Thursday, March 15, 2018

NGUZO MAMA YAENDELEA KUWA GUMZO TOKA MIAKA MINGI ILIYOPITA MPAKA LEO HII

Wanawake kote nchini wametakiwa kuwa na umoja, ushirikiano na moyo wa kujituma ili kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakabili katika kufikia mafanikio yao.
Igizo la Nguzo Mama likichezwa jukwaani ili kuwapa wageni waalikwa ujumbe unaopatikana katika igizo hilo.

Hayo yamesemwa mapema jana jijini Dar es salaam na Muadhiri wa muda mrefu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam(UDSM) Mama Penina Mlama ambaye pia ni mtunzi wa maigizo na sanaa za jukwaani alipokuwa akielezea changamoto mbalimbali alizopitia mpaka kufikia kutunga igizo la “Nguzo Mama”.

Katika shughuli hiyo iliyoandaliwa na TGNP Mtandao iliyopewa jina la burudani elimishi ya Nguzo Mama iliudhuliwa na wadau kutoka taasisi mbalimbali binafsi vikundi na wanafunzi kutoka shule na vyuo mbalimbali vya jiji la Dar es salaam.

Na lengo kuu la Burudani elimishi hii ya Nguzo Mama ni kuwajengea uwezo watoto wa kike na wanawake kwa ujumla kuweza kujisimamia wenyewe na kupambana kwa hali na mali katika kupata haki zao.

Akiongea katika semina hiyo Profesa. Penina alisema kuwa yeye alitunga maigizo mengi na moja wapo kati ya yale yaliyompatia umaarufu ni Nguzo Mama, kwani hadithi hii ilikuwa na lengo la kuwahimiza wanawake kuwa na umoja wenye nguvu ili kuweza kujikomboa katika vitendo vya ukatili wa kijinsia vinavyoendelea kutekelezwa na baadhi ya watu katika jamii zetu.

Aidha Profesa Penina aliendelea kusema kuwa hadithi hii aliiandika miaka 36 iliyopita lakini anashangaa kuona bado vitendo vya aina hii bado vipo katika jamii zetu mpaka leo.

“Igizo hili nililitunga miaka mingi iliyopita na mpaka sasa huu ni mwaka wa 36 tangu nimelitunga lakini nashangaa kuona vitendo vya miaka 36 nyuma ambavyo tulivipinga kwa nguvu zetu zote bado vinaendela mpaka leo vya wanawake kunyanyaswa na wanaume zao lakini pia kuonewa baada ya waume zao kufariki dunia” alisema Penina Mlama

Aliendelea kusema kuwa yeye ni miongoni mwa wanawake waliopitia changamoto nyingi na kuamua kupigania haki za wanawake kwa miaka mingi ambapo wanawake walikuwa wakidharaulika sana na mchango wao ulikuwa hauonekani katika jamii yao.

“Kipindi hicho mimi nikiwa  mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam tulikuwa tunatumia vyoo kwa pamoja kati ya wanawake na wanaume na mimi niliona hii siyo sawa, hivyo nilishawishi wenzangu kuleta mgomo kwa kuwa wanawake na wanaume tunatofautiana mahitaji na mkuu wa chuo aliamua kugawa vyoo kuwa hiki cha wanawake na hiki kitakuwa cha wanaume” aliendelea kusema Menina

Profesa Penina aliendelea kusema kuwa yeye pia ni miongoni mwa watu walioleta mabadiliko katika chuo kikuu cha Dar es salaam kwa kuleta usawa wa kijinsia kati ya wanawake na wanaume, na hata katika kuhakikisha wanawake wanapata mahitaji yao muhimu ikiwa ni kutenga vyoo vya walimu wanawake na wanaume ni miongoni mwa mafanikio aliyoyaleta yeye.

Na mwisho alisema kuwa ni vema kuongea na vijana hasa watoto wa kike ili waweze kusimama na kupigania haki zao wenyewe bila kushikwa mkono ama kusaidiwa na watu wengine, hii ikiwa ni kuwajengea uwezo vijana wetu wawe na uwezo wa kujieleza na kupigania haki zao wenyewe.

Igizo la Nguzo Mama likiendelea jukwaani.

Mwanafunzi wa Chuo cha Usafirishaji(NIT) Sei Charles akielezea namna gani alivyolielewa Igizo hilo la Nguzo Mama lililofanyika mapema jana Makao makuu ya TGNP Mtandao Mabibo jijini Dar es salaam.

Mwanachama wa Semina za Jinsia na Maendeleo(GDSS) Bi. Neema Mwinyi akitoa ufafanuzi wa kile alichojifunza kupitia igizo la Nguzo Mama.

Profesa Manina Mlama akitoa ufafanuzi wa jambo fulani kuhusiana na Igizo la Nguzo Mama ambalo alilitunga kwa miaka mingi iliyopita, na kwa namna gani hilo igizo limeweza kufanya vizuri ndani na nje ya nchi ya Tanzania.

Profesa Menina Mlama akiendelea kuongea na hadhara iliyofika katika Tamasha dogo la burudani elimishi ya Igizo la Nguzo Mama.

Washiriki wa Burudani Elimishi ya igizo la Nguzo Mama wakifuatilia kwa umakini matukio yaliyokuwa yakiendelea.

No comments: