Wednesday, December 13, 2017

WAZIRI WA NISHATI AWAPA SIKU TATU TANESCO KANDA YA KUSINI KUREKEBISHA MIUNDOMBINU

Waziri wa nishati Dk Medard Kalemani  akizungumza na Kaimu mkurugenzi wa TPDC,mhandisi Kapuulya Musomba,mwenye nyeusi.Kushoto ni Kaimu mkuu wa mkoa ambaye ni mkuu wa wilaya ya Mtwara Evod Mmanda
Kutokana na baadhi ya maeneo ya mkoa wa Lindi na Mtwara kukosa umeme wa uhakika waziri wa Nishati Dk Medard Kalemani ametoa siku tatu kwa viongozi wa Tanesco kanda ya kusini kuhakikisha wanarekebisha miundombinu ya umeme zikiwemo nyaya na nguzo.

Dk Kalemani ametoa maagizo hayo leo katika ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

Amesema pamoja na mitambo ya kufua umeme katika kituo cha Mtwara kuwa mibovu lakini matatizo mengine yanasababishwa na baadhi ya watendaji ambao hawatembelei wananchi kutoa elimu pamoja na kukagua miundombinu ambayo inakuwa imeharibika na kuleta athari .

"Nikimkuta mtaalamu wa Tanesco amekaa ofisini sitamuelewa,nendeni kwa wananchi,nikikuta mtaalamu wa Tanesco anakula kitumbua sitamwelewa labda akiniambia ni muhasibu nitaelewa lakini kama ni fundi sitaelewa hata mimi kama mnanifuatilia sikai ofisini hatuwezi kusubiri nguzo mpaka ianguke mwananchi alalamike ,'amesema Kalemani na kutaka ufanyike ukaguzi wa miundombinu kila mwezi.
Waziri wa nishati dkt Medard Kalemani akizungumza na wananchi katika kijiji cha Milamba Mtwara vijijini wakati wa ziara.
Wakati huo huo amewataka wakandarasi  wa REA  kuhakikisha wanapotia vijiji vyote bila pindi wanapofanya utafito badala ya kuruka ruka.

Waziri Kalemani amedai baadhi ya wakandarasi wanapofanya utafiti wanaruka vijiji bila sababu za msingi. 

"Natoa agizo kwa wakandarasi hakuna kuruka kijiji sijui nyumba hii imelegea,nyumba hii ni ya nyasi au tope hii haikuhusu mwananchi anataka umeme ndani ya nyumba yake na haya ni maelekezo ya nchini nzima,"amesema Dk Kalemani

Awali akizungumza meneja wa Tanesco mkoa wa Mtwara,Mhandisi Jafari Mpina amesema mahitaji ya mkoa wa Lindi na Mtwara ni megawati 16 na kwamba mahitaji ya mkoa wa Mtwara ni megawati 11.

Ameongeza kwamba katika kituo cha kufua umeme Mtwara kina mashine tisa na na mashine zinazofanya kazi kwa sasa ni nane ambazo zina uwezo wa kuzalisha megawati 15.8.

Pamoja na hayo amesema shirika hilo tayari lilishapokea vipuli kwa ajili ya ukarabati wa mitambo lakini takini tayari wana mpango wa kununua mashine mpya sita na mashine mbili zitaanza kazi Februari mwakani.

Katika mradi wa REA mkoani Mtwaa vijiji 393 watanufaika nao ambapo mradi wa kwanza vijiji 167 vitaunganishwa na vijiji 226 vitaunganishwa katika awamu ya pili.
Waziri wa nishati Dk Medard Kalemani  akizungumza na menaja wa kituo cha kufua umeme Mtwara mhandishi Mkulungwa Chinumba,wa pili kushoto

No comments: