Mbunge wa jimbo la Ubungo kwa tiketi ya CHADEMA, Saed Kubenea ameshindwa kuhojiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge kufuatia hali yake kuwa mbaya na kulazwa katika Dispensary ya bunge mjini Dodoma.
Kubenea alikamatwa na polisi jijini Dar es Salaam jana na kupelekwa Dodoma kwa ajili ya kuhojiwa na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge lakini ameshindwa kuhojiwa kufuatia hali yake kiafya kutokuwa nzuri jambo lililopelekea kulazwa.
Mbunge wa Tarime Vijijini John Heche amethibitisha hilo na kulilaumu jeshi la polisi kumkamata Saed Kubenea akiwa hospitali ili tu aende kuhojiwa Dodoma.
"Baada ya Mhe. Kubenea kufikishwa Dodoma ameshindwa kuhojiwa kwasababu imethibitika anaumwa sana na sasa yuko Dispensary ya bunge amelazwa. Ni aibu kwasababu inatumika nguvu kubwa na gharama bila sababu ili tu kuwaumiza wabunge wa upinzani. Polisi wanamchukua mbunge kutoka hospital kisa wito wa kamati ambayo maamuzi yake ni mwezi wa kumi na moja, vitendo hivi vya kinyama tunavyofanyiwa hata serikali za wakoloni hawakuwafanyia watu weusi" alisema John Heche
Mbunge Saed Kubenea pamoja na Zitto Kabwe kwa amri ya Spika wa Bunge waliaambiwa wanapaswa kufika katika kamati mbili tofauti ili kuhojiwa kutokana na kauli zao mbalimbali ambazo walikuwa wamezitoa, Kubenea alipaswa kufika katika Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Bunge kwa kauli yake aliyotoa kuhusu sakata la Tundu Lissu huku Zitto Kabwe akitakiwa kufika kwenye Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge.
No comments:
Post a Comment