WENYEKITI wa Chadema wilayani Temeke, jijini Dar Joseph Yona,33,
ameeleza A-Z sakata la kutekwa, kuteswa kwake na vijana sita wakati
akienda nyumbani kwake Mtoni kwa Azizi Ally.
Mwenyekiti
wa Chadema wilaya ya Temeke na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho,
Joseph Yona akipelekwa Kitengo cha Mifupa Muhimbili (MOI) kutoka wodini.
Akisimulia mkasa huo kwa mwandishi wa gazeti hili juzi Jumanne akiwa
Hospitali ya Taifa, Muhimbili, Yona ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu,
Taifa Chadema alikuwa na haya ya kusema: “ Majira ya usiku nikiwa na
baadhi ya vijana wa Chadema Tawi la Ukombozi lililopo karibu na kwangu
maeneo ya Benki Klabu, Mtoni kwa Azizi Ally tulikuwa tukiongea.
ENDELEA ------------
“Ilipofika saa sita tukatawanjika mimi nikawa naelekea nyumbani,
kabla sijafika mbali nikashitukia vijana sita wakinivamia na kunikaba
kisha kunivua tisheti na kunifunga usoni, wakaniingiza katika gari
ambalo walikuwa wamepaki pembeni.
“Nilipowauliza
mnanipeleka wapi? Wakawa wanajifanya ni askari kwani walikuwa wanasema,
‘tumeshamkamata, tunamleta huko kituoni afande’, tukiwa njiani
waliniambia niseme Zitto ni msaliti badala yake nikawaambia kuwa hilo
waulizeni viongozi wa juu.
“Baada ya kuona tumesafiri kwa muda mrefu niliwauliza mbona hatufiki
kituoni? Wakasema wewe ndiye tulikuwa tunakutafuta, utakiona cha moto,
usipokufa utawasimulia wenzako. Walinipeleka mpaka kwenye msitu, baadaye
ikafahamika kuwa ni Ununio, Tegeta wilayani Kinondoni. Huko walinipiga
sana kisha kunitelekeza katika pori hilo nikiwa nimezimia.
“Baadaye nilipata fahamu nikajikokota kwa taabu hadi kwenye nyumba
moja, nikagonga lakini hawakunifungulia. Nikaenda nyumba ya pili kugonga
napo hawakunifungulia. Nyumba ya tatu nilipoigonga wakanifungulia.
Walinishangaa na kuniuliza kulikoni umelowa damu? Nikawaeleza
kilichonipata.
“Watu hao waliwasiliana na polisi ambao walikuja na kunichukua mpaka
hapa Muhimbili nilipofanyiwa uchunguzi nikahamishiwa Taasisi ya Mifupa
na Mishipa ya Fahamu (Moi). Lakini kule porini wale watekaji walichukua
vitu vyangu kama vile simu mbili na pochi yenye fedha na waliondoka
nazo.”
No comments:
Post a Comment