Lile tamasha kubwa na la aina yake la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo limewadia kwa msimu huu wa 36, ambapo litafanyika kuanzia 23-30 Septemba mwaka huu katika viwanja vya TaSUBa, Mjini Bagamoyo Mkoani Pwani.
Wakizungumza na waandishi wa Habari mapema leo Jijini Dar e Salaam, waandaaji hao wamebainisha kuwa maandalizi yote ya tamasha hilo kongwe Barani Afrika yameshakamilika na sasa ni kufanyika huku wakiwaomba wadau wa Sanaa na watu mbalimbali kujitokeza kulishuhudia tamasha hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari,Mtendaji Mkuu wa TaSUBa , Dk. Herbert Makoye amesema Tamasha hilo kwa mwaka huu ni la kipekee huku likiwa na kauli mbiu ya kupiga vita dhidi ya matumizi ya dawa za kulevya ambayo dunia inapambana na dawa hizo hatari kwa maisha ya watu hasa vijana wadogo.
“Sanaa na Utamaduni katika Kupiga Vita Madawa ya Kulevya” ikiwa ni mahsusi katika kuunga mkono mapambano ya vita dhidi ya usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya hapa nchini.
Tamasha la Kimataifa Sanaa na Utamaduni Bagamoyo hufanyika kila mwaka na huandaliwa na Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) ikiwa na malengo ya Kutunza na kuenzi sanaa na utamaduni wa Mtanzania, Kutengeneza jukwaa ambalo wanafunzi wa Tasuba wanalitumia kupima kiwango chao cha umahiri katika sanaa kwa mwaka katika fani za sanaa za maonyesho na zile za ufundi” ameeleza Dk. Herbert Makoye.
Dk. Makoye ameweka wazi kuwa, vikundi zaidi ya 60, vitapamba kwenye tamasha hilo la 36 na litapambwa na ngoma za asili, muziki, sarakasi na maigizo pamoja na maonyesho ya sanaa za ufundi huku pia kukiwa na warsha na semina zitakazohusu mambo mbalimbali ya kijamii.
Kati ya vikundi hivyo zaidi ya 60, vilivyothibitisha kushiriki, kati ya hivyo vikundi Saba ni kutoka nje ya nchi ikiwemo Kenya, Ufaransa, Korea Kusini, Uingereza, Zimbabwe na Mayyote.
“Katika ufunguzi wa tamasha letu mwaka huu, Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mh. Dk Harrison Mwakyembe (Mb) huku tukio la kufungwa likitarajiwa kufanyika na Naibu Spika Dk. Tulia Ackson.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa tamsha hilo, John Mponda amesema tamasha hilo limekuwa kongwe kutokanana malengo mbalimbali ikiwemo kukuza tamaduni za Watanzania wa maeneo yote.
“Tamasha hili utengeneza jukwaa moja lenye kujenga mahusiano mema ya wasanii wa ndani na nje ya nchi kupitia maonyesho hayo na pia kubadilishana uzoefu na mawazo katika kuendeleza tasnia ya sanaa. Kwa mwaka huu pia tumeweeza kutenga muda muafaka kwa shule mbalimbali kufika kushuhudia kwa muda wa kawaida yaani mchana.” Alieleza Mponda.
Aidha, Mponda alitaja viingilio kwenye tamsha hilo kuwa kwa Wanafunzi ama wanafunzi wa Vyuo watakaofika kuanzia 100, watalipia punguzo la Tsh 500, kwa kila mmoja huku kwa watoto wadogo ama wanafunzi kawaida kiigilio ni Tsh. 1000 na Kawaida kwa watu wote ni Tsh.3000 na kwa Raia wa Kigeni ni Tsh. 5,000.
Uongozi huo wa TaSUBa umewakaribisha watu wote huku tayari wakiwa wameshaweka sawa masuala ya Ulinzi na Usalama pamoja na Afya kwa watu wote wanaofika kwenye tamasha hilo.
Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Dk. Herbert Makoye akizungumza na waandishi wa habari wakati akitangaza tamasha hilo la kimataifa la 36, litakalofanyika mjini Bagamoyo, kushoto ni Mwenyekiti wa Tamasha hilo John Mponda. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari MAELEZO, Rodney Thadeus
Mwenyekiti wa Tamasha la Sanaa Bagamoyo, John Mponda akizungumza wanahabari wakati wa kutangaza kwa tamsha hilo litakaloanza keshokutwa Septemba 23. Kulia ni Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa), Dk. Herbert Makoye.
No comments:
Post a Comment