Kamati mpya ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), tayari imekutana kwa mara ya kwanza baada ya kuteuliwa mapema wiki iliyopita na Kamati ya Utendaji ya TFF.
Mara baada ya kikao hicho cha jana Jumamosi, Kamati imeweka hadharani majina ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uchaguzi, kinyang'anyiro kinachotarajia kufanyika Agosti 12, mwaka huu mkoani Dodoma.
Katika kinyang'anyiro hicho, wagombea watatu wa nafasi ya urais hawakupitishwa akiwemo Jamal Malinzi ambaye alikatwa kutokana na kutohudhuria usaili kinyume cha kanuni ya 11 (7) ya kanuni za uchaguzi za TFF.
Mgombea mwingine ambaye hajapitishwa kuwania nafasi hiyo ni Fredrick Masolwa ambaye hajapitishwa kwa kukosa uzoefu kwa mujibu wa kanuni ya 9 (3) ya kanuni za uchaguzi za TFF.
John Kijumbe aliondolewa katika kinyang'anyiro hicho kwa kukosa uzoefu huku Athumani Nyamlani alijitoa kuwania uongozi wa Shirikisho hilo.
Waliopitishwa kuwania urais na Mwenyekiti wa Kamati ya uchaguzi, Wakili Revocatus Kuuli ni Imani Madega, Fredrick Mwakalebela, Wallace Karia, Ally Mayay, Shija Richard na Emmanuel Kimbe.
Nafasi ya Makamu wa Rais aliyejitoa ni Geofrey Nyange Kaburu ambaye anakabiliwa na tuhuma ya makosa matano yakiwemo ya utakatishaji fedha kwa klabu ya Simba huku waliopitishwa ni Mulamu Ng'ambi, Michael Wambura, Mtemi Ramadhani, Robert Selasela na Stephen Mwakibolwa.
Kwa mujibu wa Kuuli, zoezi linalofuata kwa sasa ni kuhakiki kwa vyeti vya kidato cha nne kwa kila mgombea baada ya kupitisha majina.
Kanda namba 1 ya Mikoa ya Kagera na Geita: waliopitishwa ni Saloum Chama, Leopold Mukebezi na Kaliro Samson huku Abdallah Mussa aliondolewa katika hatua za awali kwa kutoambatanisha cheti cha elimu ya sekondari.
Kanda namba 2 inayounganisha mikoa ya Mara na Mwanza: Vedastus Lufano, Ephraim Majinge, Samwel Daniel na Aaron Nyanda (Wamepitishwa) huku Kanda namba 3 (Mikoa ya Shinyanga na Simiyu) Stanslaus Nyongo, Mbasha Matutu na Bannista Rugora (wamepitishwa).
Kanda namba 4 (Mikoa ya Arusha na Manyara) waliopitishwa ni Omar Walii, Sarah Chao na Peter Temu (wamepitishwa), Kanda namba tano inayounganisha mikoa ya Kigoma na Tabora waliopitishwa ni John Kadutu, Issa Bukuku, Abubakar Zebo na Francis Michael.
Kanda namba 6 yenye mikoa ya Katavi na Rukwa Keneth Pesambili na Baraka Mazengo – wote wamepitishwa huku Kanda namba 7 Mbeya na Iringa waliopitishwa ni Cyprian Kuyava, Elias Mwanjala na Erick Ambakisye ilhali Abdusuphyan Sillah hajapitishwa kwa kukosa uzoefu.
Kanda namba 8 mikoa ya Njombe na Ruvuma waliopitishwa ni Golden Sanga, James Mhagama, Vicent Majili na Yono Kevela huku Kanda namba 9 Lindi na Mtwara Athumani Kambi na Dunstan Mkundi (wamepitishwa).
Kanda namba 10 Dodoma na Singida waliopitishwa ni Hussein Mwamba, Steward Masima, Mohamed Aden, Ally Suru na George Komba (wamepitishwa) huku Mussa Sima hajapitishwa kwa kukosa uzoefu.
Kanda namba 11 Pwani na Morogoro waliopitishwa ni Charles Mwakambaya, Gabriel Mkwawee na Francis Ndulane huku Hassan Othuman hajapitishwa kwa kukosa uadilifu huku Kanda namba 12 Kilimanjaro na Tanga waliopitishwa ni Khalid Mohamed na Godluck Moshi wamepitishwa wakati Thabity Kandoro hajapitishwa kwa kukosa uzoefu.
Kanda namba 13 Dar es Salaam: waliopitishwa ni Abdul Sauko, Emmanuel Kazimoto, Ayoub Nyenzi, Shaffih Dauda, Peter Mhinzi, Lameck Nyambaya, Mussa Kissoky, Said Tulliy, Ally Kamtande, Aziz Khalfan, Ramadhani Nassib na Saad Kawemba.
Wakati Saleh Abdallah hajapitishwa kwa kukosa uzoefu, Jamhuri Kihwelu na Bakari Malima (hawajapitishwa kwa kushindwa kuwasilisha vyeti vya elimu ya sekondari).
|
|
|
MCHAKATO WA UCHAGUZI RUREFA NA LIPULI
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), iliyokutana Julai 8, mwaka huu pamoja na mambo mengine pia ilijadili mchakato wa chaguzi za Mkoa wa Rukwa (RUREFA) na timu ya Lipuli inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom.
Kuhusu mchakato wa uchaguzi Mkoa wa Rukwa (RUREFA), Kamati ya Uchaguzi inayoongozwa na Mwenyekiti Msomi Wakili Revocatus Kuuli, imeagiza zoezi hilo liendelee na inamtuma Mjumbe wake siku ya usaili, Msomi Wakili Thadeus Karua kwa ajili ya kushuhudia.
“Na pia Kamati ya Uchaguzi itawatuma wajumbe siku ya uchaguzi tarehe 5 Agosti, 2017,” imesema kamati hiyo ilipoagiza kuhusu kuendelea kwa uchaguzi huo.
Kuhusu uchaguzi wa Lipuli, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi, Msomi Wakili Kuuli, imemwagiza Katibu Mkuu wa klabu hiyo, kuendelea na maandalizi ya uchaguzi kama ilivyoelekezwa na kamati kwamba ufanyike Agosti 5, mwaka huu.
“Na Kamati inamtuma mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi Msomi Wakili Mohamed Ally Mchungahela kwa ajili ya uangalizi siku ya uchaguzi,” imesema sehemu ya taarifa ya kamati kwa uongozi wa Lipuli.
Kamati imesisitiza, “Na wanachama waendelee kulipia ada za uanachama kwa kuwa watakaoruhusiwa kupiga kura ni wanachama hai tu.”
KARIA AWAPONGEZA WASHINDI TWFA
Kaimu Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amewapa kongole viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu kwa Wanawake (TWFA), waliochaguliwa kwenye Uchaguzi Mkuu uliofanyika jana kwenye Ukumbi wa Hoteli ya Chichi, Dar es Salaam.
Katika uchaguzi huo uliopata uwakilishi wa theluthi mbili ya mikoa yote ya Tanzania, Amina Karuma alitetea kiti chake kwa kupata kura 47 kati ya 52 za wapigakura wote huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti ikichukuliwa na Rose Kissiwa ambaye aliyepata kura 42.
Mwanahabari Mkongwe wa Gazeti la Nipashe kutoka Jumba la Magazeti la The Guardian, Somoe Ng’itu alishinda nafasi ya Katibu Mkuu kwa kuvuna kura 49 ilihali Theresia Mung’ong’o alishinda nafasi ya Katibu Msaidizi.
Hilda Masanche alishinda nafasi ya Mweka Hazina wa TWFA kwa kupata kura 25 wakati Mwanahabari mwingine Zenna Chande alishinda nafasi ya Ujumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF kwa kupata kura 44.
Wajumbe Triphonia Temba, Mwamvita Kiyogoma, Jasmine Soudy na Chichi Mwidege hawakushinda baada ya wagombea wote wanne kutopata zaidi ya nusu ya kura kulingana na idadi ya wapigakura kwa mujibu wa katiba ya TWFA.
Uchaguzi huo ulisimamiwa na Mwenyekiti Kamati ya Uchaguzi ya TWFA, Msomi Wakili George Mushumba, ambaye pia aliwapongeza washindi.
Awali akifungua mkutano huo wa uchaguzi, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, Salum Madadi aliwataka wajumbe hao kuwa makini katika kuchagua na kwamba si wakati wa kufanya mzaha katika soka la wanawake.
……………………………………………………………..……………………………………………………….
IMETOLEWA NA SHIRIKISHO LA MPIRA WA MIGUU TANZANIA
|
No comments:
Post a Comment