Tarehe kama ya leo (20, Jamadal Akhirah,1439 sawa na 09-03-2018) leo amezaliwa bint wa Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambae ni Bibi Fatma Zahra (a.s),Mtoto huyu au Bint huyu au Mama huyu kwasababu ya daraja lake alilokuwanalo ndani ya Uislamu, Viongozi wa Dini ya Kiislamu, Masheikh wakaitangaza siku ambayo aliozaliwa Mama huyu ni siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani,siku hiyo tumekuwa tukiikumbuka kila mwaka, siku aliyozaliwa mama huyu ni siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani kote.
Yanayotufanya tumkumbuke mama huyu, kwanza ni mwanamke mtakatifu, pili ni mwanamke aliegubikwa na sifa nyingi nzurinzuri zilizojaa ndani ya kitabu kitakatifu cha Quran, lakini vilevile mama huyu amegubikwa na sifa nyingi kutoka kwenye kinywa cha Mtume Muhammad (s.a.w.w), Mama huyu alikuwa kipenzi cha mtume Muhammad (s.a.w.w).
Tunapozungumza Wanawake watakatifu kama vile mama Asia, kama vile mama Khadija, kama vile Mariam aliemzaa Nabii Issa / Yesu (a.s), tunamzungumza vilevile Bi Fatma Zahra ni katika gurupu la wanawake hao.
Bi Fatma Zahra alikuwa na Elimu, Maarifa bila shaka tunahitajia Mama zatu na Dada zetu leo wawe na maarifa na Elimu nzuri,Dunia leo inatafuta maadili mema, dunia leo inachangamoto kubwa ya kupoteza maadili yao, ambayo Mungu amewaumba nayo, Bi Fatma Zahra (a.s) alisifika na maadili mema katika Nyanja zote, pia alisifika na Ukarimu.
Tunaamini vilevile Nyumba ya watu wenye Imani, Nyumba ya Watu wanaomtambua Mungu, Nyumba ya watu wenye hofu na Mungu, Nyumba hiyo inakuwa nyumba salama, bila shaka nyumba inapokuwa salama, jamii inakuwa salama, jamii inapokuwa salama Taifa nalo linakuwa salama, kwahivyo Nyumba ya Bi Fatma Zahra (a.s) ni Myumba ya Mwanamke ambae alikuwa akimuabudu Mungu.
Katika siku hii ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani napenda nigusie jambo zima la haki za Mwanamke ndani ya Uislamu, ziko baadhi ya fikra zinazoona Uislamu haukumpa Mwanamke haki zake, laa, napenda nisieme katika siku hii ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani kwa kukumbuka kuzaliwa kwa Binti ya Mtume Muhammad (s.a.w.w), niseme yakwamba Uislamu unamuangalia Mwanamke na Uislamu unampa Mwanamke haki zake zote.
Mwanamke anayohaki ya kurithi ndani ya Uislamu, Dini ya Uislamu inampa Mwanamke haki ya Kumiliki kama vile mwanaume anavyomiliki,Haki ya kufanya Kazi,Haki ya kuendesha gari,haki ya usawa na haki zingine ambazo ziko kwa mujibu wa dini ya Uislamu.
Katika siku ya leo siku ya Mwanamke wa Kiislamu Duniani napenda nizungumzie jambo la kuvaa sitara au hijabu, Hijabu au Sitara katika Uislamu hakiwekwa kama jambo la kumdhalilisha mwanamke laaa, sitara au hijabu ambayo yakuigwa kutoka kwa Bint ya Mtume Fatma Zahra (a.s), Sitara au hijabu yake haikumzuia kufanya kazi, sitara yake haikumzuia kufanya mambo ya Kiislamu,
sitara yake haikumzuia kuingia darasani kusomesha, sitara yake haikumfanya aache kutoa Hotuba mbele ya Maswahaba wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), kwa hivyo sitara au hijabu ni kitu cha kumsitiri mwanamke, ni heshima kwa mwanamke,ni adabu kwa mwanamke, bali mwanamke amekuwa na dhamani kubwa kwa sababu ya sitara yake.
Mwisho napenda kugusia jambo muhimu sana ambalo ni jambo la kuigwa kutoka kwa binti ya Mtume Muhammad (s.a.w.w) ambae ni Fatma Zahra (a.s), Jambo la Malezi, Mwanamke moja ya kazi aliyokuwa nayo ni kulea jamii iliyokuwa njema,Kama tunataka tutengeneze jamii ya Wachamungu, jamii ya wakweli, jamii ya watu wenye imani, jamii ya watu wanaopenda kusaidiana, ni lazima hili lianze katika ngazi ya familia, na hakuna analolitengeneza hilo isipokuwa ni Mama.
Mama ndio mwenye nafasi ya kutengeneza jamii yenye wakweli, mama ndio mwenye nafasi ya kutengeneza wabunge ambao kesho watatuwakilisha katika bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ahadi zao walizotuahidi na kuzitekeleza, kwasababu gani, Mwakilishi huyu ameleleka katika nyumba ambayo inapoahidi inatekeleza,
kama tunataka kutengeneza Wachapa kazi ambao hawachoki, kama tunataka kuunda watu ambao ni hapa kazi hilo linarudi katika ngazi ya familia na unaona Bi Fatma Zahra (a.s) angalia alivyowalea na kuwatengeneza Watoto wake kama Imam Hassan (a.s), Imam Hussein (a.s) na Bi Zainab (a.s).
Bi.Fatma Zahra ni Mtoto wa Mtume Muhammad (s.a.w.w), Mama yake ni Bi.Khadija, Mume wake ni Sayyidina Ali (a.s), Watoto wake ni Imam Hassan (a.s), Imam Hussein (a.s) na Bi.Zainab (a.s), Babu yake ni Abdallah, Bibi yake ni Amina.
Imetolewa na
Kiongozi Mkuu wa Waislamu Shia Ithnasheriya Tanzania
Maulana Sheikh Hemed Jalala
No comments:
Post a Comment