Na Karoli Vinsent
GAZETI LA TANZANIA DAIMA LEO LIMEAMUA KUANDIKA HABARI AMBAYO IMEKUWA GUMZO SANA KATIKA VICHWA VYA HABARI JIJI DAR ES SALAAM NA TANZANIA KWA UJUMLA HABARI AMBAYO ILIKUWA NA KICHWA CHA HABARI KINACHOSEMA --BAADA YA ULIMBOKA NA KIBANDA KOVA AIBUKIA KWA DK MVUNGI.
PATA NAFASI YA KISOMA KWA MAKINI YOTE HAPA--
inaendelea hapa
JESHI la Polisi limeonyesha wazi kuwa
halina dhamira ya dhati ya kuwasaka na kuwatia nguvuni wahalifu waliowateka,
kuwatesa na kuwaumiza vibaya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini (TEF),
Absalom Kibanda, na Mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
Ni zaidi ya mwaka mmoja na miezi minne
tangu Dk. Ulimboka atendewe unyama huo lakini hadi leo suala hilo limegeuzwa
sinema na jeshi hilo kwa kumkamata mtu asiyehusika ambaye baadaye walilazimika
kumwachia huru.
Hivi ndivyo imetokea pia kwa Kibanda
ambaye ni Mahriri Mtendaji wa Kampuni ya New Habari (2006), kwani tangu ateswe
na kung’olewa jicho, kucha, meno na kukatwa kidole, hakuna mtuhumiwa hata mmoja
aliyekamatwa ikiwa ni zaidi ya miezi saba sasa.
Lakini jana Waziri wa Mambo ya Ndani ya
Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, akiongozana na maofisa wengine wa jeshi hilo
akiwemo Kamishna wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, waliitisha
mkutano na waandishi kuwataja ‘vibaka’ waliokamatwa wakihusishwa kumshambulia
na kumwibia Dk. Sengondo Mvungi.
Dk. Mvungi ni mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambaye alivamiwa na
majambazi hao takriban wiki mbili zilizopita na kukatwa mapanga na kuporwa
kompyuta mpakato (laptop) na fedha.
Kwa sasa hali yake ni mbaya akiwa bado
hajitambui na hivyo kulazimika kupelekwa nchini Afrika Kusini kujaribu kuokoa maisha
yake.
Hatua ya Waziri Nchimbi kujitokeza
jana kuzungumzia tukio hilo na kuonyesha juhudi za haraka za kuwanasa
watuhumiwa, iliwasukuma waandishi wa habari kuhoji kulikoni matukio ya Ulimboka
na Kibanda yamewekwa kiporo.
Kama kawaida yake, Kamishna Suleiman
Kova alijibu kuwa kila tukio lina mazingira yake, hivyo tukio la Mvungi
halifanani la Kibanda wala Dk. Ulimboka na kueleza kuwa mfumo wa suala hilo
kiupelelezi unakwenda vizuri.
“Tukio la Mvungi na la kina Kibanda
na Ulimboka mazingira yake ni tofauti; unapeleleza halafu unatuhumiwa wewe
mwenyewe, ila watapatikana,” alisema Kova.
Katika taarifa yao hiyo, Dk. Nchimbi
na Kova walisema kuwa wamekamatwa watuhumiwa wengine watatu zaidi wanaodaiwa
kumvamia, kumjeruhi kwa mapanga na kumpora mali Dk. Mvungi.
Kova alisema kuwa operesheni ya
kuwasaka waliomshambulia Dk.Mvungi imefanikiwa kwa asilimia zaidi ya 80 ambapo
mpaka sasa wamekamatwa watu tisa wakiwa na vifaa walivyotendea uhalifu huo
ambavyo ni mapanga matano, simu ya mkononi na kigoda.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni
Msigwa Kopelo, Chibango Magozi, Ahmed Ally, Zakaria Rafael (23) dereva wa boda
boda, Manda Salowaa ( 40), Paulo Jailos (29), Juma Hamisi (29), Longishu
Semaliki(29) muuza ugoro Vingunguti na Masunga Makenza (40).
Dk. Mvungi ambaye pia ni mshauri wa
masuala ya kisheria wa Chama cha NCCR-Mageuzi alipatwa na mkasa huo usiku wa
kuamkia Novemba 3, mwaka huu, akiwa nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, Manispaa ya
Kinondoni jijini Dar es Salaam.
Baada ya kumjeruhi waliiba sh
milioni moja, bastola, simu mbili za mkononi na kompyuta mpakato (laptop).
Utendaji huu wa jeshi la polisi
unaacha mashaka makubwa hasa kwa matukio makubwa ya utekaji na utesaji ambayo
ni mageni nchini, kwani uchunguzi wake wa kuwasaka watuhumiwa unalegalega.
Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya
tukio la Dk. Ulimboka Julai 26 mwaka jana, jeshi hilo liliunda kikosi kazi
kilichowashirikisha wataalamu mbalimbali wa kanda maalumu na makao makuu.
Hadi sasa ripoti yake haikuwahi
kutolewa hadharani kama Kova alivyojigamba wakati akiitangaza, badala yake hivi
karibuni amekuwa akitupiana mpira na wakuu wake kuhusu ripoti hiyo.
Dk. Ulimboka kwa kiapo aliwataja
watu aliowatuhumu kuhusika na tukio hilo, mmoja wao akiwa ni ofisa usalama wa
taifa-Ikulu lakini hakuwahi kufanyiwa gwaride la utambuzi wala kuhojiwa na
kamati hiyo ya uchunguzi.
Siku chache kabla ya Dk. Ulimboka
kumtaja ofisa huyo, gazeti la MwanaHalisi lilichapisha habari iliyoeleza tukio
zima lakini serikali ikalifungia kwa muda usiojulikana kwa kile kinachoitwa
kosa la uchochezi.
Tukio hilo la Dk. Ulimboka limekuwa
kama sinema kwani hata mtuhumiwa pekee raia wa Kenya, Joshua Mulundi, aliyekuwa
amekamatwa na kuwekwa ndani kwa muda kadhaa na kufunguliwa kesi, ukamatwaji
wake ulikuwa wa kutia mashaka.
Wakati vinywa vya wananchi vikiwa
bado vinatafakari unyama huo, tasnia ya habari nayo iliingiliwa kwa
kushambuliwa kiongozi wa wahariri katika tukio kama lilelile la Dk. Ulimboka.
Matukio haya ni kama ya kupangwa
kutokana na kufanyika kwa ustadi wa hali ya juu na kwa muda mfupi tena bila
wahusika kuchukua chochote kwa mteswaji.
Kama ilivyokuwa kwa Dk. Ulimboka,
pia kwa Kibanda, iliundwa kamati ya uchunguzi iliyoongozwa na wataalam wakiwemo
walewale walioshindwa kuwakamata watesaji wa Dk. Ulimboka.
Hadi leo hakuna mtuhumiwa hata mmoja
ametiwa nguvumi na jeshi la polisi ambalo kila siku viongozi wake wamekuwa
wakijinasibu kuwa na intelijensia ya hali ya juu inayobaini matukio ya kihalifu
kabla ya kutokea, mathalani kuzuia maandamano na mikutano ya vyama kwa madai ya
kuepusha vurugu.
Wadadisi wa maswala ya mambo
wanashangaa jinsi maswala haya yakiwa yanaregarega katika kufanyiwa uchunguzi
huku waandishi wa habari wakifanya uchunguzi na kufanikiwa kubaini watu
wanaofanya unyama huo mfano Gazeti lilofungiwa la mwanaharisi lilifanya
uchunguzi na kufainikiwa kumbaini mtuhumiwa aliyefanya unyama na pia
kuthibitishwa na ulimboka mwenyewe,lakini katika hali yakushangaza serikali
ikalifungia gazeti la mwanaharisi kwa madai kuwa lilifanya uchochezi huko
likishindwa kumchukulia hatua mtu aliyejulikana kwa jina la Ramadhani Ighondu
ambaye inasemekana ni mfanyakazi wa idara ya usalama wa taifa
Huku serikali hii sikivu ya CCm
ikishindwa kusema bayana wahusika maswala haya ya kinyama.
No comments:
Post a Comment