Tuesday, March 6, 2018

MTANDAO WA WANAFUNZI(TSNP) WAKANUSHA KUTUMIWA NA WANASIASA NA WANENA HAYA KUHUSU KIFO CHA AQUILINE


Picha inayohusiana
Mwenyekiti wa Mtandao wa wanafunzi Tanzania Abdul Nondo akitoa ufafanuzi wa jambo mapema leo jijini Dar es salaam.

KUHUSU KIFO CHA AQUILINE
Ndugu waandishi wa habari, marehemu Aquiline alikuwa na haki zake za msingi kama binadamu ikiwemo haki za kuishi,na kila taasisi au mtu yeyote ana haki ya kukemea matendo yeyote maovu dhidi ya binadamu.

Tuwaulize TAHLISO, wao wanapata wapi mamlaka ya kukataza, kuonya, kukemea makundi, watu,taasisi zilizoguswa na suala hili kusemea juu ya tukio lile?
Pili, Aquiline alikuwa ni mwanafunzi pia, TSNP ni mtandao wa kutetea wanafunzi, tunayo hayo mamlaka kusemea, kukemea, kushauri na hata kutoa mapendekezo yetu juu ya tukio lolote linaloashiria upotevu wa haki kwa wanafunzi.  TAHLISO wanatoa wapi ujasiri, mamlaka ya kutuzuia TSNP tusitimize wajibu wetu?

Tatu, TSNP tumekuwa mstari wa mbele kusemea shida za wanafunzi mikopo, udahili, wanafunzi kufukuzwa na tumeshirikiana na taasisi za serikali na hata viongozi wa serikali katika utatuzi wa shida za wanafunzi, TAHLISO inayojinasibu kuwa inatetea wanafunzi ije iseme ilifanya nini kati ya haya hadi leo iwe na ujasiri na mamlaka ya kushambulia TSNP.

KUHUSU TSNP KUTUMIWA NA WANASIASA
Ndugu waandishi, TSNP ni taasisi ambayo haifungamani na chama chochote kile cha siasa na haifanyi kazi ya chama chochote.

Na ndiyo maana mara zote mmekuwa mkituona huwa tuna agenda zinazohusu wanafunzi tu kama vile mikopo ya wanafunzi, udahili wanafunzi, mmetuona katika makongamano ya wanafunzi.

Pia tulitoa maoni na mapendekezo yetu kuwa kama hatua stahiki hazitachukuliwa Mh. Mwigulu ajiuzulu (individual ministerial responsibility) kutokana na matendo dhidi ya uvunjifu wa haki za binadamu kushamiri bila kuwepo kwa taarifa juu ya uchunguzi na hatua stahiki kwa wahusika.

Lakini jambo la kushangaza TAHLISO wametoka mbele kutetea serikali na wizara ya mambo ya ndani na kuacha jukumu la kuwatetea wanafunzi.

Inashangaza sana kuona TAHLISO inaishambulia TSNP na kudai kuwa inatumiwa kisiasa ilihali tunashughulika na shida za wanafunzi, na wao wamejisahau wanavyoshughulika na majukumu ya kusemea na kutetea serikali.

Kwa mantiki hii sasa, kama TAHLISO wanatulaumu na kutushambulia, wanatushambulia na kwa lipi?

HITIMISHO
Tunawataka TAHLISO waache kuwa wasemaji wa wizara na serikali na wakumbuke majukumu yao mazito ya kusemea wanafunzi wa vyuo vikuu kwa sababu wanalipishwa ada vyuo vikuu.

Hivyo kulipishwa ada pasipo kutimiza wajibu unaotakiwa kutimiza, hiyo ni silent corruption.
Imetolewa na:
Mtandao wa wanafunzi Tanzania (TSNP)

No comments: