Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) wamefanya ziara katika Wodi ya Wanawake, Hospitali ya Taifa Muhimbili kuadhimisha Siku ya Mwanamke wa Afrika pamoja na wanawake hospitalini hapo.
Wafanyakazi na uongozi wa LHRC waliadhimisha Siku ya Mwanamke wa Afrika ambayo huadhimishwa Julai 31 kwa kutimiza wajibu wa kijamii wa kuwatembelea wanawake hospitalini hapo na kuwafariji huku wakiwapa zawadi mbalimbali.
Akizungumza na vyombo vya habari hospitalini hapo, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, Bi. Anna Henga alisema “Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu kimeona ni vyema kuadhimisha Siku ya Mwanamke wa Afrika kwa kuzuru Hospitali ya Taifa ya Muhimbili ili kuonesha umuhimu wa sekta ya afya na kuikumbusha serikali na wadau wengine wa sekta hiyo umuhimu wa kufanya juhudi za makusudi katika kupambana na changamoto zinazoikabili sekta hiyo hapa nchini”.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Haki za Binadamu Tanzania, 2016 inayotolewa na Kituo hicho, sekta ya afya imekumbwa na changamoto kadha wa kadha ambazo zinahatarisha haki ya msingi ya wananchi kupata huduma bora za afya. Changamoto tajwa ni pamoja na upungufu mkubwa wa wafanyakazi katika sekta ya afya, takwimu zikionyesha upungufu wa asilimia 51; sambamba na vituo vya afya takribani 2000 kuwa na wafanyakazi wasio na sifa huku kukiwa na wahitimu takribani 20,000 wenye sifa ambao hawajapatiwa ajira. Pia, Ripoti hiyo; imebainisha uwepo wa changamoto ya upatikanaji wa dawa kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ufinyu wa bajeti iliyopangwa kwa ajili ya manunuzi ya dawa muhimu ambapo Bohari Kuu ya Dawa (MSD) ilikuwa na upungufu wa asilimia 47 ya dawa muhimu.
No comments:
Post a Comment