Saturday, May 11, 2013

SIMBA SC WAENDA NUNGWI KUWEKA KAMBI YA KUENDELEZA UBABE KWA YANGA



SIMBA SC inaondoka kesho jioni kwenda kisiwani Zanzibar, kuweka kambi maeneo ya Nungwi kujiandaa na mpambano dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC Mei 18, mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
HABARI 24 inafahamu Simba SC imekata tiketi za kuondoka na boti ya saa 10:00 jioni kesho na ikifika huko, itaweka kambi katika nyumba moja kubwa ya kifahari ya mpenzi milionea mmoja wa klabu hiyo (jina tunalihifadhi).

        Na ikiwa kambini hapo, Simba SC itakuwa ikifanya mazoezi kwenye Uwanja mmoja mzuri tu ulio jirani kabisa na nyumba hiyo.
Kutoka kikosi kilichoshiriki mchezo dhidi ya Mgambo JKT Jumatano, anaongezeka Mwinyi Kazimoto tu na kufanya jumla ya wachezaji 22 wanaokwenda kambini.

        Wachezaji wanaotarajiwa kuondoka kesho ni makipa; Abbel Dhaira, Juma Kaseja, mabeki Nassor Masoud ‘Chollo’, Omary Salum, Haruna Shamte, Miraj Adam, Hassan Khatib, Shomary Kapombe, William Lucian ‘Gallas’, viungo Jonas Mkude, Abdallah Seseme, Mussa Mudde, Mwinyi Kazimoto, Amri Kiemba na washambuliaji Mrisho Ngassa, Felix Sunzu, Edward Christopher, Rashid Ismail, Ramadhani Singano ‘Messi’, Salim Kinje na Haroun Chanongo.
Simba SC inakwenda kambini kesho, ikiwa siku mbili tangu wapinzani wao waende Pemba kuweka kambi kwa ajili ya mechi hiyo.
Yanga SC imeweka kambi katika hoteli ya Samail Morden, mkabala na benki ya PBZ na kesho inafanya mazoezi kwenye Uwanja wa Gombani.
     
       Pamoja na kwamba Yanga tayari imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu, lakini inaipa uzito mkubwa mechi hiyo kwa sababu inataka kulipa kisasi cha kufungwa 5-0 na wapinzani wao hao wa jadi mwaka jana.

        Tangu umeingia madarakani, uongozi wa Yanga chini ya Mwenyekiti, Alhaj Yussuf Mehboob Manji umekuwa ukiumia kichwa na kipigo cha 5-0 mwaka jana.
Mara kadhaa Manji amewahi kukaririwa na BIN ZUBEIRY akisema kwamba 5-0 zinamuumiza kichwa hasa katika wakati ambao idadi ya mabao katika mechi za timu hiyo ilipungua.
 
     Kihistoria, Simba SC imewahi kuipa Yanga vipigo viwili vitakatifu 6-0 mwaka 1977 na 5-0 mwaka jana, wakati Yanga iliifunga SImba 5-0 mwaka 1969.
Safari hii, Yanga imepanga kuweka heshima kwa kuhakikisha inaipa kipigo kitakatifu Simba cha kuvunja rekodi ya 6-0.

No comments: