Monday, August 14, 2017

ZOEZI LA KUWAKAMATA WAPIGA DEBE LIMEANZA DAR ES SALAAM

Ule msako uliotangazwa na polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuwakamata wapigadebe kwenye vituo vya daladala jijini hapa unaanza leo.

Kaimu Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Lucas Mkondya alisema juzi kuwa, hatua hiyo imekuja baada ya kupokea malalamiko mengi ya wananchi kuporwa vitu vyao na baadhi ya wapigadebe hao.

Alisema mara nyingi wezi katika vituo vya daladala wamekuwa wakijifanya wapigadebe na kisha huwaibia abiria simu pamoja na fedha wanapokuwa wanagombea kupanda magari hasa nyakati za usiku.

“Kuanzia Jumatatu (leo) hatutaki kuwaona wapigadebe wakiita abiria kupanda gari na kondakta atakayehusika na watu hao, wote watakamatwa na kuchukuliwa hatua kali,” alisema Mkondya.

Hata hivyo, onyo hilo la polisi limewaibua baadhi ya wapigadebe ambao wamesema kuwa siyo wote vituoni wanaojihusisha na wizi na ukwapuaji wa mali za abiria.

“Kaka mimi nina familia yangu, mke na watoto na hii ni kama kazi nyingine. Nachofanya hapa ni kutafuta riziki tu, kama ningekuwa mwizi hapa nisingekuwapo maana huwezi kunyea kambi halafu ukarudi kulala hapohapo,” alisema Masoud Issa anayefanya kazi ya upiga debe kituo cha Tandika wilayani Temeke.

Jacob Joel maarufu kwa jina la Joe anayepiga debe Kituo cha Daladala cha Karume wilayani Ilala alisema kuwa wana utaratibu wa kuwafukuza wezi wanaokwenda kituoni hapo kwa kuwa hawataki kusikia vilio vya abiria.

Akizungumzia uamuzi wa jeshi hilo, Julius Nyakweele anayetumia usafiri wa daladala alisema wapigadebe wana faida na kasoro zao. “Kama mtu ni mgeni akisikia wanaita abiria inamrahisishia kujua gari analopanda, pia wapo wapigadebe wezi,” alisema.

No comments: