KESI DHIDI YA PINDA...MAPINGAMIZI 119 YAWAKILISHWA KWENYE KESI DHIDI YA WAZIRI MKUU MIZENGO PINDA ILI KUMNASUA MAHAKAMANI...! SOMA HAPA
KAMATI ya Vijana Wapenda Amani Tanzania, wanatarajia kuwasilisha
mapingamizi 119 wakiomba kesi dhidi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda itupwe
kwani ilifunguliwa kinyume cha Katiba. Pinda alishitakiwa kikatiba
Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kutokana na kauli aliyoitoa bungeni
hivi karibuni akiruhusu Jeshi la Polisi kuwapiga raia wanaokaidi amri
halali za jeshi hilo.
Kesi hiyo iliyofunguliwa na mawakili mbalimbali, itasikilizwa na
majaji watatu wakiwamo Jaji Kiongozi, Fakih Jundu, Jaji Augustine
Mwarija na Jaji Dk. Fauz Twaib.
Taarifa hiyo ilibainishwa jana
katika barua iliyoandikwa na kamati hiyo kupitia wakili wao, Sweetbert
Nkuba kwenda kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mahakama Kuu kupatiwa
nakala.
Nkuba aliwasilisha barua kwa Mwanasheria Mkuu wa
Serikali, Jaji Frederick Werema akiomba wateja wake kuingizwa katika
kesi hiyo kwa ajili ya kumtetea Pinda.
Nkuba alisema kesi hiyo
isipofutwa itakuwa na athari kiserikali, kwani mahakama itakuwa
imeruhusu watu wasiokuwa na shughuli maalumu kukwamisha mipango ya
Serikali.
“Tutakapokubaliwa kuingia katika kesi, tunatarajia
kuwasilisha mapingamizi 119 mahakamani tukiomba kesi hiyo itupiliwe
mbali kwani imefunguliwa kinyume na Katiba.
“Kama mahakama
itakubali kuendelea na kesi dhidi ya Waziri Pinda, Serikali itashindwa
kufanya kazi yake kwa sababu kila maamuzi yanayotolewa na viongozi
yatakuwa yanapingwa mahakamani na makundi ya watu wasiokuwa na shughuli
maalumu.
“Tunaweza kukubaliwa kuingia katika kesi kwa sababu
tayari tuna watu 2,000 waliosaini wakipinga waziri mkuu kushtakiwa,”
alidai wakili Nkuba.
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC)
kwa kushirikiana na Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), walifungua
kesi namba 24 ya mwaka 2013, wakipinga kauli hiyo ya waziri mkuu.
Katika
hati ya madai inadaiwa kwamba Mei mwaka huu, Pinda akiwa bungeni kama
waziri mkuu kinyume na Katiba, alitoa kauli ya kuruhusu askari wa Jeshi
la Polisi kuwapiga raia ambao hawatatii amri yao.
“Kama wewe
umekaidi, hutaki, unaona kwamba ni imara zaidi, wewe ndio jeuri zaidi
watakupiga tu na mimi nasema muwapige tu kwa sababu hakuna namna
nyingine, eeh maana tumechoka sasa,” ilieleza sehemu ya hati hiyo
ikinukuu kauli ya Pinda.
Wanadai kwa mujibu wa utekelezaji wa
sheria za jinai, kauli inayotolewa na kiongozi mwenye wadhifa wa waziri
mkuu, ni amri inayopaswa kutekelezwa na vyombo vya dola kama Polisi.
No comments:
Post a Comment