Monday, January 22, 2018

MGOMBEA UBUNGE WA JIMBO LA KINONDONI KWA TIKETI YA CCM AKUMBANA NA CHANGAMOTO HIZI KUBWA.

Wakati kampeni za uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo ya Kinondoni na Siha, zikianza kwa vitimbi, mgombea wa CCM, Maulid Mtulia amewekewa pingamizi lenye vipengele vitano.

Uchaguzi huo utakaoshirikisha vyama 12, utafanyika Februari 17 huku ukitarajiwa kuwa na mpambano mkali baina ya CCM na Chadema inayoungwa mkono na vyama vitano vya Ukawa ambavyo NLD, NCCR-Mageuzi, CUF ya upande wa Maalim Seif Sharif Hamad na Chaumma iliyojiunga hivi karibuni.

Uchaguzi huo unafanyika baada ya waliokuwa wabunge, Godwin Mollel (Siha, Chadema) na Maulid Mtulia (Kinondoni, CUF) kujivua uanachama kwa maelezo kuwa wanamuunga mkono Rais John Magufuli na baadaye kujiunga na CCM.

Chama hicho tawala kimewapitisha wawili hao kutetea majimbo hayo bila ya kuendesha mchakato wa ndani.

Kwa staili kama hiyo, Chadema imemsimamisha Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu katika jimbo la Kinondoni na Elvis Mosi (Siha).

Tayari CCM katika jimbo la Siha na CUF upande wa mwenyekiti anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Profesa Ibrahim Lipumba wamezindua kampeni jana.

Wagombea walirejesha fomu juzi katika ofisi ya jimbo la iliyopo Magomeni.

Lakini saa chache kabla ya kuanza kampeni, Mwalimu aliwasilisha pingamizi dhidi ya mgombea wa CCM, akiwa na hoja tano, ikiwemo ya kutofanya mrejesho wa gharama za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Wakili wake, Frederick  Kihwelo amesema  kuwa kwanza, Mtulia  hajafanya mrejesho wa gharama za uchaguzi wa mwaka 2015, alipogombea kwa tiketi ya CUF.

“Jambo hili hufanywa na mtu yeyote aliyegombea nafasi ya udiwani, ubunge na urais na haijalishi kama alishinda au kushindwa,” alisema Kihwelo.

“Unapaswa kuandaa mchanganuo wa gharama zako za uchaguzi na kuzipeleka ofisi ya NEC.”

Alisema hoja ya pili ni Mtulia kushindwa kukidhi matakwa ya kisheria kwa kutojaza kwa usahihi fomu zake, kwa madai kuwa zimepigwa muhuri wa katibu wa CCM badala ya muhuri wa chama hicho tawala.

“Muhuli ulipigwa katika fomu yake unasomeka wa katibu wa chama badala ya muhuri wa chama. Hii inaonyesha chama hakijamthibitisha kugombea. Jambo hili liliwasumbua sana Chadema mwaka 2014 kwa baadhi ya wagombea wao kuenguliwa, ” alisema Kihwelo.

Alisema hoja ya mwisho ni Mtulia kujaza fomu akieleza kuwa anajishughulisha na kilimo cha mbogamboga, jambo ambalo Kihwelo amesema si kweli.

“Hiki kilimo cha mbogamboga amekianza lini kwa sababu tunajua alikuwa mbunge. Tunamtaka athibitishe hili,” alisema.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Kinondoni, Latifa Almasi alisema wamepokea mapingamizi lakini haweka wazi idadi yake, na kubainisha kuwa leo msimamizi mkuu wa uchaguzi huo, Aron Kagurumjuli, atayatolea ufafanuzi

No comments: