Thursday, August 17, 2017

BENKI YA KCB TANZANIA YAZINDUA TAWI LA KCB SAHL BANK STONE TOWN, ZANZIBAR

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya KCB Tanzania, Cosmas Kimario akiongea na waandishi wa habari katika uzinduzi rasmi wa tawi la benki ya KCB Stone Town, Zanzibar kuwa benki ya Kiislamu. Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya KCB Group Bw. Ngeny Biwott, Mwenyekiti wa Bodi ya benki ya KCB Tanzania Bi. Zuhura Sinare Muro (wapili kulia) na Mkuu wa huduma za Kiislamu wa benki ya KCB Bw. Rashid Rashid (wakwanza kushoto). 
Mkuu wa Masoko na Mahusiano wa Benki ya KCB Tanzania, Bi. Christine Manyenye akifungua hafla ya uzinduzi wa KCB Sahl Bank katika tawi la Stone Town Zanzibar.


Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya KCB Tanzania, Cosmas Kimario akiongea katika hafla hiyo.

Mwenyekiti wa Bodi ya benki ya KCB Tanzania Bi. Zuhura Sinare Muro akiongea katika hafla hiyo.


Mkuu wa huduma za Kiislamu wa benki ya KCB Bw. Rashid Rashid akizungumza kuhusiana na huduma za kibenki za Kiislamu zitolewazo na benki hiyo

Mfaidika wa KCB 2jiajiri Bi. Abla Mohammed akielezea kuhusiana na faida alizopata kwenye biashara yake baada ya kupata mafunzo ya darasani yaliyotolewa na benki ya KCB kupitia program ya KCB 2jiajiri..

Mwenyekiti wa Bodi ya KCB Group Bw. Ngeny Biwott akiongea katika hafla hiyo.

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dr. Khalid Mohamed akizungumza na wageni waalikwa na waandishi wa habari kuhusiana na uzinduzi wa KCB Sahl Bank.

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dr. Khalid Mohamed akizindua rasmi Tawi la benki ya KCB Stone Town, Zanzibar kuwa benki ya Kiislamu “KCB Sahl Bank”. Pamoja nae kwenye picha ni Mwenyekiti wa bodi ya benki ya KCB Tanzania Zuhuru Sinare Muro, (wakwanza kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya KCB Group Bw. Ngeny Biwott (wapili kulia) na Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya KCB Tanzania, Cosmas Kimario (wakwanza kulia).

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dr. Khalid Mohamed akikata utepe kuzindua upya Tawi la benki ya KCB Zanzibar Stone Town kuwa benki ya Kiislam “KCB Sahl Bank”. Kwenye picha pamoja ni Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya KCB, Cosmas Kimario (wakwanza kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya KCB Group Bw. Ngeny Biwott na afisa mahusiano, Aziza Mkwizu, (kushoto).

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya KCB Tanzania, Cosmas Kimario akimuhudumia Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dr. Khalid Mohamed baada ya kufungua akaunti ya huduma za kiislamu.

Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhe. Dr. Khalid Salum Mohamed


 HABARI KAMILI IKO HAPA----

Benki ya KCB Tanzania imezindua upya tawi lake la Stone Town Zanzibar na kuwa KCB Sahl Bank, ikiwa inatoa huduma za kibenki za Kiislamu kwa wateja wake wote waliomo kisiwani humo.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Fedha na Mipango, Zanzibar Mhe. Dr. Khalid Salum Mohammed, Mwenyekiti wa Bodi ya KCB Group Ngeny Biwott, Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya KCB Bi. Zuhura Sinare Muro, wajumbe wa bodi ya benki ya KCB na wajumbe wa bodi ya shariah ya KCB.

Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya KCB Tanzania Cosmas Kimario alisema Benki ya KCB ni ya kwanza kutoa huduma za kibenki zifuatazo shariah ya Kiislam nchini Tanzania zikiwemo akaunti za kuweka amana na mikopo mbalimbali ya biashara/watu binafsi, watoto, wanafunzi n.k. Hii yote ni katika kuwahudumia wananchi wenye hitaji hilo.
Bw. Kimario alisema “Pamoja na kwamba huduma za kiislam zinapatikana katika matawi yote ya benki ya KCB, ili kujiimarisha zaidi tumeamua kubadilisha tawi letu la Stone town kutoa huduma za kibenki za kiislam tu, likiwa ni tawi la pili kwa benki yetu kutoa huduma hizi kipekee (exclusively), tawi la kwanza kufuata mfumo huu ni Lumumba lililoko Tanzania bara.
Mwenyekiti wa Bodi ya KCB Group Bw. Ngeny Biwott alisema kuwa mwezi wanne mwaka huu Benki ya KCB ilitunukiwa tuzo ya Benki Bora itowayo huduma za kibenki kupitia kitengo cha Kiislam ndani ya matawi yake yote. Tuzo hizo zilitolewa na “Al-huda Centre of Islamic Finance and Economic (CIBE)” ya dubai. “KCB tunahakikisha tunafuata kwa ufasaha kabisa shariah ya Kiislam katika utoaji wa huduma zetu” alisema Biwott.

“Benki ya KCB mbali na kufanya biashara imekuwa ikijihusisha katika miradi mbalimbali yenye manufaa kwa wazanzibari wahitaji” alisema Mwenyekiti wa Bodi ya benki ya KCB Bi. Zuhura Sinare Muro. Alizitaja baadhi ya michango iliyotolewa na benki hiyo ili kuinua hali ya maisha ya wananchi wenye shida kuwa ni; ujenzi wa kisima cha maji Mazizini Orphanage Centre, utoaji wa vyakula mbalimbali kwa Zanzibar Hayunani Association, vifaa vya kusomea na kuandikia katika shule ya Bwefum na vifaa tiba katika  hospitali za Kivunge Cottage, Mwembeladu na Kombeni. Kwa misaada hii yote Benki imetumia zaidi ya milioni 100.

Bi. Zuhura alieleza kuwa; benki ya KCB mwaka huu imetoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake wajasiriamali 32 wa Zanzibar kupitia mpango wa KCB 2jiajiri.  “Mpango wa KCB 2jiajiri unatoa fursa kwa wakinamama kufundishwa darasani kinadharia na baadae kivitendo katika ofisi zoa ambapo benki ya KCB inatuma maafisa wa aina tatu - masoko, sheria na fedha. Hili zoezi la mafunzo kwa vitendo linaendelea sasa hivi hapa visiwani” alisema Muro


Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Mhe. Dr. Khalid Salum Mohammed aliipongeza benki ya KCB kwa kufungua tawi maalum linalotoa huduma zinazofwata Shariah ya Kiislam kwa wateja wake Zanzibar. Pia aliipongeza benki ya KCB kwa kutoa misaada mbalimbali kwa kupitia sekta muhimu kama elimu, afya, mazingira, watoto yatima n.k

No comments: