Askari Polisi wawili wa kutoka kituo cha Oysterbay jijini Dar es Salaam na watu wengine sita, wamehukumiwa kwenda Jela miaka 35 na Mahakama Kuu Tanzania kwa makosa mawili ya kukutwa na nyara za serikali na kujihusisha na mtandao wa nyara za serikali
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Wakili wa Serikali, Salimu Msemo, aliwataja polisi hao wa zamani waliokutwa na hatia kutokana na makosa hayo kuwa ni wenye namba D 8656 CPL Senga Nyembo na G 553 PC Issa Mtama ambapo washtakiwa walikutwa na meno 70 ya tembo yenye thamani ya Sh. milioni 800.
Aidha, watu wengine sita waliokuwa nao na wote kukutwa na hatia ni Prosper Maleto, Seif Mdumuka, Amri Bakari, Said Mdumuka, Ramadhan Athuman na Musa Mohamed.
Msemo ambaye ni miongoni mwa mawakili maalumu wanaoshughulikia kesi za ujangili nchini, alisema washtakiwa hao walikutwa na kosa hilo katika eneo la kituo cha ukaguzi cha Kauzeni lililopo Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani kabla ya kufikishwa kortini na kukumbana na adhabu hiyo.
Akieleza zaidi, Wakili Msemo alisema kuwa katika kosa la kwanza, washtakiwa walihukumiwa kwenda jela miaka 20 kila mmoja na faini kwa kila mmoja, wakati katika kosa la pili, washtakiwa wawili ambao ni hao polisi, walihukumiwa miaka 15 kwenda jela.
Pia gari lililokuwa limebeba meno hayo ya tembo limetaifishwa na kusema maamuzi hayo yalitokana na kesi namba 203 ya mwaka 2016, yalitolewa na Mahakama Kuu Septemba 13, 2017, na Jaji Ama-Isaria Munisi kwa kusikiliza hoja za rufani zilizowasilishwa na washtakiwa wote nane, ikiwamo majibu ya hoja hizo ambayo yalitolewa na mawakili wa Serikali akiwamo yeye (Msemo) na Faraja Nchimbi.
Alisema hukumu hiyo inapaswa kuchukuliwa kuwa fundisho kwa watu wengine wenye kujihusisha na ujangili nchini, bila kujali hadhi na nafasi zao.
No comments:
Post a Comment