Saturday, December 16, 2017

MHE MWANJELWA AAGIZA BODI YA KAHAWA KUTOCHELEWESHA MALIPO KWA WAKULIMA

 Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akikaanga kahawa mara baada ya kutembelea Kitengo cha kukaanga Kahawa katika Ofisi za Bodi ya Kahawa akiwa ziarani Mkoani kilimanjaro, Jana 16 Disemba 2017. Picha Zote na Mathias Canal
 Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akikagua namna kahawa zinazohifadhiwa mara baada ya kutembelea Maabara ya kuandaa kahawa kwa ajili ya wanunuzi katika Ofisi za Bodi ya Kahawa akiwa ziarani Mkoani kilimanjaro, Jana 16 Disemba 2017
  Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akisikiliza maelezo kuhusu uendeshaji wa mnada wa kahawa kwa mfumo wa kisasa Kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Ndg Primus Kimaryo alipotembelea Ofisi za Bodi ya Kahawa akiwa ziarani Mkoani kilimanjaro, Jana 16 Disemba 2017
 Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akiwasili katika chuo cha mafunzo ya Kilimo Kilimajaro (KATC) wakati wa ziara ya kikazi Mkoani humo, Jana 16 Disemba 2017.
Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa akikagua miongoni mwa mashamba ya kufundishia kilimo cha mpunga mara baada ya kikao na watumishi wa chuo cha mafunzo ya Kilimo Kilimajaro (KATC) wakati wa ziara ya kikazi Mkoani humo, Jana 16 Disemba 2017

Na Mathias Canal, Kilimanjaro

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya serikali iliyopewa jukumu la Kusimamia sekta ya Kahawa nchini Ndg Primus Kimaryo ameagizwa kusimamia na kuwalipa haraka wakulima malipo mara baada ya kukusanya mazao yao kwani kufanya hivyo kutawezesha mazingira mazuri ya biashara na kuwanufaisha wakulima kutokana na kilimo hicho.

Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa ametoa agizo hilo jana Disemba 16, 2017 alipotembelea Ofisi za Bodi ya Kahawa akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Kilimanjaro.

Mhe Mwanjelwa alisema kuwa pamoja na wakulima kuuza kahawa kwa bei ya shilingi 5000 kwa kilo katika msimu wa mwaka 2016/2017 lakini bado changamoto ni kubwa ya ucheleweshaji wa malipo kwa wananchi jambo ambalo linarudisha nyuma ufanisi wa zao.

Alisema miongoni mwa kazi kubwa ya Bodi ya Kahawa nchini ni pamoja na kulinda maslahi ya wakulima dhidi ya makundi mbalimbali yanayofanya biashara ya zao la kahawa hivyo kucheleweshwa kulipwa malipo yao ni ishara ya Bodi hiyo kutotekeleza majukumu yake ipasavyo.

Aidha, Kaimu Mkurugenzi huyo wa Bodi ya Kahawa ametakiwa kuwa na mikakati imara na yenye tija itakayolifanya zao la kahawa kuwa na ubora zaidi Duniani kwa kwa kuliongezea thamani.

Katika ziara hiyo pia Naibu Waziri wa Wizara ya Kilimo Mhe Mary Mwanjelwa alitembelea chuo cha mafunzo ya Kilimo Cha Kilimajanro (KATC-Kilimanjaro Agricultural Training College) ambapo ameupongeza uongozi wa Chuo hicho kwa kuwawezesha zaidi ya wakulima 7000 katika skimu zaidi ya 100 kuboresha kilimo cha mpunga na mazao mengine hivyo kupata ongezeko kubwa la mazao.

Sambamba na pongezi hizo pia amewataka kuongeza ufanisi katika utendaji ili kuunga mkono kwa vitendo serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kwa kufanya kazi kwa bidii, ufanisi, na ubunifu.

Aliwasisitiza wananchi hao kutofanya kazi kwa mazoea badala yake kuwa wabunifu katika kazi ikiwa ni pamoja na kuzikabili changamoto na kuzigeuza kuwa fursa.

No comments: