Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) Ndg Andrew W. Massawe ameitaja mikoa
ya Mara, Arusha, Iringa, Geita,
Lindi, Simiyu, Mbeya na Songwe
kuwa mikoa inayoongoza katika zoezi la kuwasajili wananchi kupata Vitambulisho
vya Taifa; huku mikoa mingine ikiwa nyuma kiusajili kulinganisha na malengo
waliyowekewa.
Akizungumza katika sherehe za uzinduzi wa zoezi la usajili kwa mkoa wa Ruvuma lilofanyika katika viwanja vya Lisaboni-Songea, Ndugu Massawe amemuomba Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Mwigulu Nchemba kusaidia kuweka msukumo kwa viongozi na wananchi kwenye mikoa ambayo haifanyi vizuri ili iongeze kasi ya usajili kwa lengo la kukamilisha usajili kwenye mikoa yao kwa muda uliopangwa.
Akihutubia wananchi wa
Ruvuma waliofurika kwenye viwanja vya Lisaboni vilivyopo nje kidogo ya mji wa
Songea, Waziri wa Mambo wa Ndani ya Nchi Mhe.Dkt Mwigulu Lameck Nchemba
amewasisitizia wananchi kujitokeza kwa wingi kusajiliwa kwani kuwa na
kitambulisho cha Taifa siyo suala la hiyari ni wajibu kwa kila Mtanzania mwenye
sifa kuwa nacho.
“ Mhe. Rais wetu ametoa
hela za kuwasajili, zoezi ni bure bado kujisajiliwa kwenda kupigwa picha na
kuchuliwa alama za vidole ikushinde?” aliuliza Waziri huyo mwenye dhamana kubwa
katika kusimamia utekelezaji wa zoezi hilo.
Aidha amewataka viongozi wa
Mikoa na wote wenye dhamana katika kusimamia zoezi hili kuhakikisha
wanashirikiana kwa karibu na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa katika kuhakikisha
wananchi wenye sifa wanasajiliwa na kamwe pasiwepo wageni watakaojipenyeza
kusajiliwa Vitambulisho vya Taifa kama raia.
“Kwakuwa NIDA inatoa
vitambulisho vya aina tatu, cha Raia, Mgeni na Mkimbizi basi niwaombe wageni
badala ya kufanya udanganyifu wajisajili kwa hadhi yao kwani siyo dhamira ya
Serikali kumfukuza yeyote lakini kuwatambua Raia wake kama ilivyo kwa nchi
nyingine duniani” alisema
Naye Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma
Mhe. Christina Mndeme amemhakikishia Mhe. Waziri mkoa wake uko tayari kusimamia
na kuhakikisha wananchi wote wenye sifa wanasajiliwa na kupata Vitambulisho
ndani ya muda uliopangwa na kwamba kamwe hata mvumilia mtu yeyote ambaye
atakuwa kikwazo katika utekelezaji wa zoezi hilo kwa wananchi; akiwakemea
wanasiasa kuingiza siasa kwenye zoezi la Usajili wananchi vitambulisho vya
Taifa.
Mkoa wa Ruvuma wenye Wilaya
5 unakisiwa utawasajili zaidi ya wananchi 900,000 katika zoezi lililopangwa
kumalizika ndani ya miezi mitatu. Tayari NIDA imekamilisha usambazaji wa vifaa
na kutoa mafunzo kwa maafisa ambao watatumika kuwasajili wananchi wa Ruvuma na
viunga vyake.
kikundi cha burudani za
asili maarufu kama wana Lizombe wakitumbuiza wakati wa sherehe za uzinduzi wa
zoezi la Usajili kwa mkoa wa Ruvuma.
|
Mikoa mingine inayoendelea
na Usajili kwa sasa ni Iringa, Mbeya,
Njombe, Singida, Manyara, Arusha,
Kilimanjaro, Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara, Songwe, Lindi na Mtwara.
No comments:
Post a Comment