Saturday, June 18, 2022

Tamko la Global Peace Foundation kwenye siku ya Mtoto wa Afrika.

Mkurugenzi mkaazi, wa Global peace Foundation Tanzania Bi. Martha Nghambi.

Maadhimisho ya siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16

Global Peace Foundation Tanzania (GPF), ni asasi ya Kiraia inayofanya kazi ya kuelimisha jamii na kujenga uwezo kwa makundi mbalimbali ya kijamii juu ya umuhimu wa kulinda Amani nchi Tanzania, ikiwa imejikita zaidi katika mikoa ya Kusini mwa Tanzania  hasa ile iliyopakana na nchi jirani. Pamoja na hayo, Taasisi inafanya kazi katika eneo la kujenga uwezo kuhusu haki na usawa wa Kijinsia katika nyanja zote.
Kila mwaka tarehe 16 Juni Tanzania inaungana na Nchi zingine za Afrika kuadhimisha Siku ya Mtoto wa Afrika.

Chimbuko la Maadhimisho haya ni Azimio lililopitishwa na uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) mwaka 1990 kwa lengo la kuwakumbuka watoto wa kitongoji cha Soweto nchini Afrika ya Kusini waliouawa tarehe 16 Juni, 1976 kutokana na ubaguzi wa rangi.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “Maendeleo Endelevu 2030: Imarisha Ulinzi na Fursa Sawa kwa Watoto” Kauli mbiu hii inawataka wazazi, walezi, Serikali na wadau wengine kuzingatia wajibu wetu katika kuimarisha mifumo ya ulinzi na maendeleo ya Mtoto ili aweze kudhibiti changamoto ya ongezeko la vitendo vya ukatili nchini pamoja na kutoa haki sawa kwa watoto wote bila ubaguzi wa aina yoyote.

Sisi Global Peace Foundation, mwaka huu tunaikumbusha jamii kuhakikisha inawalinda watoto dhidi ya vitendo vya Ukatili wa Kijinsia na unyanyasaji ambao unaweza kupelekea kuathirika kisaikolojia na kujiingiza kwenye migogoro ya kifamilia au makundi hatarishi.
Kukosekana kwa ulinzi na usalama kwa watoto wadogo katika ngazi ya familia, kunawaweka katika mazingira hatarishi ya kujiingiza kwenye makundi yanayochochea vurugu na chuki na kuongezeka kwa watoto wa mitaani. 

Tunaisisitiza jamii ya watanzania wote, kushirikiana na Mamlaka za serikali za Mitaa katika kuweka mikakati ya kuwalinda watoto wote, kusaidia kuwaondoa watoto walioko katika mazingira hatarishi na kuwaweka mahali salama ili kuwa na vijana wa baadaye watakao kuwa wazazi bora na wenye hulka ya kulinda na kuijenga Amani ya taifa letu. 
GPF tunasisitiza, kuwekwa kwa mikakati dhabiti ya kisera, ikiwa ni pamoja na kuimarisha Kamati za Ulinzi wa mama na mtoto ngazi ya Kijiji, Mitaa na Kata ili kutokomeza vitendo vya Ukatili wa Kijinsia. 

Aidha Tunaendelea kuishauri serikali kuharakisha maandalizi ya Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia kwa wanawake na watoto wa Pili (NPA-VAWC II) ili kuboresha zaidi Mikakati ya kukabiliana na changamoto  za Ukatili kwa watoto. Watoto wasipofanyiwa ukatili wa Kijinsia tutakuwa na jamii yenye Amani na inayojali Amani. 

Imetolewa na 

Martha Nghambi
Mkurugenzi Mkaazi
Tanzania
June 15,2020

No comments: