Watu wanaoishi na ualbino katika
maeneo ya vijiji nchini Tanzania wanaendelea kuishi kwa hofu miongoni mwa
mitazamo mingi hali inayosababisha ukatili dhidi yao, mtaalamu mmoja wa Haki za
Binadamu wa Umoja wa Mataifa alihitimisha baada ya ziara yake ya kwanza hapa
nchini.
Mtaalamu wa kujitegemea kuhusu kunufaika na haki za
binadamu kwa watu wenye ualbino, Ikponwosa Ero, alisema bado kunahitajika kazi
zaidi ili kutatua tatizo la imani ya kiuchawi na kuelimisha umma.
“Watu wenye ualbino wanaendelea kuishi katika hali
dhaifu, sanjari na sababu za msingi za mashambulizi dhidi yao zikiwa bado juu, na
madhara ya zaidi ya muongo mmoja ya ukatili yalisababisha mlolongo wa athari
mbaya,” alisema mwishoni mwa ziara yake ya siku 11 nchini Tanzania. “Watu
wanaendelea kuishi katika hofu, hasa katika maeneo ya vijijini.”
Hata hivyo, Bi. Ero alifurahishwa na taarifa ya
kupungua kwa idadi ya mashambulizi yaliyoripotiwa na aliipongeza serikali ya
Tanzania kutokana na juhudi zake za kushughulikia tatizo hili – lilijojikita
katika imani potofu ya kwamba viungo vya binadamu wenye ualbino vina thamanni
katika vitendo vya kishirikina.
“Ninakaribisha hatua zilizochukuliwa na Serikali na
Asasi za Kiraia, na hali ya kupungua kwa idadi ya mashambulizi yaliyoripotiwa,”
alisema. “Kumekuwepo na hatua chanya ili
kushughulikia vitendo vya kichawi, pamoja na usajili wa waganga wa tiba ya
jadi.”
“Hata hivyo, uangalizi kamili wa kazi yao
haujafanikiwa, na bado kunaendelea kuwepo kwa hali ya mkanganyiko katika fikra
za wananchi kwa ujumla baina ya vitendo vya kiuchawi na kazi ya waganga wa tiba
ya jadi,” alisema Mtaalamu wa kujitegemea.
Bi. Ero aliweka mkazo juu ya saratani ya ngozi kuwa
tishio kubwa linalohatarisha maisha ya watu wenye ualibino kuliko mashambulizi.
, na alisema ni kipengele kingine kinachohitahitaji juhudi nyingi.
“Ni faraja kubwa kuona Serikali ikiwa inafanya kazi
bega kwa bega na Asasi za Kiraia katika sekta ya elimu na ya afya, hasa kwa kutoa
vifaa vya kuona na matumizi ya kliniki ya kuhama ili kuzuia kansa ya ngozi,” alisema.
“Ila programu hizi zinahitaji mno ushirikishwaji wa
Serikali, ili kuwafikia watu wengi zaidi na kuhakikisha kwamba kazi hii inakuwa
endelevu.”
Bi. Ero pia alisisitiza kuhusu wasiwasi kuhusu
shule zinazotumika kama vituo vya ulinzi na usalama kwa ajili ya watoto wenye
ualbino, ambako wakati mwingine vituo hivyo vilibadilika toka kuwa makazi ya
muda na kugeuka kuwa makazi ya kudumu.
“Licha ya kuwa na dhamira nzuri ya ulinzi wa kuwahifadhi
watoto wenye ualbino katika vituo vya shule kwa ajili ya malazi yenye ulinzi
thabiti, inaonekana kwamba maeneo haya siyo tena ya muda,” alisema.
“Wanafunzi wanaosoma shule za sekondari au vyuo
hawana chaguo lingine ila kurudi tena katika maeneo walimopata hifadhi baada ya
kumaliza kipindi cha likizo kwa sababu wanahofu kurejea tena majumbani kwao,” alisema
mtaalamu huyo. “Niliwahi kupokea ripoti kama hizi za watoto wanaosoma shule za
msingi wanaohifadhiwa katika mabweni ya vituo hivi vinavyotoa malazi kwa watoto
hawa.”
Bi. Ero alikaribisha upungufu mkubwa mno wa idadi
ya jumla ya watoto katika vituo vya hifadhi, na aliwapongeza viongozi kutokana
na bidii walioifanya kwa kuwaunganisha watoto hao na familia zao, ila aliongeza
kusema kwamba bado kunahitajika kazi zaidi.
“Serikali inatakiwa kuendelea kuuelimisha umma na
kuimarisha hatua za ulinzi, kwa sababu jamii kadha wa kadha hazikotayari
kuwapokea watoto hawa,” alisema.
Katika ziara yake nchini
Tanzania, Bi. Ero alikutana na viongozi mbalimbali wa ngazi ya juu na mashirika
ya asasi za kiraia. Alitembelea mji mkuu wa Dodoma na jiji la Dar es Salaam, na
pia alisafiri na kwenda maeneo ya kanda ya kaskazini ili kutembelea Mwanza,
Shinyanga na Kigoma..
Alikutana na watu wenye ualbino,
pamoja na wale waliosumbuliwa na vuguvugu la mashambulizi, na wanafamilia wao.
Mtaalamu wa kujitegemea, aliyeteuliwa na Baraza la
Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Haki za Binadamu, anachunguza ukiukwaji wa haki zote dhidi ya watu wenye ualbino katika
nchi mbalimbali, pamoja na mashambulizi, kuishi katika hofu ya kushambuliwa na watu
wenye ualbino kuachwa kando katika malengo ya maendeleo. Aliwahi pia
kubaini na kuhamasisha mifano bora, na kupambana dhidi ya kasumba, chuki na
vitendo viovu vinavyosababisha ukiukwaji wa haki za binadamu.
No comments:
Post a Comment