WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII MHE. DKT. HUSSEIN A. MWINYI |
WIZARA
YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
TAMKO
LA WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII MHE. DKT. HUSSEIN A. MWINYI (Mb) LA SIKU
YA KISUKARI DUNIANI, TAREHE 14 NOVEMBA 2013
Ndugu Wananchi,
endelea hapa
Siku
ya kisukari Duniani, huadhimishwa duniani kote kila mwaka tarehe 14 ya Mwezi
Novemba.
Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya
kisukari Duniani mwaka 2013 ni“Linda
Maisha yajayo dhidi ya ugonjwa wa Kisukari” Kauli mbiu hii inalenga kuhamasisha jamii juu ya matatizo mbalimbali
yanayotokana na ugonjwa wa kisukari katika jamii.
Tanzania
kama zilivyo nchi nyingine duniani inaadhimisha siku hii, kwa Wizara ya Afya na
Ustawi wa Jamii kushirikiana na Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania kutoa elimu ya umuhimu wa kuzuia na kujikinga
na madhara mbalimbali yatokanayo na ugonjwa wa kisukari.
Ndugu Wananchi,
Ugonjwa
wa Kisukari ni hali ambayo hutokea wakati sukari katika damu inapokuwa nyingi
kupita kiwango cha kawaida kwa muda mrefu. Sukari hutumiwa na mwili ili kupata
nishati lishe. Ili mwili uweze kutumia sukari inayotokana na vyakula, unahitaji
kichocheo cha insulin. Insulin husaidia sukari kuingia kwenye chembechembe hai
ili kutengeneza nishati lishe. Ugonjwa wa kisukari unasababishwa na kichocheo
hiki kupungua au kutofanya kazi kama inavyotakiwa, hivyo kiwango cha kisukari
kinabaki kikubwa kwenye damu kwa sababu sukari haikuwezeshwa kuingia kwenye
chembechembe hai za mwili
Ndugu Wananchi,
Tafiti
za ugonjwa wa kisukari zinaonyesha kuwa mwaka 2007 kulikuwa na wagonjwa 246
milioni duniani. Ttakwimu za mwaka 2012 zinaonyesha kuwa kulikuwa na wagonjwa
371 milioni ulimwenguni kote, ambapo nusu ya wagonjwa hawa walikuwa hawajaanza
matibabu. Asilimia 80 ya wagonjwa wote wa kisukari ulimwenguni wanaishi katika
nchi zinazoendelea, ikiwemo Tanzania.
Utafiti
uliofanyika mwaka 2012 na kuhusisha wilaya 50 nchini Tanzania ulionyesha ya
kuwa asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wana
ugonjwa wa kisukari.
Katika
nchi 10 zinazoongoza kwa kisukari barani Afrika Tanzania inashika nafasi ya 8.
Ndugu Wananchi,
Kauli
mbiu ya maadhimisho ya siku ya kisukari duniani kwa mwaka 2013, inalenga
kuelimisha na kuhamasisha jamii kuhusu kinga dhidi ya ugonjwa wa kisukari
pamoja na kubainisha mambo ambayo yanaongeza uwezekano wa kupata maradhi yasiyo
ya kuambukiza ikiwemo kisukari. Magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza yanayoendana
na kisukari ni pamoja na magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani na
magonjwa sugu ya njia ya hewa.
Mambo
yanayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa haya yasiyo ya kuambukiza ni pamoja
na ulaji usiofaa hasa matumizi ya chumvi kwa wingi, mafuta na sukari, uzito
uliozidi, unene uliokithiri, kutofanya mazoezi, uvutaji wa sigara na bidhaa
zitokanazo na tumbaku, unywaji pombe kupita kiasi na msongo wa mawazo.
Ndugu Wananchi,
Ulaji
usiofaa ni kula chakula bila kuzingatia aina na kiasi
kulingana na mahitaji ya mwili. Hii huweza kusababisha kupungua au kuzidi kwa
virutubishi mwilini. Ulaji usiofaa ni pamoja na kula vyakula vyenye mafuta
mengi hasa yale yatokanayo na wanyama, kula vyakula vyenye chumvi nyingi,
sukari nyingi, kula chakula kupita kiasi, kukoboa nafaka na kutokula mbogamboga
na matunda kiasi cha kutosha. .
Kutofanya
Mazoezi ya mwili chakula
kinacholiwa kwa kawaida hutumika na mwili kufanya kazi mbalimbali. Iwapo
chakula hakitatumika hubadilishwa na kuhifadhiwa mwilini kama mafuta na
hatimaye husababisha uzito kuzidi. Mambo yanayochangia mwili kutotumia chakula
kilicholiwa ni pamoja na kukaa muda mrefu bila kufanya mazoezi ya mwili, kwa
mfano : kuketi ofisini, darasani, kukaa na kuangalia runinga kwa muda
mrefu, kutumia lifti kwenda ghorofani badala ya ngazi, kupanda gari mahali pa
umbali mfupi badala ya kutembea kwa miguu, na kutoshiriki katika michezo.
Uzito
na unene uliozidi uzito unakuwa
umezidi pale ambapo uzito wa mtu unakuwa asilimia 20 zaidi ya uzito unaotakiwa.
Ili kupima hali hiyo viashiria mbalimbali hutumika; njia inayotumika mara
nyingi ni ile ya uwiano wa uzito na urefu wa mwili kulingana na viwango maalumu
vilivyowekwa.
Msongo
wa mawazo huweza kusababisha
ulaji usiofaa na huweza kufanya mifumo mbalimbali ya mwili kutofanya kazi
vizuri.
Matumizi
ya pombe huchangia katika
kuongeza uzito mara nyingi. Unywaji wa pombe za aina zote huendana na ulaji wa
vyakula kwa wingi ambayo huchangia kuongeza uzito. Pombe yenyewe ikizidi
inaweza kuharibu maini, kusababisha utapiamlo kwa wale wanaoishia kunywa pombe
zaidi ya kula chakula.
Uvutaji
wa Sigara na matumizi ya bidhaa zitokanazo na Tumbaku licha ya kuwa ni
matumizi yasiyo na tija, tumbako husababisha madhara mengi mwilini yakiwemo
magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani na magonjwa sugu ya njia ya hewa.
Ndugu Wananchi,
Ili
kuzuia ugonjwa wa kisukari na maradhi mengine yasiyo ya kuambukiza ni muhimu kufuata kanuni za afya
ambazo ni ulaji bora, na mtindo bora wa maisha ambao ukifuatwa vyema huweza kwa
kiasi kikubwa kuzuia mtu kupata kisukari au kwa mtu ambaye tayari ana ugonjwa
wa kisukari hupunguza uwezekano wa kupata madhara makubwa ya kiafya.
Ndugu Wananchi,
Serikali
inaendelea na utekelezaji wa Sera ya Afya (2007) ambayo inalenga kutoa huduma kwa
magonjwa yasiyo ya kuambukiza ikiwemo
kisukari kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa ndani ya nchi na wa kimataifa.
Aidha, serikali, sekta binafsi, mashirika ya kimataifa na taasisi zinazotoa
huduma bila faida zinaendelea kuandaa na kurekebisha sheria, kanuni na taratibu
zinazoimarisha uzuiaji na udhibiti wa magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Serikali
kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inatumia maadhimisho haya
kuwa sehemu ya uhamasishaji kwa jamii kama ilivyo kwenye nchi zote duniani.
Ndugu Wananchi,
Serikali
inaeendelea kuandaa miongozo na mikakati ya kisera kwa kushirikisha jamii
katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza,
ikiwemo kisukari.
Serikali
imeimarisha ushiriki wa sekta mbalimbali za umma na za binafsi katika
kukabiliana na vyanzo vinavyosababisha magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Ndugu wananchi,
Kwa
kutambua gharama za kutibu ugonjwa wa kisukari, kuanzia mwaka 1993, serikali
ilitoa msamaha kwa wagonjwa wote wa kisukari kutochangia gharama za matibabu na
inajitahidi kwa uwezo wa bajeti yetu pamoja na wahisani wetu kuhakikisha kuwa
dawa muhimu zinapatikana. Kwa sasa watoto wote na vijana chini ya miaka
ishirini na miwili walio na kisukari wanapata mahitaji yao yote kupitia kliniki
za kisukari zilizopo nchini.
Kuanzia
mwaka 2012, serikali pamoja na washirika wake inatekeleza mpango wa kuthibiti
ugonjwa wa kisukari nchini. Lengo ni kuwa na kliniki hizo hadi katika hospitali
za wilaya kwa sasa zipo kliniki za kisukari kwenye ngazi za mikoa na kuwapatia
wananchi elimu ya ugonjwa wa kisukari ili waweze kushiriki kikamilifu kwenye
kinga na tiba ya magonjwa haya.
Tanzania
inaungana na mataifa yote duniani kutekeleza azimio la Umoja wa Mataifa la
mwaka 2011 la kuhakikisha ya kuwa kuna mpango kabambe wa kuthibiti magonjwa
yasiyo ya kuambukiza. Nchi yetu inaungana na mataifa mengine kuhakikisha ya
kuwa magonjwa yasiyo ya kuambukiza
yanapungua kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2025. Sasaunaandaliwa mpango huo kwa kukishirikiana na wadau wengine wahusika.
Ndugu
wananchi,
Kama nilivyosema mwanzoni, wengi wetu hawajitambui ya
kuwa wana ugonjwa huu. Wengine wanakuwa na dalili lakini hawachukui hatua
mapema. Dalili za kisukari ni rahisi kuzitambua nazo ni: kiu isiyoisha, kukojoa
mara kwa mara, kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati na mwili kukosa nguvu.
Ukiwa na dalili hizi nenda hospitali ukapime sukari.
Ndugu
wananchi,
Kwa bahati mbaya, unaweza kuwa na ugonjwa huu kwa muda
mrefu bila kuwa na dalili nilizotaja hapo awali. Hata hivyo, jinsi sukari inavyokuwa
juu, inaharibu mishipa ya damu na ya fahamu, macho, figo na kusababisha upofu,
moyo na figo kushindwa kufanya kazi, na miguu kufa ganzi, kuwa na vidonda.
Hivyo ninatoa
wito kwa kila mmoja wetu kuhakikisha
kuwa anapima afya yake kwa kuwa ugonjwa huu unaweza usionyeshe dalili yoyote
mapema. Ni vyema kila mmoja akapima afya yake mara kwa mara ili kutambua hali
yake ya afya. Endapo utatambuliwa kuwa una ugonjwa wa kisukari tumia huduma za
afya kulingana na ushauri utakaopewa na wataalam wa afya.
Kwa wale ambao
wameshajitambua kuwa na matatizo ya kisukari lakini hawatumii huduma za
afya ipasavyo, nawaasa watumie huduma za afya zilizopo kwa manufaa ya afya zao
na kuepusha athari zinazotokana na ugonjwa ya kisukari.
ASANTENI KWA KUNISIKILIZA
No comments:
Post a Comment