Sunday, December 17, 2017

SEMINA YA KUWAJENGEA UWEZO MAIMAMU NCHINI YAFUNGULIWA LEO NA MUFTI ZUBERI

Maimamu kote nchini wametakiwa kuondoa fikra za kuwa msikitini ni sehemu ya kuswali peke yake bali ni sehemu muhimu ya kuwajenga waumini na wasio waumini kiakili na kiuchumi.
Mufti mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakary Zuberi akiongea na Maimamu kutoka misikiti mbalimbali hapa nchini mapema leo jijini Dar es salaam.

Hayo yamesemwa na Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakary Zuber alipokuwa akifungua semina elekezi kwa Maimamu wa misikiti mbalimbali ya hapa nchini, mapema leo katika hotel ya Urban Rose jijini Dar es salaam.

Mufti Zubery alisema lengo la Semina hiyo ni kuwajengea uwezo Maimamu ambao ni viongozi wakuu wa Msikiti ili wajue namna ya kuiongoza misikiti yao kwa kufuata sheria na taratibu za dini ya kiislamu.
Masheikh kutoka katika misikiti mbalimbali hapa Tanzania wakifuatilia kwa umakini semina ya kuwajengea uwezo Maimamu wa misikiti ili waweze kuiongoza vizuri misikiti yao.
Aliendelea kusema kuwa Masheikh wanatakiwa kuwajenga vizuri waumini wao kiimani na kiuchumi ili msikiti uweze kujitegemea wenyewe kwa kuwa na uchumi wake mzuri, lakini pia mtu mmoja mmoja ili waweze kujiongoza katika kujitafutia riziki zao.

Aidha Mufti aliendelea kusema kuwa utaratibu huu umeanza kwa Maimamu wa misikiti ambao ni watu wanaoifikia jamii moja kwa moja lakini utaendelea kwa ngazi ya Kata, Wilaya Mkoa na hatimaye Taifa.
Mufti Mkuu wa Tanzania Sheikh Abubakary bin Zubery katikati akiwa katika semina ya kuwajengea uwezo Maimamu wa ndani ya nchi, ili waweze kuiongoza misikiti yao vyema na kushoto kwake ni Sheikh Mkuu wa Shia Ithnasheria Maulana Hemed Jalala na kulia kwake ni Sheikh wa wilaya ya Ilala Adamu Mwinyipingu akimkaimu Sheikh mkuu wa mkoa.
Akiongezea sheikh mkuu wa dhehebu la Shia Ithanasheria Maulana Hemed Jalala alisema kuwa mkutano huo ni muhimu kutokana kuwa umelenga mambo makubwa mawili kwanza ni Maimamu lakini pia vijana.

Sheikh Jalala aliendelea kusema kuwa kwa imani yake Maimamu hao wataweza kufanya kazi kwa pamoja kwa kushirikiana na vijana ,ili kuweza kuwakomboa katika dimbwi la mawazo mabaya kama ugaidi, wizi na mambo mengine yanayoleta chuki kati yao na kuwa Wazalendo kwa nchi yao.

“Kwa kuwa viongozi wa dini watu ambao wapo karibu sana na jamii na ni watu wenye wafuasi wengi zaidi hivyo wataweza kuboresha kazi zao na wataweza kuleta mabadiliko makubwa sana kupitia semina watakayopewa leo” alisema Sheikh Jalala


      ANGALIA HAPA KUIPATA HOTUBA YOTE YA MUFTI NA MAULANA JALALA

                   

No comments: