunavyoambiwa, lakini bado wananchi wetu walio wengi wanaishi kwenye dimbwi la ufukara, maana msingi (base) ya ukuaji huo wa Uchumi hauhusishi kilimo, hauhusishi zaidi ya robo 3 ya Watanzania. 
Tunajenga uchumi unaowaacha pembeni zaidi ya theluthi 2 ya watanzania wote. Ukuaji huu mdogo wa Kilimo unapaswa kuishtua Serikali kwani ni hatari sana, ni hatari mno. Maana unajenga uchumi unaowaacha karibu zaidi ya robo 3 ya Watanzania kwenye ufukara huko vijijini, ni uchumi unaopanua matabaka ya mafukara na matajiri. Ndio msingi wa umasikini wa wananchi wetu miaka 50 baada ya Uhuru wetu.
Tatizo hasa ni nini? Kwanini ukuaji wa kilimo unashuka na hivyo umasikini wa Watanzania kuzidi? Tatizo kubwa ni sera za Serikali pamoja na utekelezaji wake. Serikali haiwekezi vya kutosha kwenye kilimo, Na hata ikipanga mipango juu ya kilimo haitekelezi kabisa mipango husika au haitekelezi kwa wakati, kiasi matokeo yenye tija yanayotarajiwa hayapatikani kabisa. Tatizo hilo ndio mzizi mkubwa kwenye sekta nzima ya kilimo nchini, na hata kwenye hili sakata la hali mbaya ya pembejeo katika mikoa mitano inayolima korosho zaidi nchini.
Katika bajeti ya mwaka 2015/16, bajeti ya mbolea ya Ruzuku katika Wizara hii ilikuwa ni shilingi bilioni 78. Bajeti ya kwanza ya Serikali ya awamu ya tano ilishusha fedha za ruzuku ya mbolea mpaka Shilingi bilioni 10 katika mwaka wa Fedha wa 2016/17. Hii ilikuwa ishara ya dhahiri ya kukipuuza kilimo, kuwapuuza 65.5% ya Watanzania wote, kutokujali chanzo cha 100% ya chakula chote cha Watanzania, kupuuza sekta inayochangia theluthi moja ya uchumi wa Taifa. Si hivyo tu, katika bajeti ya mwaka 2016/17, bunge liliidhinishia Wizara hii fedha za miradi ya maendeleo katika kilimo, kiasi cha bilioni 100.53. Waziri alilieleza bunge hapa kuwa mpaka Mei 4, 2017, Wizara imepokea shilingi bilioni 3.34, sawa 3.31% ya fedha zote za maendeleo ya kilimo. Jambo hili linasikitisha mno, ni jambo linaonyesha kuwa hatuwajali wanyonge wa Taifa hili.
Kwetu sisi ACT Wazalendo tunaofuata Ujamaa wa Kidemokrasia, Kilimo ndio sekta ya msingi, ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa, ni sekta nyeti ambayo hatutaacha kuisemea, ndio msingi wa waraka huu.

HALI YA UZALISHAJI WA KOROSHO NCHINI PAMOJA NA MCHANGO WA ZAO HILI KATIKA UCHUMI WA TAIFA
katika msimu wa mwaka 2016/2017 uzalishaji wa mazao makuu ya asili ya biashara ambayo ni Korosho, Miwa ya Sukari, Pamba, Mkonge, Kahawa, Chai, Tumbaku na Pareto umepungua na kuongezeka kwa viwango tofauti ingawa uzalishaji wa jumla kwa mazao hayo umeongezeka kufikia tani 881,583, ikilinganishwa na tani 796,502 mwaka 2015/2016. Uzalishaji unaoendelea kwa mwaka 2016/2017 na matarajio kwa mwaka 2017/2018 ni kuzalisha jumla ya tani 953,825 ya mazao hayo kama ilivyooneshwa katika Jedwali Na. 1.
Uzalishaji wa mazao ya Korosho, Sukari na Pareto umeongezeka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo bei nzuri katika zao la Korosho kutokana na Mfumo wa Stakabadhi Ghalani, Ushiriki wa Wanunuzi kutoka nchi za China na Vietnam, pamoja na hamasa iliyotokana na ongezeko la bei. Kwa Takwimu za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) za mwezi Februari mwaka 2017, zao Korosho lililiingizia Taifa fedha za Kigeni, Dola za Kimarekani, milioni 346.6, ukilinganisha na kipindi kama hicho kwa mwaka 2016, ambapo tulipata Dola za Kimarekani milioni 184.9, kiasi hicho kinalifanya zao la korosho kuwa zao namba 1 la kuingiza fedha nyingi za kigeni hapa nchini kwetu.
Jedwali Na. 1 Uzalishaji wa Mazao ya Asili ya Biashara (Tani) kati ya 2015/2016 na 2017/2017 na matarajio kwa mwaka 2017/2018.
Zao
2015/2016
2016/2017
 2017/2018
Pamba
149,445
122,000
150,000
Chai
32,629
31,000
35,000
Pareto
2,011
2,500
2,600
Korosho
155,416
260,000
300,000
Mkonge
42,314
42,000
43,000
Sukari
293,075
329,840
324,325
Kahawa
60,921
47,999
43,000
Tumbaku
60,691
60,691
55,900
Jumla
796,502
881,583
953,825
Ukizitazama takwimu zote hizi kwa undani, utagundua kuwa msimu wa korosho ulioshia Februari mwaka huu katika mikoa ya Lindi, Mtwara, Pwani, Ruvuma na Tanga ndio msimu bora zaidi kuliko yote kwa wakulima tangu tuanze kulima zao hilo nchini. Hiyo ni kwa sababu, kwanza uzalishaji uliongezeka kwa zaidi ya tani 100,000, pili bei ya korosho kupaa kwa zaidi ya mara mbili, bei ya zao hilo ilipanda hadi kati ya Sh3,700 na Sh4,000 kwa kilo, wakati bei elekezi ya msimu iliyokuwa imepitishwa na kikao cha wadau waliokutana Bagamoyo ilikuwa Shilingi 1,300. Miaka ya nyuma wakulima wamekuwa wakiuza korosho zao kwa wastani wa wa Sh1,200 kwa kilo. Uchambuzi wa takwimu uliofanywa na ACT Wazalendo katika minada 10 ya awali iliyokuwa chini ya chama kikuu cha ushirika cha Mtwara na Masasi (Mamcu), unaonyesha kuwa bei ya chini ilikuwa ni Shilingi 2,610 kwa kilo ambayo bado ni kubwa mara mbili ya bei elekezi.
Sababu kuu ya kupanda kwa uzalishaji wa zao la korosho nchini ni kutokana na wakulima kuandaa mashamba yao vizuri, kupiga dawa kwa wakati na hivyo kupata korosho bora kuliko zilizopatikana katika nchi nyingine kama Msumbiji na nyingine za Afrika Magharibi.
Sababu kuu ya kupaa kwa bei ya korosho nchini ni mabadiliko mbalimbali ya kiuzalishaji na kisoko ndani na nje ya nchi, hususan kuporomoka kwa uzalishaji katika nchi maarufu kwa zao hilo kama Vietnam (inayozalisha 58% ya korosho zote duniani). Uzalishaji wa Vietnam ulipungua kwa asilimia 11 mwaka jana kutokana na ukame, huku mahitaji yake yakiongezeka kwa asilimia 53 tangu 2010. Hivyo haikushangaza kwa mara ya kwanza katika historia ya soko la korosho nchini, kushuhudia ushiriki mkubwa wa wazabuni kutoka nchi za China, Singapore na Vietnam tofauti na wazabuni wa kawaida tu kutoka nchini India.
Katika kanuni za biashara, kwa kuongezeka kiwango cha uzalishaji wa korosho nchini kama ilivyokuwa mwaka huu, ilitarajiwa kuwa bei yake ingeshuka zaidi, lakini hapa nchini bei imeongezeka kwa sababu mahitaji ya zao hilo kwenye soko la dunia yalikuwa ni makubwa mno tofauti na uzalishaji wake mdogo. Hivyo utaona kuwa hali ya bei hii kubwa ya korosho nchini, ilitokana na kiasi kikubwa na kuanguka kwa uzalishaji wa zao hilo katika nchi zinazoongoza kama Vietnam.
Sababu nyengine ni udhibiti wa soko wa wakulima kwa kuzuia unyonyaji uliotokana na utaratibu wa uuzwaji holela wa korosho (Kangomba), korosho yote kuuzwa kwa pamoja na kwa uwazi, kwa matakwa ya wakulima ambao wanashirikishwa kuteua mzabuni mwenye bei nzuri kwenye mnada, pamoja na mfumo mpya wa mauzo ya korosho kwa kuendesha minada kila wilaya.
TAARIFA JUU YA HALI YA UPATIKANAJI, USAMBAZAJI NA UGAWAJI WA PEMBEJEO KWA WAKULIMA WA KOROSHO NCHINI
Ongezeko hili la bei ya zao la korosho limeongeza umuhimu wa zao hili kwa wakulima, kama mkombozi wa kuwaondoa kwenye umasikini, na limeleta hamasa kubwa kwenye mikoa hii mitano inayozalisha korosho zaidi nchini, hasa kwa mikoa ya kusini ambapo korosho ndio zao kuu la kilimo pia. Mashamba yaliyotelekezwa yamefufuliwa, vichaka vimefyekwa na mikorosho imepaliliwa. Hata mikoa ambayo kijadi haikuzalisha korosho kama vile Singida, Dodoma, Njombe, Iringa, Njombe na Morogoro nayo imechangamkia fursa hii na kuanza kupanda miche ya korosho.
Pamoja na umuhimu wa zao la korosho kwa uchumi wa nchi, na kwa wakulima wote wa korosho nchini, bado Serikali haijaweka mkazo wa kutosha kuhakikisha zao hili linawaondolea umasikini wananchi, badala yake imekuwa kikwazo cha kuondoa umasikini huo wa wananchi. Tutaeleza.
Tanzania ni nchi mojawapo Barani Afrika kusini mwa jangwa la Sahara yenye matumizi ya chini sana ya mbolea katika ngazi ya wakulima wadogo (smallholder farmers). Kwa sasa Tanzania imefikia kiwango cha kilo 19 tu za virutubisho kwa hekta, yakiwa ni matumizi madogo mno kwa viwango vya dunia, mfano nchi ya China ina wastani wa matumizi ya kilo 210 kwa hekta moja.
Matumizi hayo yetu ya mbolea na virutubisho pia ni kiwango cha chini hata kwa viwango vya Kiafrika. Azimio la Maputo (The Maputo Declaration, 2003) liliazimia masuala mbalimbali katika kilimo, pamoja na mambo mengine; liliweka sharti la kuongeza matumizi ya mbolea katika eneo la ukanda wa SADC kufikia angalau kilo 50 za virutubisho kwa hekta.
Moja ya matatizo makubwa ya uzalishaji wa zao la korosho ni ugonjwa wa ubwiri unga. Ugonjwa huu unasababishwa na vimelea aina ya uyoga (fungus) viitwavyo Oidium anacardii. Ugonjwa huu ni hatari sana, kiasi kwamba kama haukuthibitiwa, unaweza kupunguza mavuno kwa zaidi ya asilimia 70, ugonjwa huu umeenea katika mikoa yote inayolima zao hili Tanzania. Hapo awali ugonjwa huu ulikuwa unaitwa kwa jina la “ukungu” kutokana na uhusiano wake mkubwa na hali ya hewa ya ukungu (litabwe kwa Kimakonde) unaoonekana alfajiri/asubuhi katika miezi ya Juni - Septemba. Hivyo basi, jina la Ubwiri unga linatumika sasa ili kuwawezesha wakulima wasichanganye vitu hivyo viwili.
Ugonjwa huu unashambulia maeneo yote machanga na teketeke katika mti wa mkorosho, hasa machipukizi, majani, maua, mabibo na korosho changa (tegu). Athari kubwa ya ugonjwa huu inatokana na mashambulizi ya maua, ambayo hushindwa kufunguka na kuwezesha chavua kufanya kazi yake, hatimaye hunyauka na kukauka.
Dawa ya Salfa (Sulphur) ndiyo dawa inayotumika kwa wingi zaidi kukinga ugonjwa wa ubwiri unga. Dawa hii ambayo ni ya unga, inapulizwa kwa kutumia mashine maalumu (motorized blower) ya kupulizia dawa km. Maruyama. Kiwango cha gramu 250 kwa mti, kwa mzunguko, ndicho kinapendekezwa. Hivyo basi kwa mizunguko mitano kiasi cha kilo 1.25 cha salfa kwa mti kwa mwaka kinahitajika.
Wakati sahihi wa kuanza upuliziaji unaanza pale ambapo karibu asilimia 20 za maua yamejitokeza na wakati zaidi ya asilimia 5 ya maua hayo tayari yawe yanaonyesha dalili za ugonjwa.
Sababu kuu ya kupanda kwa uzalishaji wa zao la korosho nchini kwa msimu uliopita ni kutokana na wakulima kuandaa mashamba yao vizuri, kupiga dawa ya Salfa kwa wakati na hivyo kupata korosho bora kuliko zilizopatikana katika nchi nyingine kama Msumbiji na nyingine za Afrika Magharibi. Serikali yetu inataka kuua uzalishaji huu mkubwa wa wakulima wetu.
Nini Kimetokea? Mwezi Mei mwaka huu, kwenye kikao cha mwaka cha wadau wa zao la korosho kilichofanyika mjini Dodoma, Serikali ilitangaza uamuzi wa kugawa pembejeo bure kwa wakulima wote wa zao la korosho. Uamuzi huo ulitangazwa na waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, ndugu Charles Tizeba mbele ya Waziri Mkuu, ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano huo. Kutangazwa kwa uamuzi huu kuliibua shangwe kubwa kwa wakulima wa korosho ambao walifurahia kupunguziwa mzigo wa kununua pembejeo.
Uamuzi huu ulileta matokeo yafuatayo:
  1. Mfumo wa Pembejeo ya ruzuku ulifutwa.
Kabla ya mfumo wa kugawa pembejeo bure kutangazwa, kulikuwa na mfumo wa pembejeo uliokuwa ukiendeshwa na Vyama vya Msingi vya ushirika (Amcos). Vyama hivi vya msingi vya ushirika vilikuwa vinakusanya fedha kwa wakulima wakati wa mauzo (kiasi cha shilingi 15,000 tu kwa mfuko), kununua pembejeo nje ya nchi na kugawa kwa wakulima.
  1. AMCOS Walirudisha Fedha za Wakulima
Kabla ya kutangazwa kwa uamuzi huu, vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) vilikuwa vimeshakusanya fedha kwa wakulima na vinajipanga kununua Salfa nje ya nchi. Kwa uamuzi huu wa serikali, vyama vya ushirika viliamriwa kuwarudishia wakulima fedha zilizokusanywa kwa sababu “Pembejeo ya bure” ingeletwa.
  1. Wakulima Walizitumia Fedha Zilizorejeshwa Kutoka Amcos
Baada ya wakulima kurejeshewa fedha zao kutoka kwa vyama vyao vya msingi vya ushirika (Amcos), wengi wao walizitumia fedha hizo kwa matumizi mengine kwa kuwa walikuwa na uhakika wa kupata pembejeo ya bure kutoka serikalini.
  1. Waagizaji Binafsi “Waliufyata”
Mbali na vyama vya ushirika, pembejeo huuzwa pia kwenye soko na wafanyabiashara binafsi. Kwa msimu wa mwaka 2016/2017, pembejeo aina ya Salfa, ambayo ndiyo maarufu zaidi, iliuzwa kati ya shilingi 3000 - 35,000 kwa mfuko mmoja, na wauzaji binafsi. Kutangazwa kwa ujio wa Salfa ya bure kuliwafanya wafanyabiashara wengi binafsi kukhofia kukosa soko la Salfa na pembejeo nyingine muhimu walizoagiza na hivyo kupata hasara.
Kinyume na ahadi ya serikali ya kuleta pembejeo ya bure, ya kutosha na kwa wakati, hali imekuwa tofauti mno. Matatizo makubwa yametokea kama ifuatavyo;
  1. Pembejeo Hazikuletwa kwa Wakati
Kwa mfano katika Wilaya ya Nachingwea, Mkoani Lindi, ambayo iliongoza kwa uzalishaji wa korosho katika msimu uliopita kwa kuzalisha tani 20,000 huwa inapofikia mwezi Mei kila mwaka wanakuwa wameanza kupuliza dawa hizo. Lakini mpaka mwezi wa Juni mwishoni pembejeo husika hazikuwa zimefika. Hali hiyo iko hivyo kwa mikoa yote mitano.
Watafiti wa Chama chetu waliojikita kwenye wilaya hii kwa sababu ndiyo wilaya iliyoongoza kwa uzalishaji, walizungumza na wananchi, wakulima, viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika ambao kwa undani walielezea hali ilivyo na kuitupia lawama serikali kwa ucheleweshaji huo wa pembejeo.
Maelezo haya ya wakulima kwa watafiti wetu hayakuwa tofauti na maelezo waliyoyatoa mbele ya viongozi wa serikali. Mfano, Juni 22, 2017 wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara, mbele ya mkuu wa wilaya ya Nachingwea, Rukia Muwango, uliofanyika katika kijiji cha Mpiruka A, mkutano ambao viongozi wa ACT Wazalendo walihudhuria, wakulima hawa walionyesha kukatishwa tamaa na uchelewehwaji wa pembejeo, na matumaini yao ya uzalishaji mkubwa kama msimu uliopita yameanza kufifia kabisa.
  1. Pembejeo Zilizoletwa ni Kiduchu Mno.
Hata baada ya pembejeo hizo kuletwa, mwezi huu (Julai) mwanzoni, bado kasma iliyopelekwa haikidhi haja na mahitaji yaliyopo, maana ni ndogo mno. Kwa mfano, Wilaya ya Tunduru, Mkoani Ruvuma, yenye mahitaji ya tani 5,000 za Salfa kwa msimu huu wa uzalishaji, imepewa mgao wa tani 1000 tu Salfa, ambayo ni 20% ya mahitaji yote.
Mfano mwengine ni Wilaya ya Nachingwea, wilaya iliyoongoza kwa uzalishaji wa korosho nchini katika msimu uliopita, kwa mujibu wa mkuu wa Wilaya hiyo, mahitaji halisi ya dawa ya Salfa ya unga ni tani 20,000. Hata hivyo mgao ulitolewa na bodi ya korosho ni tani 1300 tu, ikiwa ni 6.5% ya mahitaji ya wilaya nzima.
Hii imesababisha wakulima wengi kutopata kabisa Salfa, na hivyo kuwaacha bila pembejeo kwa mikorosho yao. Hata kwa waliopatiwa Salfa, wengi wao wamepata wastani wa mfuko mmoja unaotosha kupulizia hekari moja tuu yenye mikorosho 30 tu. Hii ni kinyume na ahadi ya serikali kugawa Salfa, na hivyo hata kwa mkulima mdogo tu mwenye hekari chache kutopata pembejeo za kutosha. Kinyume na ahadi ya Serikali ya kutoa bure pembejeo za kutosha.
  1. Pembejeo Zilizoletwa Kutokuwa na Ubora
Yapo madai kutoka katika wilaya za mikoa yote mitano ambazo Viongozi na Watafiti wa ACT Wazalendo walizungumza na wananchi, wakulima pamoja na viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos) kuwa Salfa husika iliyosambazwa, pamoja na kutofikishwa kwa wakati na kuwa kidogo mno, bado ina ubora duni kwa sababu ya kujaa chengachenga zinazopunguza ufanisi wakati wa kupulizia.

Jedwali Na. 2 Bei za Salfa katika baadhi ya Wilaya zinazozalisha zao la korosho zaidi nchini.
Eneo
Bei ya Salfa (Amcos)
Bei ya asili ya Wafanyabiashara
Bei ya sasa ya Wafanyabiashara
Nachingwea
15,000
30,000
80,000
Kilwa
15,000
35,000
Pembejeo ya  Salfa haipatikani kabisa
Liwale
15,000
35,000
53,000
Tandahimba
15,000
35,000
55,000
Masasi
15,000
30,000
90,000
Newala
15,000
30,000
70,000 – 80,000
Tunduru
15,000
35,000
70000-80000
Mtwara Mjini
15,000
30,000
50,000
Mtwara Vijini
15,000
35,000
55,000
Ruangwa
15,000
35,000
60,000 – 80,000
Lindi Mjini
15,000
35,000
60,000 – 80,000
Lindi Vijijini
15,000
35,000
60,000 – 100,000
Nanyumbu
15,000
35,000
90,000
Ndanda
15,000
35,000
90,000
Rufiji
15,000
35,000
70,000
Mkinga
15,000
35,000
70,000
Mkuranga
15,000
35,000
70,000
Kisarawe
15,000
35,000
70,000
Nanyamba
15,000
35,000
90,000
Baada ya kugundua kuwa serikali imefeli kutekeleza ahadi yake ya kugawa Salfa yenye ubora bure, kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa, wakulima wameamua kupambana binafsi ili kunusuru mikorosho yao, mustakabali wao na kujiepusha na kuzama kwenye ufukara, kwa kila mmoja kwa nafasi yao kujaribu kununua Salfa kutoka kwa wafanyabiashara binafsi. Kwa wafanyabiashara binafsi, jambo hili limegeuka fursa kwao, baada ya kugundua kuwa Serikali imefeli katika kutimiza ahadi yake wafanyabiashara hawa wametumia fursa hiyo kujitajirisha, kwanza kwa sababu ya uhaba wa Salfa, pili kwa kuwa wanajua wakulima hawana njia mbadala ya kupata Salfa tofauti na kwao wao.
Bei ya Salfa inapanda kila uchwao kwa kasi ya roketi. Kwa mfano, kwa Wilaya ya Tunduru, kwa kipindi cha mwezi mmoja tu wa Julai, bei ya mfuko mmoja wa Salfa imepaa kutoka 35,000 hadi 100,000 sawa na ongezeko la zaidi ya 200%. Kiwango hicho cha bei juu ya Salfa hakijawahi kushuhudiwa tangu kilimo cha korosho kianze nchini, uzembe wa Serikali unawaletea mateso wananchi.
Wakulima wachache wenye akiba ya fedha wanatumia akiba yao ambayo wangeitumia kwenye shughuli za maendeleo kununulia Salfa kwa matumaini hafifu kuwa “Dhahabu ya Kusini” itawalipa. Wengi wanayatazama mashamba yao waliyoyapalilia kwa uchungu kwa sababu hawana namna ya kufanya. Furaha yao ya awali ya kupata Salfa ya bure imegeuka kilio kikuu.
Tujiulize maswali haya:
  1. Je Serikali Ilikuwa na hakika au ilikuwa inafanya mzaha na siasa tu kwa ahadi yake hewa ya pembejeo za bure inayogharimu maisha ya wakulima?
  2. Je Serikali Ilifanya uchambuzi wa kina kuhusu mahitaji halisi ya pembejeo ya wakulima wa korosho nchini, na uwezo wa Serikali au ilikurupuka tu?
  3. Waziri Mkuu, Waziri wa kilimo na Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho walipohakikishia wakulima kuwa pembejeo itapatikana kwa wingi, walimaanisha hii hii iliyokuja kwa kuchelewa, isiyo na ubora na iliyogawiwa kwa uchache au kuna nyingine inakuja?
  4. Serikali ilipovunja mfumo wa pembejeo ya ruzuku chini ya vyama vya msingi vya ushirika vya walikuwa na nia njema na wakulima?
Ni dhahiri kuwa Serikali hii imeshindwa kuwajali wakulima hawa, ni dhahiri kuwa kuwa Serikali imeshindwa kuendesha uchumi wan chi hii.
MAPENDEKEZO YA ACT WAZALENDO
Ni dhahiri kuwa Serikali ya CCM wameshindwa kuendesha uchumi wa Taifa, imeshindwa kutimiza ahadi zake kwa wakuliwa wa korosho, imevunja na kuharibu mfumo imara wa wakulima wenyewe kupata pembejeo kwa wakati na kwa bei nafuu, haijui ukubwa wa tatizo ililolitengeneza kwa kuwa haishughuliki na masuala ya wananchi bali inashughulika na na hujuma dhidi ya vyama vya upinzani tu. Ni dhahiri kuwa hali iliyoko sasa ikiachwa iendelee itapunguza uzalishaji wa korosho nchini, itapunguza kipato cha wananchi, na itawadidimiza kwenye ufukara.
Kutokana na hali hiyo, Chama cha ACT Wazalendo kinatoa wito kwa serikali ya CCM kuchukua hatua za haraka kurekebisha mambo, ikiwemo:
HATUA ZA DHARURA:
  1. Serikali ifanye haraka kutimiza ahadi yake ya kufikisha pembejeo ya bure kwa wakulima wa korosho, kwa kuhakikisha inafikisha kiwango cha pembejeo kinacholingana na mahitaji yaliyoko. Taarifa juu ya mahitaji ya wakulima ziko Serikalini, ni muhimu serikali ipeleke pembejeo kulingana na mahitaji. Serikali ichukue hatua za dharura kuagiza pembejeo kuondosha uhaba wake.
  2. Serikali inunue pembejeo zote kutoka kwa wafanyabiashara binafsi, na kuigawa bure kwa wananchi kama ilivyoahidi wakati, au itoe ruzuku kuhakikisha kuwa wakulima watanunua kwa bei ya Amcos ya 15,000 kwa mfuko mmoja.
  3. Serikali ichukue hatua kali dhidi ya wauzaji wa pembejeo wanaopandisha bei ya pembejeo kila siku bila huruma. Ongezeko la sasa la hadi shilling 100,000 kwa mfuko mmoja wa Salfa halina utetezi wowote wa kibiashara zaidi ya uchu wa kutumia uhaba wa pembejeo uliosababishwa na uzembe wa serikali kujitajirisha.
  4. Serikali ichunguze ubora wa Salfa inayogawiwa ambayo inalalamikiwa na wakulima kuwa na ubora duni.
  5. Serikali ichukue hatua kali dhidi ya wafanyabiashara wanaolalamikiwa kuchanganya unga wa nafaka kwenye sulphur ili kujipatia faida maradufu.

HATUA ZA MUDA WA KATI:
  1. Serikali ifanye uchambuzi wa kina wa mahitaji halisi ya kila mkulima na kuwa na uhakika wa bejeti yake ndipo itangaze na kutekeleza mfumo wa Salfa ya bure. Isikurupuke tu kwa lengo la kutaka sifa.
  2. Serikali itoe taarifa za uhakika mapema kuhusu upatikanaji wa pembejeo badala ya kutoa taarifa za hadaa. Kwa miaka mingi wananchi wamekuwa wakijinunulia pembejeo wenyewe. Ni bora serikali ieleze wazi juu ya uwezo wake ili wakulima waweze kujiandaa mapema kwa kujiwekea akiba kwa ajili ya kununua pembejeo.
  3. Iwapo serikali serikali itakuwa haina uwezo wa kugawa Salfa yote bure, kama ilivyoonekana, ieleze kwa undani kiwango inachoweza kutoa bure, na iimarishe mfumo wa pembejeo kupitia Amcos kama ilivyokuwa kawaida.
HATUA ZA MUDA MREFU:
  1. Kufungamanisha sekta ya korosho na hifadhi ya jamii ili kupitia fao la bei kuweza kuweka uimara wa bei za mazao na pembejeo. Fao la bei litalinda ustawi wa wakulima wa korosho na kuwaepusha na hasara iwapo bei ya korosho ya msimu huu itaanguka tofauti na msimu uliopita. Hilo litawezekana kwa kutunga Sheria kuwezesha mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutoa mafao ya Bima ya Afya, Bima za Mazao na majanga (Crop Insurance) kwa kilimo na mifugo na Fao la Bei (Price Stabilization Benefit).
  2. Kuwaunganisha wakulima wote wa korosho nchini katika hifadhi ya jamii, na hivyo kuwa na uhakika wa akiba uzeeni kama ilivyo kwa wafanyakazi wa sekta rasmi pamoja na kupata faida ya Bima ya Afya, na hivyo matibabu bure yatokanyo na mifuko ya hifadhi ya jamii. Mchango kwa watu walio nje ya sekta rasmi ni shilingi 20,000 tu kwa mwezi.
  3. Kupanua hifadhi ya jamii na kuwafikia wakulima, wafugaji na wananchi wengine waliojiajiri kwa kutunga sheria itakayopelekea Serikali kuchangia theluthi moja ya kila mchango wa mwananchi atakayechangia kima cha chini cha michango kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. Kwa sasa mchango wa 20,000 wa mtu asiye kwenye sekta rasmi unabaki kama ulivyo tu bila kujaliziwa.
  4. Serikali ichochee Tija kwenye Kilimo cha korosho kwa kuhakikisha tunaongeza thamani ya mazao ya korosho hapa nchini kwa kuhimiza kupunguza uuzaji wa korosho ghafi. Jambo hilo litawezekana kwa uwekezaji mkubwa wa viwanda vya ubanguaji wa korosho.
  5. Kutumia Hifadhi ya Jamii kuwezesha wakulima kujiwekea akiba kupitia vyama vyao vya msingi vya ushirika (Amcos) na kupata mikopo ya gharama nafuu ili kuanzisha upanuzi wa kilimo chao, uongezaji thamani wa mazao na kupata Bima ya Afya.
  6. Kutumia Hifadhi ya Jamii kuwekeza kwenye miradi mikubwa kama miundombinu ya kilimo, viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, vyuo vya ufundi na miundombinu ya usafirishaji mazao kama reli kwani kwa uasili wake madai dhidi ya mifuko (liabilities) ni ya muda mrefu.
Hitimisho: Sisi kama chama cha siasa, kwa kuzingatia falsafa ya chama chetu ya Siasa ni Maendeleo, tunaendelea kusisitiza kuwa Serikali ni lazima itimize wajibu wake wa kulinda maisha na hali za wananchi kwa kuhakikisha hakuna uhaba wa pembejeo kwa wakulima hawa wa korosho nchini, kuhakikisha kuwa pembejeo husika znapatikana katika bei ambayo watanzania wanaimudu, na zinapatikana kwa wakati. 
Ado Shaibu – Katibu, Kamati ya Itikadi, Mawasiliano ya Umma na Uenezi
ACT Wazalendo
Julai 30, 2017

Dar es salaam, Tanzania

No comments: