Saturday, September 2, 2017

LOWASSA KUMPIGIA KAMPENI UHURU KENYATTA

Waziri Mkuu wa zamani na mjumbe wa kamati kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Edward Lowassa amesema atarudi nchini Kenya kumpigia debe Rais wa nchi hiyo Uhuru Kenyatta katika kampeni za uchaguzi unaotarajiwa kurudiwa baada ya kufutwa na Mahakama.

Lowassa aliyekuwa mgombea wa urais nchini mwaka 2015 kupitia vyama vinavyounda Ukawa, August mwaka huu alikwenda nchini Kenya kushawishi raia wa nchi hiyo kumchagua Kenyatta kwa mara nyingine kuwa Rais wao katika uchaguzi uliofanyika August 8 mwaka huu.
Katika mahojiano na kituo cha Runinga cha Azam Lowassa amesema atafanya hivyo na ni kitu ambacho atakifurahia kukifanya.
Katika hatua nyingine Lowassa ameeleza sababu ya kumuunga mkono Kenyatta ingali yeye ni mpinzani nchini Tanzania.
“Kuwa upinzani ni barabara tu, nyenzo ya kufika sehemu fulani, nilipendezwa na Rais Kenyatta kwa anavyokubali mambo ya ushirikiano wa kimataifa, lakini la pili namuheshimu anavyoheshimu demokrasia na katika uongozi wake inalindwa, wabunge wana haki, vyama vina haki, kila mtu ana haki,” amesema Lowassa.
“La tatu uongozi wake ni wenye malengo, amerithi nchi imetoka katika migogoro ya kivita lakini kaingoza katika miaka mitano kimya wakijenga maendelea na wanatupita, kwa hiyo ni  Rais mwenye upeo, makini na mahiri ,” ameongeza.
Hiyo jana Mahakama ya Juu nchini Kenya ilifutilia mbali matokeo ya uchaguzi wa Urais uliofanyika Agosti 8 mwaka huu, ambapo Uhuru Kenyatta alitangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi huo, hivyo kurudiwa siku 60 zijazo.
Maamuzi hayo ya mahakama ni baada ya vyama vinavyounda umoja wa Upinzani (NASA), kupeleka malalamiko yao Mahakamani wakishutumu kudukuliwa kwa matokeo ya uchaguzi huo huku wakidai kuwa haukuwa wa huru na wa haki.

No comments: