Monday, October 1, 2012

Wateja wa Tigo Sasa Wanaweza Kununua Maudhui Mtandaoni Kupitia Tigo Pesa





Tigo Pesa na Google team waungana kuwezesha Watanzania kulipia maudhui au application yoyote inayopatikana Google Play Store

  
Je umewahi kutaka kununua muziki, cinema, apps au kusoma maudhui kwenye mtandao wa Google Play Store lakini ukashindwa kufanya hivyo kwa sababu hukuwa na kadi ya benki?

Tangu Juni ya mwaka huu, kampuni inayoongoza kwa maisha ya kidigitali nchini, Tigo iliingia katika makubaliano na Google kuwapa wateja uwezo wa kulipia maudhui kutoka mtandao wa Google Play Store kwa njia ya Tigo Pesa.

Huduma hii inayowezeshwa na Bango inawawezesha wateja 7 milioni wanaotumia  huduma ya kifedha ya Tigo Pesa kulipia maudhui au application yoyote inayopatikana Google Play Store kwa kutumia akaunti yao ya Tigo Pesa.

‘Wateja wa Tigo wanaotumia simu janja za Android ama tablet sasa wanaweza kufanya manunuzi ya moja kwa moja au malipo kwa njia ya kujisajili kupitia Play Store. Huduma hii inapatikana kwa njia rahisi na haraka mahali popote pale nchini kupitia Tigo Pesa. Hii inawapa wateja wetu uwezo zaidi wa kupakua na kufurahia maudhui ya kimtandao kutoka Google Play Store huku wakitumia mtandao wetu wa uhakika na wenye kasi ya juu zaidi wa 4.5G nchini,’ Mkuu wa Huduma ya Kifedha ya Mtandao wa Tigo, Hussein Sayed alisema jijini Dar es Salaam leo.

Suluhisho hili linawawezesha wateja kufurahia huduma za manunuzi ya bidhaa na huduma walizozoea kwa kuunganisha matumizi ya Google Play na Tigo Pesa. Ili kukamilisha manunuzi mteja anatakiwa kufuata hatua za kawaida za kufanya manunuzi kwenye Play Store na katika hatua ya kufanya malipo achague Tigo Pesa. Fuata hatua rahisi za kuunganisha akaunti yako ya Google na akaunti yako ya Tigo Pesa kisha unda na uingize herufi 6 za siri zitakazotumiwa kwa manunuzi yote ya Play Store.

Mahir Sahin, Mkurugenzi wa Google – Huduma za Android Barani Afrika, alisema “Tuna furaha kubwa kuungana na Tigo kuzindua ubunifu huu utakaowezesha wateja wa Tigo Pesa kufanya malipo ya moja kwa moja kwenye Googe Play Store. Hii itawezesha mamilioni ya Watanzania ambao hawana kadi za benki kufurahia huduma kamili za maudhui yanayopatikana kwenye Google Play.”

‘Tigo inaongoza mageuzi ya maisha ya kidigitali na Tigo Pesa ndio kinara wa ubunifu katika utoaji wa huduma za kifedha kwa njia ya mtandao, kwa sababu ndio huduma ya kwenza kuwezesha Watanzania kununua maudhui kutoka Google Play Store. Hii inathibitisha kuwa Tigo Pesa ni huduma kamili ya kifedha inayowapa wateja huduma nyingi na bora zaidi za malipo,” Hussein aliongeza.

Idadi kubwa ya Watanzania wanapenda kutumia simu zao za mkononi kufanya manunuzi ya huduma ya bidhaa, na sasa Tigo inawawezesha kununua maudhui wanayopenda zaidi kupitia huduma inayoongoza duniani ya Tigo Pesa.


No comments: