Friday, December 29, 2017

KESI YA MALINZI NA WENZAKE YAPIGWA KALENDA MWAKA MPYA KULA WAKIWA JELA

Kesi  ya  kutakatisha Dola za Marekani 375,418 inayomkabili aliyekuwa Rais wa shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Jamal Malinzi na wenzake, imepigwa kalenda hadi Januari 11, 2018 baada ya upande wa Jamhuri kudai bado haujakamilika.

Hata hivyo,  upande wa utetezi uliiomba  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  Dar es Salaam, kuuamuru upande wa mashtaka kuharakisha upelelezi wa kesi hiyo.

Kesi hiyo ilitajwa jana na  Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Leonard Swai, alidai kuwa  upelelezi bado haujakamilika, hivyo akaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Wakili wa utetezi, Nehemiah Nkoko, alidai kuwa kesi hiyo ni ya muda mrefu na kila siku wanaambiwa jalada bado lipo kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Hakimu Mashauri alisema mahakama hiyo inafanya kazi ya kutafsiri sheria na kama itafanya vinginevyo itakuwa nje ya sheria.

Alisema kesi hiyo itatajwa Januari 11, 2018 na washtakiwa wataendelea kukaa mahabusu.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu wa TFF, Mwesigwa Selestine na Mhasibu wa shirikisho hilo, Nsiande Mwanga ambao wanakabiliwa na mashtaka 28, ikiwamo ya utakatishaji fedha ambazo ni Dola za Marekani, 375,418.

No comments: