Friday, December 6, 2013

MKASA MZIMA WA BAUNSA AUWA KWA RISASI HUKO TEMEKE-DSM

 
Stori:  Hamida Hassan na Gladness Mallya
KIJANA aliyefahamika kwa jina moja la Andrew, mkazi wa Yombo, jijini Dar amedaiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na mlinzi ‘baunsa’ wa Kampuni ya Harvest Public Action iliyopewa dhamana ya kuuza nyumba na Benki ya BOA.
Marehemu Andrew enzi za uhai wake.
Kikizungumza na Ijumaa hivi karibuni, chanzo makini kilidai Endrew alifika na pikipiki katika eneo la nyumba moja iliyopo Temeke mtaa wa Uwanja wa Taifa, Kata ya Mgulani, Wilaya ya Temeke yenye kitalu namba KT/MBR/BS/47 kwenda kushuhudia mnada huo ndipo alipopigwa risasi. Chanzo kilidai kuwa, mnada huo ulikuwa ni kwa ajili ya kuuza nyumba ya marehemu Thabit Tibwa ambapo Endrew aliagizwa na bosi wake akaangalie inauzwa bei gani.
Jeneza lenye mwili wa marehemu Andrew.

Ilidaiwa, nyumba hiyo ilikuwa kwenye mgogoro ambapo baba mdogo wa watoto wa marehemu ambaye ndiye msimamizi wa mirathi aliyetambulika kwa jina moja la Robert, alichukua mkopo katika Benki ya BOA huku akiandika nyumba hiyo kama dhamana yake, akashindwa kulipa. Chanzo hicho kiliendelea kudai kuwa, baada ya kijana huyo kufika eneo la mnada, yalitokea majibizano kati ya wauzaji na baadhi ya wateja waliojitokeza na baunsa wa kampuni hiyo alidaiwa kumpiga risasi Andrew na kusababisha kifo chake. “Walimpiga risasi, akafariki palepale huku watu wengine wakikimbia kuokoa maisha yao,” kilisema chanzo hicho bila kufafanua zaidi chanzo cha mabishano hayo.
 Andrew baada ya kupigwa risasi.
Mwenyekiti wa serikali ya mtaa huo, Vincent John, alisema siku hiyo akiwa ofisini kwake, walifika vijana wawili waliomletea barua ya kumpa taarifa juu ya mnada huo. “Tuliwaambia nyumba hiyo ni ya watoto na ina mgogoro ambao umefikishwa mahakamani na kesi yake ingeanza kusikilizwa Jumatatu ya Desemba 2, lakini wao walisema hiyo haiwahusu na ndipo yakatokea hayo,” alisema mwenyekiti huyo na kuongeza: “Tulitoka na kushuhudia maiti na tulipouliza kulikoni wale mabwana wa Harvest waliingia kwenye gari na kukimbiza gari lao, hata hivyo tulipokwenda Kituo cha Polisi Chang’ombe, tuliwakuta wameshajisalimisha mikononi mwa polisi na kusema wameua kwa bahati mbaya walipokuwa wakijihami.”  Diwani wa mtaa huo, Juma Mkenga alisema amesikitishwa na tukio hilo na kuiomba serikali ihakikishe inakusanya silaha kwa watu wasiokuwa na vigezo vya kumiliki silaha hizo kwani mauaji ya silaha yamezidi kushamiri kila kukicha.
                GPL

No comments: