Tuesday, August 22, 2017

Meya Mwita ashauri Wananchi wenye kipato duni, mazingira magumu wapatiwe elimu kuhusu Bima ya Afya.


 NA CHRISTINA MWAGALA, OFISI YA MEYA WA JIJI

MSTAHIKI Meya wa jiji la Dar es Salaam Isaya Mwita amesema kuwa ipo haja ya kuangalia nijinsi gani watu wenye kipato duni na wale wanaoishi kwenye mazingira magumu wanaweza kufikiwa na kuelimishwa umuhimu wa kuwa na Bima ya Afya.

Meya Mwita amesema hayo jijini hapa leo wakati alipokuwa akifungua mkutano wasiku mbili wa wadau wa kujadili upatikanaji wa huduma za afya kwa makundi maalumu sambamba na ukiwa na lengo la kuboresha upatikanaji wa huduma hizo kwa watu wenye kipato cha chini.

Amefafanua kuwa watu wenye kipato cha chini ,makundi mbalimbali wanashindwa kuwa na huduma hiyo kutokana na kukosa uhamasishaji, elimu ya kutosha hivyo akashauri kuwa ni vyema jambo hilo likazingatiwa kwenye maeneo yote.

“ Tunapozungumzia huduma bora za afya kwa wakazi wa jiji letu,  tuliangalie pia eneo la gharama za utoaji  wa huduma, namna tunavyoweza kuihamasisha jamii kujiunga na bima ya afya ili kumsaidia na kumhakikishia mwananchi kupata  huduma hiyo pale anapozihitaji” amesema Meya Mwita.

Ameongeza kuwa kwakuwa jiji la Dar es Salaam linaongoza kuwa na idadi kubwa ya watu ni muhimu kuhakikisha nguvu kazi iliyopo jijini hapa ni ile watu wake wana afya njema.

Amesema jambo la msingi katika majadiliano ya mkutano huo, ni kuainisha hatua zinazo hitajika kuchukuliwa ili kuhakikisha wakazi wa jijini hapa ,hususani wale wenye kipato cha chini na waishio kwenye mazingira magumu wanafikiwa na kupata huduma bora za afya.

Hata hivyo alisema kulingana na takwimu za sense ya Taifa ya mwaka 2012, jiji la Dar es Salaam linakadiriwa kuwa na takribani watu milioni 4.4 hivyo kwa kuzingatia hilo ni muhimu kuwa na mipango madhubuti ambayo itawawezesha wakazi wake kupata huduma bora za kijamii, hususani za kiafya.

Jiji la Dar es Salaam limekuwa na ushirikiano na urafiki wa jiji la Hamburg kwa kipindi cha miaka 10, mkutano huo ni mwendelezo wa juhudi za wadau na Taasisi ndani ya majiji haya katika kuendeleza utamaduni wa undugu na urafiki uliopo.

Mkutano huo umehusisha , Tume ya Kikristu ya huduma za jamii (CSSC), marafiki kutoka Diakonie ya Hamburg  Ujerumani, Madiwani kutoka kata za Mtoni Mtongani, Ukonga, Buguruni na zinginezo.


No comments: