JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewatia mbaroni watu watano wanaodaiwa kuvamia, kuvunja na kuiba pesa kwenye ofisi za Prime Attorneys anazofanyia kazi wakili anayemtetea Yusuf Manji, Hudson Ndusyepo.
Akizungumza na wanahabari leo jijini Dar, Kamanda wa Polisi wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa amesema watuhumiwa wamekamatwa kufuatia oparesheni kali.
“Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar mnamo Septemba 12, 2017 lilipokea taarifa za kuvamiwa kwa ofisi za Prime Attorneys ambapo watuhumiwa walivunja na kuiba pesa taslim Tsh. Milioni 3.7, kompyuta, laptop mbili, nyaraka za ofisi na za wateja wao.
Baada ya msako huo watuhumiwa walikamatwa na walipohojiwa, wote wamekiri kuhusika na tukio hilo huku wakitaja matukio mengine waliyohusika kupora. Pia wameonyesha pesa walizopora kwenye tukio hilo.
Watuhumiwa hao ni; Said Idrisa Saleh (47), mkazi wa Mbezi Luis, Musatapha Ibrahim Said (35), mkazi wa Magomeni Mwembechai, Somfi Nguza Somfi (52), mkazi wa Magomeni Mapipa, Imani Mbago Mhina (36), mkazi wa Kimara Mwisho na Hussein Hajji Suleiman (45), mkazi wa Kigogo Mbuyuni.
Aidha, Kamanda Mambosasa amesema jeshi lake linaendelea na upelelezi kubaini watuhumiwa wengine waliohusika na tukio hilo.
Ofisi za kampuni hiyo zipo jengo la Prime House lililopo Mtaa wa Tambaza, Upanga jijini Dar es Salaam jirani na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani Ilala.
No comments:
Post a Comment