WAZIRI wa Uchukuzi Dk. Harrison Mwakyembe ameteua kamati ya watu wanne akiwemo Katibu wa Chama cha Marubani Tanzania (PTPA), Kapt. Khalil Iqbal kwa ajili ya kutatua matatizo ya Chama hicho.
Dk. Mwakyembe alifikia hatua hiyo mara baada ya kusikia matatizo yanayokikabili Chama hicho katika kikao kilichofanyika jana kwenye Makao Makuu ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege (TAA).
Kikao hicho kiliwakutanisha Wanachama wa PTPA, TCAA, Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA), na Wasafirishaji wa Anga (TAOA).
Waziri Mwakyembe alisema atafanya kazi na kamati hiyo akishirikiana na Waziri wa Kazi, Mambo ya ndani na Uhamiaji ili kuyatatua mahitaji ya Wataalamu hao.
Alisema utatuzi wa kero zao uko ndani ya uwezo wa Serikali na kwamba hauhitajiki msaada kutoka kwenye Mashirika ya Kimataifa hivyo mpaka kufikia Aprili yatakuwa yameisha.
Katibu Mkuu wa PTPA Khahil Iqbal, alisema tatizo kubwa linalowakabili ni ukosefu wa ajira ambao umeshamiri nchini, huku wataalamu wa fani hiyo wakipaza sauti juu ya tatizo hilo kwa muda mrefu.
Alisema Chama chake kinasikitishwa na ajira zao kuporwa na watu
kutoka mataifa ya nje wanaokuja na kufanya kazi kinyume cha Sheria.
Katibu Mkuu huyo alizungumzia
kwa undani juu ya kuwepo kwa mkanganyiko wa majibu yanayotolewa na idara mbalimbali zinazohusika na ajira katika fani hiyo.
Iqbal alisema kuwa tatizo hilo sugu lililoshamiri na kuathiri thamani ya Marubani wazalendo hapa nchini linakatisha tamaa vijana wenye nia ya kusomea fani hiyo .
Alisema fani hiyo inatakiwa kupewa kipaumbele kutokana na umuhimu wake katika Sekta ya uchukuzi na usafirishaji.
No comments:
Post a Comment