Thursday, March 22, 2018

TAASISI YA BINTI MAKINI YAIBUA CHANGAMOTO HIZI KATIKA MKOA WA TANGA

Serikali imetakiwa kutoa ajira kwa walimu wa kike hasa kwa maeneo ya vijijini ili kuwasaidia wanafunzi wakike wapate watu wa kuwaeleza changamoto zao  za  kimaumbile ambazo hawawezi kumueleza mwalimu wa kiume.
 Kiongozi wa Taasisi ya Binti Makini Janeth John Kiko akitoa ufafanuzi wa jambo mbele ya washiriki wa Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) mapema wiki hii jijini dar es salaam.

Ameyasema hayo Janeth John Kiko ambaye mwanzilishi wa Taasisi ya Binti Makini katika Semina za Jinsia na Maendeleo (GDSS) wakati akitoa mrejesho wa mafunzo waliyokwenda kuyafanya katika wilaya mbili za Mkoa wa Tanga ambazo ni Muheza na Pangani.

Amesema kuwa mpaka leo hii kuna baadhi maeneo hapa nchini mabinti hawajui matumizi ya toulo za kike na badala yake wanatumia vitambaa kama njia za kujihifadhi, huku akieleza kuwa njia hizo sio nzuri kiafya na zinashindwa kustahimili kwa muda mrefu.

Aidha Bi Janeth ameongezea kuwa miongoni mwa changamoto kubwa walizokutana nazo ni watoto wakike kutopewa thamani yao inayostahili na kufikia kufananishwa na nyanya mbovu ambayo wenyewe watu wa Tanga wanasema ikikaa sana itaharibikia nyumbani hivyo kusababishwa watoto kuozwa wakiwa na umri mdogo.

Aliendelea kusema kuwa watoto wengi katika maeneo hayo wamekosa fursa ya kusoma kutokana na ndoa za utotoni lakini pia kuwaeleza wasifanye vizuri mashuleni kwa kuwa hakuna uwezo wa kuwasomesha endapo watafaulu na kuchaguliwa kuendelea na sekondari.

Washiriki wakifuatilia semina kwa umakini.

“Katika eneo la Pangani kumekuwa na changamoto kubwa ya watoto wa kike kusagana na watoto wa kiume kuwa mashoga na hii inaanzia mashuleni mpaka kwenye mitaa na wazazi pamoja na walimu wameshindwa kuchukua hatua zozote kuwaokoa watoto hawa ambao ni taifa la kesho” alisema Janeth

Kwa upande mwingine ameongelea changamoto zinazowakabili wanawake wa maeneo hayo, hii ikiwa ni pamoja na wanaume wao kutopenda kujishugulisha na kutumia muda mwingi kwa kucheza bao hali inayofanya wanawake hao kuwa ndio wazalishaji mali wakubwa katika familia.

Aliendelea kusema kuwa wanawake katika maeneo hayo hawana sauti katika jambo lolote na wakijaribu kuhoji wanatishiwa kuachwa au kuolewa wake wenza ili kupunguza dharau ndani ya nyumba, lakini pia wanaume wanajisifia kuwa na wanawake wengi ndio msingi wa wao kushinda kwenye bao na kuwafanya wanawake kama mtaji wa kuwazalishia mali.


Dada Nyanjura Kalindo akitoa maoni yake katika semina mapema wiki hii.


Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Bw. Omary Uled akichngia mawazo katika semina ilikuwa ikihusu changamoto za kijinsia katika Mkoa wa Tanga.


Semina ikiendelea.

No comments: