Tuesday, February 6, 2018

TAMKO SIKU YA KIMATAIFA YA KUPINGA UKEKETAJI - FEBRUARI 6, 2018



MAADHIMISHO YA SIKU YA KIMATAIFA YA KUPINGA UKEKETAJI
FEBRUARI 6, 2018

Tarehe 6 Februari kila mwaka ni siku ya kimataifa ya kupinga Ukeketaji duniani kote. Historia ya siku hii ilianza mwaka 2003 ambapo Baraza la Umoja wa Mataifa liliidhinisha kuwa siku rasmi ya kimataifa ya kupinga Ukeketaji duniani kote. Baraza la Umoja wa Mataifa lilifikia uamuzi huu baada ya kutathimini na kuona athari kubwa zitokanazo na vitendo vya ukeketaji kwa mtoto wa kike.
Kauli mbiu ya mwaka huu ni:

Pinga Ukeketaji, kwa Maendeleo ya Mwanamke na Mtoto wa Kike!

Ukeketaji ni nini?
Ukeketaji ni kitendo cha kukata, kuvuta ama kuharibu kwa namna yoyote ile kiungo cha ndani au cha nje cha uke wa mtoto wa kike. Tendo hili hufanywa pasipokuwa na sababu zozote za kisayansi/kiafya. Ni kitendo kinachomdhalilisha mtoto wa kike na kumwondolea utu wake kama mwanandamu aliyeumbwa kamili. Historia ya utekelezaji wa mila hii potofu inasadikika kuanza yapata miaka 2000 iliyopita. Ukeketaji mara zote hufanyika kwa sababu ya misukumo ya kibinadamu, ikiwemo kupata mali kwa kumwozesha binti aliyekeketwa, kutii masharti ya mila kama ya kutambika mizimu, kuondoa mikosi katika familia, kumvusha mtoto rika na nyinginezo nyingi. Hata hivyo sababu hizo zote hazina maana zaidi ya kuendeleza tamaduni kandamizi kwa wanawake na watoto wa kike.

Madhara ya Ukeketaji
 Yapo madhara mengi yanayosababishwa na ukeketaji; madhara hayo yanaweza kuwa ya kiafya au hata kisaikolojia. Madhara yanayosababishwa na ukeketaji yanaweza kuwa ya papo kwa papo kama maumivu makali wakati wa ukeketaji, mshtuko, homa kali, kumwaga damu nyingi na mara nyingine hata kupelekea kifo, kuambukizwa magonjwa kama Virusi Vya UKIMWI na msongo wa mawazo. Yapo pia madhara ya muda mrefu kama vile; kuathirika kisaikolojia, ulemavu/kovu la kudumu katika uke, fistula, kupata shida wakati wa kujifungua na muda mwingine kupelekea kupata ugumba.

Jitihada za wadau
Pamoja na jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali, Mashirika na Taasisi mbalimbali bado ukeketaji umeendelea kutekelezwa katika baadhi ya jamii. Kwa mujibu wa Takwimu za Taarifa ya Demographia na Afya ya 2012 zinaonyesha kuwa pamoja na jitihada za kutokomeza vitendo hivyo, bado kuna mikoa mitano inayoongoza kwa ukeketaji nchini ikiongozwa na Manyara wenye asilimia (58) ukifuatiwa na Dodoma (47), Arusha (41), Mara (32) na Singida yenye asilimia (31). Ziko sababu nyingi zinazosababisha, kuendelea kwa ukeketaji moja kati ya hizo ni usiri mkubwa uliopo katika jamii husika. Jamii kwa kuamini kuwa kukeketa ni mila na desturi zao, wameendelea kuhifadhi na kutunza siri za wale wanaoendeleza vitendo hivyo, ili kuwaepusha wahusika na mkono wa dola. Hali hii hupelekea watoto wa kike na wanawake kuendelea kunyanyasika bila msaada

Mtandao wa mashirika yanayopinga ukeketaji hapa nchini umeendelea kusimama imara katika kuhahikisha kuwa ukeketaji unakoma ifikapo 2030 ili kuendana na mikakati ya maendeleo endelevu ya kidunia ya kuondoa aina zote za ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake na watoto na vilevile kuendana na mikakati ya kitaifa kama ilivyoainishwa katika mpango kazi wa kitaifa wa kupinga vitendo vyote vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto. Zipo juhudi kubwa zimefanyika katika wilaya mbalimbali nchini ikiwemo miradi ya kutoa elimu na kusaidia watoto wa kike kukabiliana na mila ya ukeketaji katika mikoa iliyotajwa. Kazi ambazo zimekuwa zikifanywa na wanamtandao ni pamoja na Mafunzo kwa wazee wa mila, ngariba, jeshi la polisi, mhimili wa mahakama, walimu, watoto, wazazi na jamii kwa ujumla ambayo yameleta chachu katika kukuza na kuimarisha uelewa wa kila mtu katika mapambano dhidi ya ukeketaji kwa  watoto wa kike na wanawake..

Sambamba na hilo mtandao unafanya kazi kuwezesha wahanga wa ukeketaji kufikia vyombo vya kisheria ikiwemo polisi na mahakama ili kuwachukulia hatua wale wote wanaendeleza mila hii kandamizi.
Serikali imeendelea kuboresha sheria na sera mbalimbali ili kupanua wigo wa adhabu kwa wale wanaoendelea kutekeleza kitendo hicho cha kikatili. Kwa mfano mabadiliko ya Sheria ya Mtoto (2009) yamelenga pamoja na mambo mengine kupanua adhabu na kutengeneza mnyororo mpana wa washiriki. Maboresho ya Sheria ya Kanuni ya Adhabu (2002) nayo yamepanua uwanda wa kutoa adhabu na kubaini kipimo cha ushiriki wa mtuhumiwa katika kufanya ukeketaji.
Sera mbalimbali za kitaifa ikiwemo Sera ya Elimu ya 2015 inapinga kila aina ya unyanyasaji kwa mtoto wa kike na inaweka na kutambua misingi ya haki na usawa kwa watoto wote wa kike na wa kiume. Sera hii pia imelenga kuondoa ubaguzi na unyanyasaji kwa mtoto wa kike.
Serikali ya Jamhuri ya Mungano pia imeendelea kuridhia na kutekeleza sera na sheria mbalimbali za kimataifa zinazolenga kutokomeza ukeketaji na unyanyasaji kwa mtoto wa kike. Tanzania imeridhia mkataba wa kimataifa wa Kupinga aina zote za Ukatili kwa wanawake CEDAW wa mwaka 1979 na mikataba mingine mingi. Kuendelea kutumika kwa sheria hizi za kimataifa na kikanda kumezidi kutanua wigo wa sheria na uwajibikaji wa kitaasisi katika kulinda masilahi ya mtoto wa kike dhidi ya ukeketaji.
Wadau wengine kama Jeshi la Polisi, Mahakama, taasisi za kidini na viongozi wa kimila wameonyesha nia na jitihada kubwa katika kuunga mkono kampeni za kutokomeza ukeketaji nchini.
Nini kifanyike ili kutokomeza kabisa ukeketaji?
Mbali na jitihada kubwa zinazochukuliwa na wadau kutokomeza ukeketaji nchini, bado kuna mambo kadhaa ya kufanya ili kuondosha kabisa mila hii potofu katika jamii zetu.
1.      Serikali kusimamia kikamilifu sheria kuhakikisha watekelezaji wa vitendo vya ukeketaji wanakamatwa na kuwajibishwa kwa mujibu wa sheria za nchi. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania idumishe ushirikiano na taasisi zisizo za kiserikali pamoja na mashirika rafiki ya kimataifa ili kwa pamoja tuweze kutokomeza ukeketaji na ukandamizaji kwa mtoto wa kike na wanawake.
2.      Jamii inapaswa kuungana na kukemea kwa nguvu vitendo vya ukeketaji na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ikiwemo kutoa taarifa na ushahidi ili kufanikisha vita dhidi ya ukeketaji na ukatili wa kijinsia kwa ujumla.
3.      Wadau waongeze juhudi katika kuzifikia jamii zinazotekeleza mila ya ukeketaji kwa elimu na kwa msaada wa moja kwa moja ili kutokomeza janga hili.

Imetolewa na Mtandao wa Kupinga Ukeketaji Tanzania
Mtando wa mashirika yanayopinga ukeketaji Tanzania unaundwa na mashirka yafuatayo:
1.      Children Dignity Forum (CDF)
2.      Tanzania Media Women’s Association (TAMWA)
3.      Tanzania Women’s Lawyers Association (TAWLA)
4.      Legal and Human Rights Center (LHRC)
5.      Christian Council of Tanzania (CCT)
6.      World Vision Tanzania (WVT)
7.      Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA)
8.      Network Against Female Genital Mutilation (NAFGEM)
9.      Women Wake Up (WOWAP)
10.  Anti-Female Genital Mutilation Network (AFNET)
11.  Dodoma Inter - African Committee (DIAC



No comments: