Sunday, March 18, 2018

MKOA WA PWANI WAPOKEA MBEGU BORA ZA MAHINDI WEMA 2109

 Ofisa mradi wa Mbegu za Mahindi yanayostahimili  Ukame ya Wema 2109  kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa na Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Bestina Daniel, akizungumza wakati wa uzinduzi wa shamba darasa la mbegu hiyo katika Kijiji cha Kilemela kilichopo Kata ya Kerege wilayani Bagamoyo jana. W a pili kutoka kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga na hao wengine ni viongozi mbalimbali katika wilaya hiyo.
 Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Pwani, Kapilima George akizungumza.
 Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, akitoa hutuba yake.
 Mkurugenzi wa Fedha wa Fedha na Utawala wa COSTECH,Shabani Hussein (kulia), akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga  mbegu hizo kabla ya kuzindua shamba darasa. Katika ni Ofisa mradi wa Mbegu za Mahindi yanayostahimili  Ukame ya Wema 2109  kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa na Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB), Bestina Daniel.
 Mwakilishi wa Kikundi cha Kikuki Malengo Group kutoka Kitongoji cha Amani, Othman Said Ally akikabidhiwa mbegu. Wa pili kulia ni Mtafiti  Kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga mkoani Morogoro, Nikidadi Hamidu.
 Mkulima Julius Maina (kushoto), kutoka Kitongoji cha Zinga akikabidhiwa mbegu.
 Mkulima Anaseli Macha kutoka Kijiji cha Kongo Kaya ya Yombo akikabidhiwa mbegu.
 Mkulima Ahazi Mwasibata akikabidhiwa mbegu.
 Hapa wakielekezwa namna ya upandaji wa mbegu hiyo.
  Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Majid Mwanga, akizundua shamba darasa hilo kwa kupanda mbegu.
 Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Pwani, Kapilima George na Ofisa Kilimo Ushirika na Umwagiliaji wa Wilaya ya Bagamoyo, Mary Kisimbo wakipanda mbegu hiyo.
Mbegu hiyo ikipangwa katika shamba darasa eneo la Zinga.

Na Dotto Mwaibale, Bagamoyo

MKOA wa Pwani umepokea mbegu bora ya mahindi aina ya Wema kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kupitia Jukwaa na Bioteknolojia kwa Maendeleo ya Kilimo (OFAB) kwa ajili ya kupandwa kwenye mashamba darasa mkoani humo.

Akizungumza wakati akipokea mbegu hiyo wakati wa uzinduzi wa shamba darasa uliofanyika jana katika Kijiji cha Kilemela Kata ya Kerege wilayani Bagamoyo Mkuu wa wilaya hiyo Majid Mwanga alisema mbegu hiyo itasaidia kuondoa changamoto ya kupata mbegu bora kwa wakulima wilayani mwake.

"Niwashukuru wenzetu wa COSTECH na OFAB kwa kutukumbuka kwa kuendesha program hii ya kugawa mbegu bora ya mahindi katika mkoa wetu hususan kwenye wilaya yangu ya Bagamoyo" alisema Mwanga.

Alisema mradi huo utasaidia kuongeza ari ya kilimo cha mahindi kwenye wilaya hiyo na kuunga mkono jitihada za Rais Dk.John Magufuli za kuhimiza kufanya kazi kwa bidii na kuanzisha viwanda hapa nchini.

Aliwaomba wakulima hasa kwa wanavikundi waliopata mbegu hizo kuhakikisha wanayatunza mashamba darasa hayo kwa manufaa ya wakulima wote wa wilaya hiyo.

Ofisa Kilimo wa Mkoa wa Pwani Kapilima George alisema mbegu hizo zitaongeza mazao ya mahindi kwani licha ya kutumia mbegu zingine mkoa huo kwa mwaka jana ulipata tani 110.
  

Akizungumza kwa niaba ya  Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH wakati wa kukabidhi mbegu hizo, Mkurugenzi wa Fedha wa Fedha na Utawala wa COSTECH, Shabani Hussein alisema kazi kubwa ya COSTECH ni kuishauri serikali katika masuala yote yanayohusu  Sayansi na Teknolojia na kusimamia tafiti zote za kisayansi katika maeneo mbalimbali na kilimo na kuhakikisha zinawafikia walengwa.

Alisema mbegu hizo walizozikabidhi zimefanyiwa utafiti na zitapandwa katika mashamba darasa na baadae kusambazwa kwa wakulima wengine ili kuondoa changamoto ya kukosekana kwa mbegu bora kutokana na wakulima kukabiliwa na mbegu ambazo zilikuwa hazina ubora.

Mtafiti  Kutoka Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha Ilonga mkoani Morogoro, Nikidadi Hamidu alisema iwapo mkulima atafuata ushauri wa upandaji wa mbegu hiyo ya Wema 2109 katika ekari moja atapata magunia 35 tofauti na mbegu nyingine ambapo wanapata chini ya hapo.

Ofisa mradi huo kutoka COSTECH, Bestina Daniel alisema kwa mkoa huo wametoa mbegu kilo 58 kwa ajili ya mashamba darasa katika wilaya ya Bagamoyo na Chalinze ambapo kwa wakulima mmoja mmoja wametoa kilo 42 pamoja na mbolea ya kupandia.




No comments: