Tuesday, August 15, 2017

BENKI YA EXIM TANZANIA YASHEHEREKEA MIAKA 20 YA HUDUMA KWA KUWEKEZA MILIONI 200 KATIKA SEKTA YA AFYA

15 Agosti 2017, Dar es Salaam. Benki ya Exim Tanzania imeadhimisha miaka 20 ya huduma kwa kuzindua mradi wa mwaka mzima unaoitwa “miaka 20 ya kujali jamii” ambao utawekeza shilingi milioni 200 katika sekta ya afya Tanzania. Mradi huu unalenga kusaidia upungufu wa vitanda katika hospitali nchini hivyo benki ya Exim itatoa magodoro 500 na vitanda katika hospitali za serikali mikoa 13 nchini.
Mkurugenzi wa fedha wa Exim benki Bw. Selemani Ponda akiongea na waandishi wa habari pamoja na wageni walioudhuria kwenye tafrija fupi ya kukabidhi vitanda kwenye hospitali ya Temeke (kushoto) kwake ni kaimu mganga mkuu wa hospitali hiyo Bi. Husna Msangi.
Haya yalitamkwa katika sherehe za kuadhimisha miaka 20 ya benki hiyo iliyofanyika katika hospitali ya Temeke jijini Dar es Salaam, ikiwa ni hospitali ya kwanza zitakazofikiwa na mradi huo.

Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa kitengo cha fedha cha benki ya Exim Selemani Ponda alisema, “ Mwaka huu benki ya Exim imefikia hatua muhimu sana. Tunasheherekea miaka 20 ya uvumbuzi na kujitolea kwa jamii. Kwa miaka mingi benki ya Exim imewekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya afya, mazingira na elimu nchini. Tunatambua juhudi za serikali katika kuboresha huduma za afya hivyo basi tumejitolea mwaka huu mzima kuwekeza katika hospitali za serikali katika maeneo mbalimbali nchini.”
Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya Temeke Bi. Husna Msangi akiongea na waandishi wa habari pamoja na wageni walioudhuria kwenye tafrija fupi ya kukabidhiwa vitanda na magodoro kwenye hospitali hiyo mapema leo jijini Dar es salaam (kushoto) kwake ni Katibu wa afya wa hospitali hiyo Bi. Sanura Kondo.
Hospitali na kliniki nyingi nchini zina tatizo la ukosefu wa dawa, vifaa na vitanda hasa katika hospitali za rufaa. Takwimu za Shirika la afya duniani ‘WHO’ zinaonyesha kuwa Tanzania ina uwiano wa vitanda saba kwa kila watu elfu kumi. Hivi sasa hali ya kuona wakinamama wajawazito wawili wakitumia kitanda kimoja au wengine kulala sakafuni ni jambo la kawaida katika hospitali hizi.

Daktari Mkuu wa hospitali ya Temeke Dkt. Gwamaka Mwabulambo alisema, “ Upungufu wa vitanda katika hospitali ya Tememke ni changamoto kubwa. Tunahitaji vitand  katika wodi ya watoto na wodi ya wazazi. Msaada huu kutoka benki ya Exim wa hivi vitanda 40 na magodoro utasaidia sana katika kupunguza changamoto hii katika hospitali yetu.”
Baadhi ya wafanyakazi wa Exim Benki pamoja na waandishi wa habari warioudhuria kwenye tafrija fupi ya kutoa misaada ya vitanda na magodoro kwenye hospitali ya Temeke jijini Dar es salaam
Ikiwa kama sehemu ya mradi wa “miaka 20 ya kujali jamii” benki ya Exim itatoa msaada wa vitanda 500 na magodoro yake kwa hospitali … katika mikoa ya Mbeya, Arusha, Morogoro, Tanga, Dodoma, Kigoma, Kilimanjaro, Shinyanga, Mtwara, Pemba na Unguja.

Benki ya Exim ilitambuliwa kama benki bora kwa huduma ya wateja binafsi mwaka huu na taasisi ya The Banker ya Afrika Mashariki na sasa inasheherekea miaka 20 ya mafanikio, ukuaji na kuwa kiongozi katika kuingia katika masoko mapya barani Afrika. Benki ya Exim ilianzishwa mwaka 1997 na imetanua soko lake kwa kufungua kampuni tanzu katika nchi za Comorro (2007), Djibouti (2010) na Uganda (2016). Benki hii inajivunia kuwa ya kwanza ya Kitanzania kuingia katika masoko ya nje ya nchi. Lengo muhimu kwa benki hiyo ni kutengeneza thamani ya uwekezaji kwa wanahisa wake na kufanikisha ukuaji kupitia utoaji wa huduma za tofauti na zinazomfaa mteja. 

Mkurugenzi wa Fedha wa Exim Benki Bw. Selemani Ponda (kushoto) akikabidhi misaada ya vitanda na magodoro kwa hospitali ya Temeke na (kulia) ni Kaimu Mganga Mkuu wa hospitali ya Temeke Bi. Husna Msangi akipokea misaada hiyo kwa niaba ya Mganga Mkuu wa hospitali hiyo.
Mwaka jana benki ya Exim ilipata faida kabla ya kodi ya kiasi cha shilingi 83.3 bilioni ikiiweka benki hiyo kwenye nafasi ya nne kwa mtaji nchini Tanzania. Katika kipindi cha miaka 19 ya kuwepo sokoni benki hiyo imejenga taasisi imara kijiografia, katika bidhaa za kivumbuzi, mahusiano mazuri na wateja na uwezo wake wa kutoa huduma kwa haraka zaidi. 

No comments: